Kisa Kisichokuwa Sahihi Kinachonasibishwa Na Swahabi Tha'labah Bin Haatwib Kuhusu Kukataa Kutoa Zakaah

Kisa Kisichokuwa Sahihi Kinachonasibishwa Na Swahabi Tha'labah Bin Haatwib Kuhusu Kukataa Kutoa Zakaah  

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Baadhi ya makhatibu Misikitini na wahadhiri wanamnasibisha    Swahabi Tha’labah bin Haatwib (رضي الله عنه) na Aayah zifuatazo katika Suwrah At-Tawbah zinazotaja kuhusu unafiki:

 

وَمِنْهُم مَّنْ عَاهَدَ اللَّـهَ لَئِنْ آتَانَا مِن فَضْلِهِ لَنَصَّدَّقَنَّ وَلَنَكُونَنَّ مِنَ الصَّالِحِينَ﴿٧٥﴾

Na miongoni mwao wako waliomuahidi Allaah (kuwa): Akitupa katika fadhila Zake, bila shaka tutatoa Swadaqah, na bila shaka tutakuwa miongoni mwa Swalihina.

 

فَلَمَّا آتَاهُم مِّن فَضْلِهِ بَخِلُوا بِهِ وَتَوَلَّوا وَّهُم مُّعْرِضُونَ﴿٧٦﴾

Alipowapa katika fadhila Zake; walizifanyia ubakhili, na wakakengeuka huku wakipuuza.

 

فَأَعْقَبَهُمْ نِفَاقًا فِي قُلُوبِهِمْ إِلَىٰ يَوْمِ يَلْقَوْنَهُ بِمَا أَخْلَفُوا اللَّـهَ مَا وَعَدُوهُ وَبِمَا كَانُوا يَكْذِبُونَ﴿٧٧﴾

Basi Akawapatilizia unafiki katika nyoyo zao mpaka Siku watakayokutana Naye kwa vile walivyomkhalifu kwao Allaah kwa waliyomuahidi, na kwa yale waliyokuwa wakikadhibisha.    [At-Tawbah: 75-77]

 

 

Kikatungwa kisa kirefu kinachosema kuwa Tha’labah  (رضي الله عنه)  ndiye aliyekusudiwa katika Aayah hizo kwamba alikataa kutoa Zakaah kumpa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

Kisa hicho cha uzushi kinadai kuwa:

 

 

“Tha’labah (رضي الله عنه) alikuwa masikini sana na kwamba alikuwa amembatana na Msikitini mpaka akapewa jina la kubandika akaitwa “Njiwa wa Msikiti.” Kisa kinaendela kusema kuwa: “Siku moja Tha’labah alimwambia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) "Niombee du’aa ili Allaah Aniruzuku wanyama wengi sana."  Na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)  akamuombea du’aa na idadi ya kondoo wake ikaongezeka ikambidi atafute nyumba nje ya mji wa Madiynah. Basi kwa kushughulishwa na mali hiyo nyingi ya wanayama, akawa haswali tena isipokuwa baadhi tu ya Swalaah za fardhi. Idadi ya kondoo ikazidi kuongezeka hadi ikabidi asogee nje zaidi ya mji wa Madiynah, na akawa hana tena wakati wa kuswali isipokuwa siku ya Ijumaa tu.  Idadi ya kondoo ikaongezeka tena akaacha kuswali hata hiyo Ijumaa, na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)  alipompeleka mjumbe wake kwa ajili ya kukusanya pesa za Zakaah, Tha’labah akakataa na kusema: "Hakuna Zakaah yenu katika mali yangu, mali hii ni yangu mwenyewe nimeirithi kwa babu zangu." Kisa kinaendelea: “Tha’alabah alihisi vibaya akachukua mali ya Zakaah na kuipeleka kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) naye akaikataa mali hiyo. Na pindi Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alipofariki dunia, Tha’labah alichukua mali ya Zakaah akamuendea Abu Bakr (رضي الله عنه) akamuambia:  "Chukua!" Lakini Abu Bakr (رضي الله عنه) akaikataa akamwambia: "Siwezi kukubali alichokikataa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم).” Akaipeleka Zakaah yake kwa ‘Umar (رضي الله عنه) naye pia akasema: "Wa-Allaahi siwezi kukubali alichokikataa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم).”

