Nyama Ya Halaal Uchinjaji Wake

 

Nyama Ya Halaal Uchinjaji Wake

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Asalam Alaykum

Kwa jina la Allaah Mwingi rehma mwenye kuneemesha neema ndogo ndogo na mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa.  Swala na salamu zimfikie kipenzi chetu Nabii Muhammad (SAW) na Swahaba zake (RA) na watangu wema mpaka siku ya Kiama.

 

Swala langu ni kama lifuatavyo, na litahusiana na ulaji wa nyama halali huku nchi za Magharibi.

Ni kawaida yangu, kununua nyama moja kwa moja toka katika machinjio, ambayo nyama ile inakua imechinjwa katika misingi na taratibu za kiislam kama ilivyoamrishwa na Allaah na kuwekwa wazi katika hadith za Nabii Muhammad (SAW). Kikawaida ninaweka oda wiki moja au siku tatu kabla ya kwenda kuchukua ile nyama, au kwa upande mmoja au mwingine kama ni mwenye kubahatika unaweza kupita pale machinjioni ukakuta nyama halal. Sasa hii jana, nimekwenda kule buchani kuchukua nyama ambayo tayari nimeshaiwekea oda,  kwa bahati mbaya au nzuri, nyama halal ilikua haipo kwa wakati ule.  Sasa yule mwenye bucha ni Mzungu mkatoliki alinichukua mpaka ndani ya kwenye machinjio, na kufika kule nikapewa kisu nimchinje yule kondoo, kwa kipindi kile bila ya mimi mwenyewe kufahamu kuwa nililoitiwa mule ndani ni nini, kwa kweli nilishtuka kidogo, na mshituko wangu una sababu moja kuu, nayo kwamba mimi binafsi sijawahi kuchinja mnyama kama kondoo, sasa kwangu mimi ilikua ni mtihani kidogo.  Sasa yule Mzungu, anauzoefu wa siku nyingi na ameona waislam wengu ambao wanananua nyama kwake na jinsi ya uchinjaji wake bila ya kumtesa yule mnyama, kwa kumaanisha kile kisu kinapitishwa sehemu gani hasa, kuondoa utesaji wa mnyama wakati wa kutoa roho.

 

Sasa swala ni kama ifuatavyo, je yule Mzungu Mkatoliki, anaweza kunichinjia yule mnyama hali yakuwa mimi mwenyewe nipo, kwa kusoma bismillah, na kutaja jina la Allaa? Naomba munichambulie kutokana na Hadiyth na maamrisho ya Allaah. Maasalam

 

 

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Tunamshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) pamoja na ndugu zetu ambao wamekuwa wakituombea katika kuwafikisha kazi hii nzito na pia wenye kutuuliza maswali tofauti ambayo yanatupatia sisi fursa ya kurejea vitabu na kuongeza elimu yetu zaidi.

 

 

Tafadhali bonyeza kwanza viungo vifuatavyo upate mafunzo ya kuharamishwa kufupisha Thanaa za Allaah ('Azza wa Jalla) na kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

Hukmu Ya Kufupisha Thanaa (Kumtukuza Allaah) Na Kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) Na Maamkizi Ya Kiislam

Al-Lajnah Ad-Daaimah: Haijuzu Kufupisha Kumswalia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Katika Maandishi

Imaam Ibn Baaz: Kufupisha Kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Kwa Mfumo Wowote Haijuzu

 

Kuhusu kuchinja, inaeleweka kuwa Waarabu wapagani walikuwa wakichinja wanavyotaka, bila kutaja jina la Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  na kutumia kifaa chochote wanachotaka. Uislamu ukaweka kanuni ya kumchinja mnyama bila kumsumbua au kumtesa. Ukaweka pia ulazima wa kutaja jina la Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  wakati wa kuchinja. Katika Shariy’ah zake ukafanya vyakula vya watu waliopewa Vitabu kuwa ni halaal ikiwa ni nyama halaal au punje punje. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Aliyetukuka Anasema:

 

الْيَوْمَ أُحِلَّ لَكُمُ الطَّيِّبَاتُ ۖ وَطَعَامُ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ حِلٌّ لَّكُمْ وَطَعَامُكُمْ حِلٌّ لَّهُمْ ۖ  

Leo mmehalalishiwa vizuri. Na chakula cha wale waliopewa Kitabu ni halali kwenu, na chakula chenu ni halali kwao.  [Al-Maaidah: 5]

 

Hii ni Aayah iliyokusanya jamii ya vyakula vyao vya kuchinjwa na vyenginevyo. Hivyo vyote ni halaal maadamu chakula chenyewe si haraam kwetu sisi Waislamu kama mfu, damu, nguruwe na kadhalika.

