Thariyd: Supu Ya Nyama Kwa Khubz Raqaaiq Chakula Alichokuwa Akipenda Mno Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)

 

Thariyd   Supu Ya Nyama Kwa Mikate Khubz Raqaaiq (Mikate Mepesi Mikavu)

Chakula Alichokuwa Akipenda Mno Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Na Akakifadhilisha kuliko vyakula vingine na soma historia yake upate faida.

 

 

Vipimo

Nyama ya mbuzi ya mifupa - 1 kilo

Kitunguu katakata vidogodogo sana - 3

Nyanya katakata ndogo ndogo au saga - 3

Thomu (saumu, garlic) ilosagwa - 1 kijiko cha kulia

Tangawizi mbichi ilosagwa - 1 kijiko cha kulia

Pilipili mbichi zisage - 2-3 takriban

Lumi (ndimu kavu) - 1

Hiliki ponda au saga - 3

Bizari mchanganyiko - 1 kijiko cha chai

Nyanya paste (tomatoe paste) - 3 vijiko vya kulia

Ndimu au siki ukipenda - kiasi

Chumvi - kiasi

 

Ukipenda ongezea:

Viazi  /mbatata menya katakata vipande - 2

Kusa (aina ya mumunya ya kijani madogodogo) - 3

Bilingani katakata - 1 la kiasi

Koli flower (cauliflower) katakata - ¼

 

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika   Supu Ya Thariyd

  1. Katika sufuria, weka nyama, hiliki, thomu, tangawizi mbichi, pilipili mbichi, bizari, chumvi, lumi (ndimu kavu). Weka katika moto ichemke hadi ikaribie kuiva na supu ibakie.
  2. Weka sufuria ndogo katika moto, kaanga vitungu hadi viwe laini na vigueuke rangi kidogo, tia nyanya kaanga, tia nyanya kopo kaanga.
  3. Mimina mchaganyiko wa nyanya katika supu.
  4. Mimina, viazi, na mboga zote acha ichemke kiasi, usiwivishe sana mpaka zikavurugika.
  5. Onja chumvi, ongezea ndimu au siku ukipenda. Tia hiliki na ongeza bizari ukipenda.

 

6-Kabla ya kupakua, chota nyama na mboga weka upande.

 

7-Katakata mikate ya raqaaiq katika sahani au chombo.

 

 

 

8-Kisha mwagia supu irowane, kisha weka juu yake nyama .  Ukipenda weka supu ya nyama na mboga. Thariyd tayari….

Vidokezo: 

  1. Asili ya thariyd ni supu ya nyama na mikate tu, ila ukipenda kuongezea viazi na mboga kama karoti, koli flawa, bilingani, kusa vile upendavyo kama kwenye picha ifuatayo.
  2. Bonyeza upate upishi wa Khubz Raqaaiq

         Khubz Raqaaiq Mikate Mepesi Mikavu

  1. Khubz raqaaiq huuzwa tayari kwa wingi katika bakeries au viduka vya kuchomwa mikate. Ikiwa hukupata unaweza kutumia mikate mingineyo.

Bis-swihhah wal-hanaa (kula kwa siha na kufurahika)

 

Faida kuhusu Thariyd:

 

Thariyd’, asili yake ni mikate mepesi mikavu inayopikwa kwa unga wa shayiri (talbiynah/barley) na inakatwakatwa na kuchanganywa na supu ya nyama. Kwa hiyo vipimo vyake vikuu ni supu ya nyama na mkate. Mikate hukatwakatwa katika sahani kisha humiminwa supu ya nyama kuirowesha na kuliwa.

 

‘Thariyd’ ni chakula cha zama za Ujaahiliyyah (Kabla ya Uislamu) na baada ya Uislamu, katika kuwakirimu wageni wa heshima. Ni mfano wa biriani katika jamii yetu.

 

Inasemekana kuwa aliyeanza mwanzo kukipika ni Nabiy Ibraahiym ('Alayhis-Salaam) kikaendelea kupikwa na vizazi mpaka kumfikia Haashim Ibn 'Abdil-Manaaf ambaye ni babu wa babu yake Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Aliitwa Haashim kwa kuwa maana ya  هشم   ni kupondaponda au kuvurugavuruga. Naye alikuwa akiwaandalia Mahujaji wa Al-Haram Makkah 'thariyd' akikatakata au kupondaponda mikate kwa ajili ya thariyd. Na ndio maana 'thariyd' kikawa ndio chakula maarufu kwa Maquraysh wa Makkah katika kuwakirimu wageni wao. Kauli nyengine imesema kuwa هشم maana yake ni "kulisha walio na njaa" basi babu yake Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaitwa  هشم الجِياع. Na Allaah Anajua zaidi      