 

 

Bainisho La Kutokuthibiti Kisa Hicho:

 

 

Kisa hiki si cha kweli na Isnaad yake ni ya kupangwa, juu ya kuwa kimesimuliwa na baadhi ya ‘Ulamaa kama Ibn Kathiyr na Ibn Jariyr na Ibn Athiyr, na hii ni kwa sababu zifuatazo:

 

 

1-Allaah (سبحانه وتعالى) Hakatai tawbah  ya mja Wake kama Anavyosema:

 

  فَإِن تَابُوا وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَآتَوُا الزَّكَاةَ فَخَلُّوا سَبِيلَهُمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ﴿٥﴾

Lakini wakitubu, na wakasimamisha Swalaah na wakatoa Zakaah, basi iacheni njia yao (huru). Hakika Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [At-Tawbah: 5]

 

 

Na Anasema pia Allaah (سبحانه وتعالى):

 

قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا ۚ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ﴿٥٣﴾

Sema: Enyi waja Wangu ambao wamepindukia mipaka juu ya nafsi zao: Msikate tamaa na rahmah ya Allaah; hakika Allaah Anaghufuria dhambi zote; hakika Yeye Ndiye Mwenye kughufuria, Mwenye kurehemu. [Az-Zumar: 53]

 

 

Aayah zilizotangulia zinatujulisha kuwa hata mshirikina akitubia, Allaah (سبحانه وتعالى) Ataikubali tawbah yake, hivyo basi itakuwaje Allaah Asipokee tawbah ya Muislamu aliyeacha kutoa Zakaah?

 

 

2-Imaam Al-Qurtwuby amesema katika Jaami’ al-Ahkaam:

 

“Tha’labah alipigana vita vya Badr, na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alishuhudia kuwa ni Muislamu wa kweli, kwa hivyo kisa hiki anachonasibishwa nacho si cha kweli.”

 

 

3-Al-Haafidh Al-‘Iraaqiy amesema katika tahakiki ya Hadiyth za kitabu cha Al-Ihyaa ‘Uluwm ad-Diyn cha Ghazaaliy:

 

“Hadiyth hii imetolewa na Atw-Twabaraaniy na Isnaad yake ni dhaifu.”

 

 

 

4-Ibn Hajar amesema katika Al-Iswaabah Fiy Tamyiyz Asw-Swahaabah:

 

“Kisa hiki sidhani kama ni sahihi kwa sababu Tha’labah huyu amepigana vita vya Badr, na Hadiyth Swahiyh ya Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)  inasema kuwa; “Waliopigana vita vya Badr hawaingii Motoni, na kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) aliwaambia; “Fanyeni mtakacho, mumekwisha ghufuriwa madhambi yenu.”

 

Kwa hiyo iweje Tha’labah awe mnafiki?”

 

 

5-Fatwa ya Al-Lajnah Ad-Daaimah imekanusha madai hayo:  Fatwa imetaja:

 

“Kilichopokelewa kuhusu sababu ya kuteremshwa kwa Aayah:

 

وَمِنْهُم مَّنْ عَاهَدَ اللَّـهَ لَئِنْ آتَانَا مِن فَضْلِهِ لَنَصَّدَّقَنَّ وَلَنَكُونَنَّ مِنَ الصَّالِحِينَ﴿٧٥﴾

Na miongoni mwao wako waliomuahidi Allaah (kuwa): Akitupa katika fadhila Zake, bila shaka tutatoa Swadaqah, na bila shaka tutakuwa miongoni mwa Swalihina.

 

kuwa ni Tha’labah bin Haatwib, Isnaad sio sahihi,  na Tha’labah bin Haatwib ni Answaariy aliyeshiriki vita vya Badr, akafariki Shahidi katika vita vya Uhud, kama walivyothibitisha Wanazuoni kadhaa miongoni mwao ni Al-Haafidh Ibn Hajar  (رحمه الله).  

 

 [Fataawaa al-Lajnah ad-Daaimah Lil-Buhuwth al-‘Ilmiyyah wal Iftaa’ (49/26) -      ‘Abdulaziyz bin ‘Abdillaah Aal-Shaykh, Shaykh ‘Abdullaah bin Ghudayaan, Shaykh Swaalih Al-Fawzaan na Shaykh Bakr Abu Zayd]

 

 

6-Imaam Ibn ‘Uthaymiyn  (رحمه الله) amesema kuhusu kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَمِنْهُم مَّنْ عَاهَدَ اللَّـهَ لَئِنْ آتَانَا مِن فَضْلِهِ لَنَصَّدَّقَنَّ وَلَنَكُونَنَّ مِنَ الصَّالِحِينَ﴿٧٥﴾

Na miongoni mwao wako waliomuahidi Allaah (kuwa): Akitupa katika fadhila Zake, bila shaka tutatoa Swadaqah, na bila shaka tutakuwa miongoni mwa Swalihina.

 

na Aayah zinazoendelea kuwa zimeteremshwa kwa ajili ya wanafiki. Na kuwa Habari zisizo sahihi zilizokuwa maarufu zinazodai kuwa Aayah hizo zimeteremshwa kumhusu Tha’labah bin Haatwib katika kisa kirefu ambacho  wafasiri na wahadhiri wengi wanakielezea ni kisa dhaifu hakina usahihi. Na pia kisa kinapingana na lile linalojulikana katika Dini kuwa ni jambo lilothibiti na linapaswa kufahamika kuwa Allaah (سبحانه وتعالى)  Anapokea Tawbah ya mwenye kutubia kwa dhambi yoyote ile atakayoifanya.”

[Sharh Uswuwl fiy Tafsiyr - Ibn ‘Uthaymiyn]. 

 

 

 

 

Share