Hikma Ya Ruhusa Ya Ukewenza

 

Hikma Ya Ruhusa Ya Ukewenza

 

 Alhidaaya.com

 

Kuna sababu nyingi za kibinafsi, kimaadili, kiuchumi na kijamii zinazoonesha kuwa wakati mwengine kuoa mke zaidi ya mmoja ni jambo lisilobudi.

 

Kabla ya kulieleza jambo hili ni vyema tukaelewa nini maana hasa ya ndoa (Nikaah) katika Uislam. Ndoa ni mkataba ('Aqd) wa hiari kati ya mume na mke wa kuishi pamoja kwa wema na upendo kufuatana na masharti na taratibu zilizowekwa na sheria ya Kiislam.

 

Kwani umuhimu wa ndoa kwa mtazamo wa Uislam ni jambo lililokokotezwa sana kutokana na umuhimu wake katika kujenga na kuendeleza jamii. Kama Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Alivyosema katika kitabu Chake kitukufu cha Qur-aan Suwrah Al-Nuwr, Aayah ya 32:

وَأَنكِحُوا الْأَيَامَىٰ مِنكُمْ وَالصَّالِحِينَ مِنْ عِبَادِكُمْ وَإِمَائِكُمْ ۚ إِن يَكُونُوا فُقَرَاءَ يُغْنِهِمُ اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ ۗ وَاللَّـهُ وَاسِعٌ عَلِيمٌ ﴿٣٢﴾

Na waozesheni wajane miongoni mwenu na walio Swalihina kati ya watumwa wenu wanaume na wajakazi wenu. Wakiwa mafakiri Allaah Atawatajirisha katika fadhila Zake. Na Allaah Mwenye Wasaa, Mjuzi wa yote. [An-Nuwr: 32]

 

Tafsiri yake ni kwamba:

Na waozesheni wajane miongoni mwenu (waungwana) na walio wema katika watumwa wema (wanaume) na wajakazi wenu.

 

Pia vile vile Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema katika Suwrah An-Nisaa, Aayah ya 3:

 فَانكِحُوا مَا طَابَ لَكُم مِّنَ النِّسَاءِ مَثْنَىٰ وَثُلَاثَ وَرُبَاعَ ۖ

Basi oeni waliokupendezeni katika wanawake wengine; wawili au watatu au wanne. Lakini mkikhofu kuwa hamtoweza kufanya uadilifu, basi mmoja tu. [An-Nisaa: 3]

 

Tafsiri:

Oeni walio wazuri miongoni mwa wanawake wawili, watatu na wanne, ikiwa munaogopea uadilifu kwa wanawake hao basi oeni mmoja.

 

Hii inadhihirisha kuwa tendo la ndoa lina umuhimu mkubwa katika jamii, ambazo zimetubainishia kuwa ndoa ni ngao ya kujikinga na kitendo kichafu cha zinaa.

 

Allaah Amehalalisha ndoa na kuitilia mkazo kwa wale wenye uwezo kama tunavyojifunza katika Aayah zifuatazo: 

وَأُحِلَّ لَكُم مَّا وَرَاءَ ذَٰلِكُمْ أَن تَبْتَغُوا بِأَمْوَالِكُم مُّحْصِنِينَ غَيْرَ مُسَافِحِينَ ۚ 

Na mmehalalishiwa wengineo wasiokuwa hao, mtafute (kuwaoa) kwa mali zenu mkijistahi pasi na kuzini. [An- Nisaa:24]

 

Pia katika Suwrah ya [Al-Maaidah: 5]

الْيَوْمَ أُحِلَّ لَكُمُ الطَّيِّبَاتُ ۖ وَطَعَامُ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ حِلٌّ لَّكُمْ وَطَعَامُكُمْ حِلٌّ لَّهُمْ ۖ وَالْمُحْصَنَاتُ مِنَ الْمُؤْمِنَاتِ وَالْمُحْصَنَاتُ مِنَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ مِن قَبْلِكُمْ إِذَا آتَيْتُمُوهُنَّ أُجُورَهُنَّ مُحْصِنِينَ غَيْرَ مُسَافِحِينَ وَلَا مُتَّخِذِي أَخْدَانٍ ۗ وَمَن يَكْفُرْ بِالْإِيمَانِ فَقَدْ حَبِطَ عَمَلُهُ وَهُوَ فِي الْآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ ﴿٥﴾ 

Leo mmehalalishiwa vizuri. Na chakula cha wale waliopewa Kitabu ni halali kwenu, na chakula chenu ni halali kwao. Na wanawake walioimarisha sitara (wasiozini) miongoni mwa Waumini wanawake na wanawake walioimarisha sitara miongoni mwa wale waliopewa Kitabu kabla yenu; mtakapowapa mahari yao mkijistahi bila ya kuwa maasherati wala kuchukua hawara. Na yeyote atakayekanusha iymaan; basi kwa yakini imeporomoka ‘amali yake naye Aakhirah atakuwa miongoni mwa waliokhasirika. [Al-Maaidah: 5]

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kwamba: 

"Enyi vijana na atakaeweza kati yenu gharama za ndoa (mahari) na aoe."

 

Pia katika hadithi nyengine amesema:

 

'Abdullaah bin Mas'uud (Radhwiya Allaahu 'anhu) ameeleza kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema “Enyi kongamano la vijana na aoe yule alie na uwezo miongoni mwenu, hakika kunainamisha macho (na matamanio) na kuhifadhi tupu (humzuilia mtu na zinaa)na asiyeweza kuoa na afunge, Hakika funga hukata matamanio. [Al-Bukhaary na Muslim].