 

Sasa tukirudi kwa swali lako wewe mwenyewe ulimuona mnyama akichinjwa na ukasema

 

بِسْمِ اللَّهِ

 

BismiLlaahi

 

pamoja na kisu kuwa kikali. Ikiwa hayo yamefanyika basi nyama hiyo inakuwa halaal bila wasiwasi aina yoyote. Masharti haya yako wazi katika machimbuko ya Shariy’ah ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

فَكُلُوا مِمَّا ذُكِرَ اسْمُ اللَّـهِ عَلَيْهِ إِن كُنتُم بِآيَاتِهِ مُؤْمِنِينَ ﴿١١٨﴾

Basi kuleni katika ambavyo limetajwa Jina la Allaah (wakati wa kuchinjwa) mkiwa nyinyi ni wenye kuziamini Aayaat (na hukmu) Zake. [Al-An’aam: 118]

 

Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Kilichochinjwa kwa kumwagwa damu yake na kutajwa jina la Allaah juu yake Kuleni.” [al-Bukhaariy]

 

 

Pia maagizo ya Uislamu ni kuwa unapotaka kumchinja mnyama basi kinoe kisu chako ili umuondolee usumbufu mnyama. Hadiyth ifuatayo inatoa mafunzo ya uchinjaji:

 

عَنْ شَدَّادِ بْنِ أَوْسٍ  رضى الله عنه  قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ  صلى الله عليه وسلم {" إِنَّ اَللَّهَ كَتَبَ اَلْإِحْسَانَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ، فَإِذَا قَتَلْتُمْ فَأَحْسِنُوا اَلْقِتْلَةَ، وَإِذَا ذَبَحْتُمْ فَأَحْسِنُوا اَلذِّبْحَةَ، وَلْيُحِدَّ أَحَدُكُمْ شَفْرَتَهُ، وَلْيُرِحْ ‏ ذَبِيحَتَهُ"} رَوَاهُ مُسْلِمٌ

Kutoka kwa Shaddaad bin Aws (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakika Allaah Ameandika hisani juu yake kila jambo. Mnapouwa, uweni kwa namna nzuri, na mnapochinja chinjeni kwa uzuri. Mmoja wenu akinoe kisu chake na amuondolee mashaka mnyama anayemchinja] [Muslim na wengineo]

 

 

Si hayo, bali mnyama anatakiwa afanyiwe ihsani zaidi kuliko hivyo, kwani Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) amesimulia Hadiyth kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: “Akichinja mmoja wenu mnyama basi amalize upesi upesi.” [Ibn Maajah].

 

Hii ina maana mtu anafaa anowe kisu barabara, amlishe, ampatie maji mnyama na ampapase kabla ya kumchinja.

 

Ibn ‘Abbaas anasimulia kuwa wakati mmoja Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuona mtu akinoa kisu baada ya kumlaza kondoo chini kwa ajili ya kuchinjwa. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimrekebisha kwa kumwambia: “Unataka kumuua mara mbili? Kwa nini hukunowa kisu chako kabla ya kumlaza chini?” [Al-Haakim]

Ikiwa hayo yametimia basi mnyama aliyechinjwa anakuwa halaal.

 

Tunatoa nasaha kwa ndugu zetu sote tuwe ni wenye kuondoa uoga katika kuchinja ili tuweze kufanya wenyewe hata bila ya kusaidiwa na wengine kwani huenda siku moja ukawa ni wewe peke yako na mtarajiwa kuwa unaweza tekeleza shughuli hiyo. Tujiandae, In Shaa Allaah.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

 

Share