Waislamu Wanapopata Madaraka Huwa Na Khiyana; Hawasaidii Wenzao

 

Waislamu Wanapopata Madaraka Huwa Na Khiyana; Hawasaidii Wenzao

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali:

 

Kwa Nini Waislam Waliowengi (nguzo Tano Wanazingatia) Wanapopata Madaraka Angalau Ya Usimamizi Tu (supervisory) Achilia Mbali Ngazi Za Juu, Wanakuwa Na Hiyana Na Hasadi Za Roho  Juu Ya Waislamu Wenzao.

 

Tofauti Na Dini Nyingene Ambapo Wanakuwa Na Hata Mtandao Wa Kusaidiana? Nini Hukumu Ya Watu Kama Hawa?

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Hakika hayo uliyoyasema ni kweli kabisa na hilo limekuwa tatizo sugu katika jamii yetu. Imekuwa Muislamu aliye na madaraka aina yoyote anamfadhilisha asiyekuwa Muislamu kumpatia nyadhifa mbali mbali kuliko Muislamu aliye na uzoefu na elimu sawa.

 

 

Muislamu kwa njia yoyote ile hawi hasidi wala hafanyi hiyana kabisa. Kitabia Muislamu anawapendelea kheri watu wote – Waislamu na wasiokuwa Waislamu kwani hawa wa pili ni wanaadamu nao wanahitaji kuvutwa kwa Uislamu ili wawe wanaadamu wazuri na wema zaidi. Muislamu hapendi tabia ya husda, kwani hiyo ni kupinga ugawaji kwa Allaah Aliyetukuka na fadhila Zake kwa viumbe Wake. Anasema Aliyetukuka:

أَمْ يَحْسُدُونَ النَّاسَ عَلَىٰ مَا آتَاهُمُ اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ ۖ

Au wanawahusudu watu (Nabiy Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم na Waumini) kwa yale Aliyowapa Allaah katika fadhila Zake? [An-Nisaa: 54].

 

 

Ama hiyana ni alama moja ya unafiki kwa mujibu wa Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama ilivyonukuliwa na al-Bukhaariy na Muslim.

 

 

Allaah Aliyetukuka Amehimiza sana watu na hasa Waislamu wasaidiane katika wema. Wema ulio bora wakati huu ni kumsaidia nduguyo kupata kazi na pato la halali. Allaah Aliyetukuka Anasema:

وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَىٰ ۖ وَلَا تَعَاوَنُوا عَلَى الْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ

Na shirikianeni katika wema na taqwa, na wala msishirikiane katika dhambi na uadui. Na Mcheni Allaah;  [Al-Maaidah: 2].

 

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Mnusuru (na msaidie) ndugu yako akiwa amedhulumu au amedhulumiwa". Akaulizwa: “Aliyedhulumiwa tunafahamu, je huyu aliyedhulumu tumsaidie vipi?” Akasema: “Msaidie asidhulumu” [Al-Bukhaariy].

 

 

Mbali na kusema ya kwamba Uislamu unapinga sana sifa na tabia ya hiyana na hasadi na kuhimiza sana kusaidiana na kujenga udugu, inatakiwa tufahamu kuwa Uislamu unahimiza sana uadilifu na usawa. Haitokuwa sawa Kiislamu kwa Muislamu kumpatia kazi Muislamu kwa kuwa tu ni Muislamu japokuwa hana uzoefu wa kazi au hakusoma. Allaah Aliyetukuka Anasema:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُونُوا قَوَّامِينَ لِلَّـهِ شُهَدَاءَ بِالْقِسْطِ ۖ وَلَا يَجْرِمَنَّكُمْ شَنَآنُ قَوْمٍ عَلَىٰ أَلَّا تَعْدِلُوا ۚ اعْدِلُوا هُوَ أَقْرَبُ لِلتَّقْوَىٰ ۖ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ ﴿٨﴾

Enyi walioamini!  Kuweni wasimamizi madhubuti kwa ajili ya Allaah mkitoa ushahidi kwa uadilifu. Na wala chuki ya watu isikuchocheeni kutokufanya uadilifu. Fanyeni uadilifu; hivyo ni karibu zaidi na taqwa. Na mcheni Allaah; hakika Allaah ni Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika kwa yale myatendayo.  [Al-Maaidah: 8].

 

Pia,

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُونُوا قَوَّامِينَ بِالْقِسْطِ شُهَدَاءَ لِلَّـهِ وَلَوْ عَلَىٰ أَنفُسِكُمْ أَوِ الْوَالِدَيْنِ وَالْأَقْرَبِينَ ۚ إِن يَكُنْ غَنِيًّا أَوْ فَقِيرًا فَاللَّـهُ أَوْلَىٰ بِهِمَا ۖ فَلَا تَتَّبِعُوا الْهَوَىٰ أَن تَعْدِلُوا ۚ وَإِن تَلْوُوا أَوْ تُعْرِضُوا فَإِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرًا ﴿١٣٥﴾

Enyi walioamini! Kuweni wenye kusimamisha uadilifu mtoapo ushahidi kwa ajili ya Allaah japokuwa ni dhidi ya nafsi zenu au wazazi wawili, au jamaa wa karibu. Akiwa tajiri au maskini Allaah Anawastahikia zaidi. Basi msifuate hawaa mkaacha kufanya uadilifu. Na mkiupotoa au mkikanusha basi hakika Allaah kwa yale myatendayo ni Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika. [An-Nisaa: 135].

 

 

Hapa Aayah zinazungumzia kuhusu ushahidi kwa wenye kutoa ushahidi hawafai kupendelea. Hivyo hivyo, katika kutekeleza mambo mengine kama kuajiri ni lazima mtu Muislamu awe muadilifu katika kutekeleza wadhifa wake.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

Share