Katazo La Swiyaam (Funga) Ayyaamut-Tashriyq: 11, 12, 13 Dhul-Hijjah Na Amali Za Kutenda

 

 

Katazo La Swiyaam (Funga) Ayyaamut-Tashriyq:

Tarehe 11, 12, 13 Dhul-Hijjah  Na Amali Za Kutenda

 

 Alhidaaya.com

 

 

Walio na ada ya kufunga Swawm za Sunnah za Jumatatu na Alkhamiys, au Ayyaamul-Biydhw haitoruhusiwa kufunga tarehe hizo kwani ni katika masiku yaliyokatazwa kufungwa.

  

Ayyaamut-Tashriyq ni masiku ya kula na kunywa; yanayoanzia siku ya pili baada ya ‘Iydul-Adhwhaa ambayo ni tarehe 11, 12 na 13 Dhul-Hijjah. Masiku haya yameitwa At-Tashriyq kwa sababu Hujaji walikuwa wakikata nyama vipande vipande na kuanikwa juani. Na pia imeitwa At-Tashriyq kwa sababu Swalaah ya 'Iyd huswaliwa baada ya kuchomoza jua, na ndio masiku matatu yaliyofuatia yakajulikana kwa jina hilo. Na pi siku hizi hujulikana kwa: ‘Siku za Minaa'

 

Katazo La Swawm Na 'Amali Za Kutenda:

 

 

a) Haifai Swawm (kufunga) katika Ayyamut-Tashriyq: 

 

Haifai kufunga masiku haya ya Tashriyq hata kama mtu alikuwa na mazowea ya Swawm za Sunnah kama vile Jumatatu, Alkhamiys au Ayyaamul-Biydhw. Dalili ya makatazo ni katika Hadiyth ifuatayo:   

 

عن أبي هريرة  أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ بَعَثَ عَبْدَ اللَّهِ بْنَ حُذَافَةَ يَطُوفُ فِي مِنًى أَنْ: ((لَا تَصُومُوا هَذِهِ الْأَيَّامَ فَإِنَّهَا أَيَّامُ أَكْلٍ وَشُرْبٍ وَذِكْرِ اللَّهِ عَزَّ وَجَلَّ))

Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimtuma 'Abdullaah bin Hudhaafah azunguke Minaa na atangaze: "Msifunge siku hizi, kwani hizi ni siku za kula na kunywa na kumdhukuru Allaah ‘Azza wa Jalla.” [At-Twabariy 4: 211]

 

Lakini anaweza mtu kufunga tarehe 14, 15 na 16 kukamilisha siku tatu ili apate fadhila za kufunga siku tatu kila mwezi. [Fataawaa ibn Baaz]

 

 

b) Kumdhukuru Allaah ('Azza wa Jalla) kwa Wingi:

 

Katika siku hizi inampasa Muislamu azidishe kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kama Anavyosema:

((وَاذْكُرُواْ اللّهَ فِي أَيَّامٍ مَّعْدُودَاتٍ)

((Na mdhukuruni Allaah katika siku za kuhesabika.)) [Al-Baqarah: 203]

 

Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) amesema: Siku za kuhesabika ni siku za tashriyq (11, 12, 13 Dhul-Hijjah) na siku maalumu ni siku za kumi za mwanzo za Dhul-Hijjah. [Al-Qurtwubiy: 3.3]

 

Pia kutamka Tabkiyr Al-Muqayyad (Takbiyr za kuthibitika mahali maalumu na nyakati maalumu za kukadirika) imekusudiwa kila baada ya Swalaah ya fardhi. Rejea kiungo kifutacho kupata maelezo na faida:

 

Amali Za Kutenda Ayyaamut-Tashriyq: Tarehe 11, 12, 13 Dhul-Hijjah Na Katazo La Swiyaam

 

 

Ukumbusho Wa Takbiyr Katika Masiku Kumi Na Tatu Ya Dhul-Hijjah: Tarehe 1–13 Dhul-Hijjah

 

 

Siku Kumi Bora Kabisa Za Allaah - 01 - 10 Dhul-Hijjah

 

 

Mdhukuru Allaah Kwa Wingi Na Omba Maghfirah Baada Ya Kutenda Mema Katika Siku Kumi Bora Kabisa Za Allaah

 

12-Dhul-Hijjah: Mafunzo Katika Miezi Ya Hijri: Ya Kutekeleza Na Ya Kujiepusha

 

 

Fataawaa:

 

 

 

 

Wa biLlaahi At-Tawfiyq

 

 

 

Share