 

Na Imaam Ibn Al-Qayyim amesema: “Thariyd ni mchanganyiko wa nyama na mkate, na nyama ni chakula bora kabisa katika vyakula vinavyoliwa na mkate. Na mkate ni chakula bora kati ya vyakula, kwa hiyo vinapochanganywa (viwili hivi) hakuna tena baada yake kilichokuwa bora kuliko hivyo”  [Zaad Al-Ma’aad (4/271)]

  

Thariyd mpaka hii leo kimekuwa ni chakula  maarufu mno kupikwa khasa pande za Arabuni na pande za Shaam.  Na kwa sasa hupikwa kwa kuongezewa aina mbali mbali za mboga na bizari apendazo mtu.  

 

Hadiyth kadhaa zimetajwa faida na fadhila za thariyd kama ifuatavyo:

 

1-Ubora wa Thariyd umelinganishwa na Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa):

 

عَنْ أَبِي مُوسَى الأَشْعَرِيِّ رضى الله عنه قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم: (( كَمَلَ مِنَ الرِّجَالِ كَثِيرٌ، وَلَمْ يَكْمُلْ مِنَ النِّسَاءِ إِلاَّ مَرْيَمُ بِنْتُ عِمْرَانَ، وَآسِيَةُ امْرَأَةُ فِرْعَوْنَ، وَفَضْلُ عَائِشَةَ عَلَى النِّسَاءِ كَفَضْلِ الثَّرِيدِ عَلَى سَائِرِ الطَّعَامِ ))‏

 

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Muwsaa Al-Ash’ariyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Wanaume wengi wamefikia daraja ya ukamilifu lakini hakuna mwanamke aliyefikia daraja hiyo isipokuwa Aasiyah mke wa Fir'awn, na Maryam bint 'Imraan. Na ubora wa 'Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kwa wanawake wengine ni kama mfano wa ubora wa thariydkwa vyakula vingine.” [Al-Bukhaariy na wengineo]

 

2- Thariyd pamoja na talbiynah (unga wa shayiri) ni chakula kinachopasa apikiwe mgonjwa na aliyefiwa kwa kuwa kinatuliza moyo na kuondosha baadhi ya huzuni.

 

عنْ عَائِشَةَ زَوْجِ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَنَّهَا كَانَتْ إِذَا مَاتَ الْمَيِّتُ مِنْ أَهْلِهَا فَاجْتَمَعَ لِذَلِكَ النِّسَاءُ، ثُمَّ تَفَرَّقْنَ إِلا أَهْلَهَا وَخَاصَّتَهَا ، أَمَرَتْ بِبُرْمَةٍ مِنْ تَلْبِينَةٍ فَطُبِخَتْ ، ثُمَّ صُنِعَ ثَرِيدٌ فَصُبَّتْ التَّلْبِينَةُ عَلَيْهَا ، ثُمَّ قَالَتْ: كُلْنَ مِنْهَا ، فَإِنِّي سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يقُول : ((التَّلْبِينَةُ مُجِمَّةٌ لِفُؤَادِ الْمَرِيضِ، تَذ هبُ بِبَعْضِ الْحُزْنِ))

Imepokelewa kutoka kwa ‘Aaishah mke wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba alikuwa pale mtu alipofariki  katika jamaa zake na wanawake wakakusanyika katika nyumba ya aliyefiwa kisha huondoka isipokuwa jamaa zake na rafiki wa karibu kabisa. Huamrisha ipikwe ‘talbiynah’ (uji wa unga wa sha’iyrah). Kisha ‘thariyd’ (mikate katika supu ya nyama) hupikwa na ‘talbiynah’ humiminwa juu yake. Kisha ‘Aaishah huwaambia wanawake: “Kuleni kwani nimesikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: “Talbiynah inapooza moyo wa mgonjwa na inaondosha baadhi ya huzuni.”  [Al-Bukhaariy katika Kitaab Atw-Twa’aam, Muslim katika Baab As-Salaam]

 

3-Thariyd ni chakula kinachosifika kuwa kina baraka:

 

عن سلمان رضي الله عنه قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم:  ((البَرَكةُ في ثلاثةٍ : في الجماعةِ، والثَّريدِ    والسُّحُور))ِ

Imepokelewa kutoka kwa Salmaan Al-Faarisy (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Baraka zimo katika vitatu: Al-Jamaa’ah (umoja), Ath-Thariyd (Supu ya nyama ilorowanishwa na mkate), na As-Suhuwr (daku).” [Swahiyh Al-Jaami’ (2882), Swahiyh At-Targhiyb (1065)]

 

 

 

 

Share