Manufaa Na Matatizo Katika Ndoa

 

Mume Na Mke

 

Imefasiriwa Na: Ummu Ahmad

 

Alhidaaya.com

 

 

Manufaa Katika Ndoa

 

1.    Kupata kizazi ambacho kwanza kitasaidia katika ujengaji wa jamii, pili kueneza jinsia ya watu wa kila kabila au mataifa mbali mbali, na kubwa zaidi ni kuongeza idadi ya kizazi cha jamii ya kiislamu.

 

2.    Kumridhisha Allaah (Subhaanahu Wa Ta'aalaa) na Nabiy Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwa   kueneza idadi ya wafuasi wa dini ya Kiislamu.

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema katika hadithi sahihi:

 

"Oeni wake wema muwapendao na wataowapatia kizazi chema, kwani siku ya Qiyaamah nitajivunia ukubwa wa umati wangu." [Ahmad]

 

3.    Kupata baraka za mtoto mwema ambaye atakayemsomea dua mzee wake (atakapofariki). Maneno haya yamethibitishwa na Hadiyth maarufu inayosema kuwa:

 

"Binaadamu anapokufa, basi ‘amali zake nzuri hukatika au humalizika, isipokuwa mambo matatu makuu nayo ni: Sadaka yenye kuendelea, Elimu yenye kunufaisha na Mtoto mwema atakayemuombea du’aa mzee/wazee wake." [Riyadhus-Swaalihiyn]

 

Faida nyenginezo zipatikanazo katika ndoa ni:

 

4.    Kinga kutokana na Shaytwaan katika mambo yanayopelekea au yanokaribisha tendo la zinaa.

 

5.    Utulivu wa akili na moyo na kuwa na urafiki ambao hupelekea mapenzi na huruma baina ya mume na mke.

 

6.     Kunganisha kwa Familia za pande mbili za ukeni na uumeni.

 

7.     Kusaidiana katika kazi za nyumba (sio kumuachia mke kazi zote za ndani ya nyumba). Hii ni tabia ambayo ingalipo kwa baadhi ya akina baba. Kwa vile tabia hii imekuzwa na utamaduni wetu wa tunakotoka, kinyume kabisa na maamrisho ya dini yetu ya Kiislamu yanavyotuagiza.

 

8.    Kuelimishana majukumu ya kifamilia. Pia kuweka bidii na kuwa tayari   kuihami na kuitunza familia. Na vile vile kuishughulikia na kuitimizia mahitaji yake yakiwa ama ya (kimwili, kimavazi, kisiha, kimawazo na kiroho) na kustahamiliana pale panapotokea kutoelewana.

 

 

Matatizo Katika Ndoa 

 

Wakati huo huo kuna matatizo yanayopatikana katika ndoa ambayo inabidi tuzingatie na kujichunga ili tuepukane na matatizo hayo. Nayo ni kama yafuatayo:

 

a.    Kushindwa kuchuma pato la halali, ambapo itapelekea kutafuta njia ambazo si za halali za kimapato ili kuweza kutimiza mahitaji ya familia. Haimfalii mke kumlazimisha mumewe ampatie mambo yaliyo nje ya uwezo wa mume. Na tuwaige wanawake wema waliopita, ambao kila waume zao wakitoka kwenda kwenye shughuli zao za kutafuta riziki, wakiwausia kuwa wasirejee na chochote cha haramu. Wakiwanasihi waume zao kuwa ni bora wastahamili kwa njaa ya hapa duniani kwani adhabu ya kesho Aakhirah sio ya kustahamilika.

 

b.   Kushindwa kutimiza majukumu ya ndoa, na hasa kutimiza haki za mke au kutoweza kustahamili kwenye wakati mgumu wa kimaisha. Na tuwe makini katika suala hili kwani kuna ile dhana ya kuwa ndoa ni jambo la kujionyesha tu kuwa fulani kaoa au kaolewa.

 

"Kila mmoja kati yenu ni mchungaji, na kila mmoja kati yenu atapaswa kuulizwa ya juu ya kile anachokichunga. Mume ni mchungaji wa familia yake, naye atapaswa kuulizwa juu ya anaowachunga. Na mke ni mchungaji wa nyumba ya mumewe, naye pia atapaswa kuulizwa juu ya anachokichunga. Hivyo basi, kila mmoja kati yenu ni mchungaji ambaye atapaswa kuulizwa juu ya anaowachunga" [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

c.     Kuacha kushughulikia mambo muhimu ya kidini, kwa mfano kutumia muda mwingi katika mambo ya anasa za kidunia kama vile kuangalia Televisheni, kwenda kwenye shehere za kuzaliwa mtoto au kwa kutimiza umri fulani wa mtoto (birthday party), badala ya kutumia muda huo kwa kutengeneza maisha ya Aakhirah ambayo ndio ya milele. Kama tunavyotanabahishwa kwenye Quraan Tukufu:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تُلْهِكُمْ أَمْوَالُكُمْ وَلَا أَوْلَادُكُمْ عَن ذِكْرِ اللَّـهِ ۚ وَمَن يَفْعَلْ ذَٰلِكَ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ﴿٩﴾

Enyi walioamini! Zisikupurukusheni mali zenu na wala watoto wenu mkaacha kumdhukuru Allaah. Na yeyote atakayefanya hivyo basi hao ndio waliokhasirika. [Al-Munaafiquun 63: 9]

 

Mwandishi wa mada hii amemalizia kwa kusema kuwa:

Dinaar (pesa) unayoitumia katika njia za Allaah (Subhaanahu Wa Ta'aalaa), dinaar unayoitumia kumuachia huru mtumwa, dinaar unayoitumia katika kutoa sadaka kwa mtu anayehitaji sadaka hiyo, basi hakuna Dinaar iliyo bora kati ya dinaar hizo ila ile unayoitumia kwa ajili ya familia yako.

 

Msemo huu una maana ya kwamba hakuna jambo muhimu katika mafundisho ya kijamii ya Kiislamu kama lile la kuzishughulikia familia zetu kwa mali na hali, ili kuweza kupata umma mwema na bora duniani na Aakhirah.

 

Mwishoni tunamuomba Allaah (Subhaanahu Wa Ta'aalaa) Atupe wake, waume na watoto watakaotupa kitulizo cha macho na nyoyo zetu, na Atufanye tuwe viongozi wazuri wa familia zetu. Ee Allaah Mpe Bwana Wetu Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Baraka na Amani na Familia yake pamoja pia na Swahaba wake. "Aamiyn"

 

 

Share