 

Pia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

"Mmoja wenu atakapomuona mwanamke kisha akamtamani, hana budi kumuendea mkewe kwani ana kile alichonacho huyo mwanamke aliyemtamani." [At-Tirmidhy]

 

Ndoa ni Sunnah lakini itakuwa wajibu kwa mwenye kuweza na akawa anayo matamanio na anaogopa kutumbukia katika zinaa.

 

Katika suala la kuoa mke zaidi ya mmoja ni jambo lisilo budi, kwa kuangalia mifano kadhaa kama vile:

 

a)        Kama mke ni tasa

Mfikirie mwanamme ambae amehakikisha kuwa mkewe ni tasa na bado ana    hamu ya kupata mtoto atakayekuwa mrithi wake. Katika hali hii mwanamme huyu atafanya mojawapo katika haya yafuatayo:

 

i.        Atakaa na kusononeka kwa kukosa mtoto katika maisha yake yote au

ii.       Atamuacha huyo mwanamke asiyezaa ili aoe mwengine anayezaa au

iii.   Atatembea na mwanamke mwengine nje ya ndoa ili ampatie watoto, japo kisheria si watoto wake au

iv.  Ataendelea kukaa na mkewe kwa mapenzi na furaha kisha aoe mke mwengine atakaemzalia watoto ambao watakuwa wake kisheria.

 

Utakuta uchaguzi wa kuoa mke wa pili ndio ulio bora kabisa. Wengi katika jamii ya Kiislam wameoa mke wa pili kwa sababu hii.

 

b)      Kama mke ana maradhi ya kudumu

Mfikirie tena mwanamme ambaye mkewe ana ugonjwa wa kudumu kwa kiasi kwamba hana uwezo wa kutekeleza majukumu yake kama mke bila ya shaka mwanamme huyu atafanya mojawapo kati ya yafuatayo:

 

i.        Atajizuia na matamanio yake ya kimwili kwa muda wote wa maisha yake uliobakia au

ii.    Anaweza kumtaliki, mkewe mgonjwa wakati ambapo anahitajia uangalizi, huruma na mapenzi ya hali ya juu kutoka kwake, ili aoe mke mwengine atakayetosheleza mahitaji yake au

iii.     Anaweza kubakia na mkewe mgonjwa na kufanya uzinifu na wanawake wengine nje au

iv.     Ataoa mke wa pili atakayemsaidia kumuhudumia mkewe mgonjwa

 

Hebu tuzijadili hizi hatua tatu (3) kwa mtazamo wa mafundisho ya Uislam

 

Hatua ya kwanza: Inakwenda kinyume na umbile la mwanaadamu. Allaah Analifahamu fika umbile la mwanaadamu ya haja yake ya kutosheleza matamanio ya jimai na Ameweka utaratibu mzuri wa sheria ya ndoa wa kutosheleza mahitajio haya ya kimaumbile.

 

Hatua ya pili: Ni kinyume kabisa na ubinaadamu, kumuacha mke kwa sababu amekuwa mgonjwa badala ya kumuhudumia kwa upendo na huruma ni kinyume kabisa na utu. Utaona kuwa hatua ambayo inamuwezesha mume huyu aendelee kumtunza mkewe kwa huruma na wakati huo huo aweze kutosheleza mahitajio yake ya kimaumbile kwa utaratibu mzuri wa heshima ni kuoa mke wa pili

 

c)       Wanawake Wajane

Wajane ni wanawake waliofiwa na waume zao, hakuna jamii isiyokuwa na wajane na idadi yao huongezeka zaidi wakati wa vita ambapo wanaume wengi huuliwa vitani. Je, wanawake hao warudishwe kwa wazazi au walezi wao au kukaa hivyo hivyo bila ya kukidhi matashi yao ya kimaumbile mpaka wazeeke, au waachiwe wawe malaya na kuitokomeza jamii kutokana na matatizo mbali mbali yanayosababishwa na zinaa? Kwa vyovyote vile, njia pekee ya kuwahifadhi wanawake na watoto wao ni hii ruhusa ya kuoa mke zaidi ya mmoja hadi wanne, kwa kufuata masharti yaliyowekwa.

 

d)      Wanawake Wakiwa Wengi Katika Jamii

Inatokezea katika jamii nyingi wanawake kuwa wengi zaidi kuliko wanaume. Katika jamii hizi, kama tutaweka sheria ya mume mmoja – mke mmoja kama wanavyodai watetezi wa usawa wa wanawake. Wanawake watakaokosa wa kuwaoa watakwenda wapi? Watafanyaje ili kukidhi matashi yao ya kimaumbile?

 

Je, kama watazuiliwa mpaka wazeeke huoni hii itawaathiri kimwili, na kifikra na kuwafanya wasiwe watu wenye manufaa katika jamii? Nani watakaotoa hifadhi kwa wanawake hawa kiuchumi na kimaadili? Ilivyo katika maadili ya kibinaadamu, kila mwanamke wa kawaida anahitajia kuwa na mwanamme anayempenda na kumuhurumia, hivyo wanawake hawa watakapokosa waume wa ndoa watafanya kila hila za kuwashawishi wanaume kwa kuwawekea mitego mbali mbali kama vile kujipitisha mbele yao wakiwa wamejipodoa na kujiremba, kutembea mbele yao uchi, kuzurura kwenye majumba ya sinema n.k. ambayo itawanasa na kuwatumbukiza katika zinaa.

 

e)      Kuhifadhi jamii na zinaa

Matamanio ya jamii ni katika maumbile na hayaepukiki katika Uislam. Ndoa ni jambo lililokokotezwa sana kutokana na umuhimu wake katika kujenga na kuendeleza jamii. Ndoa kwa mtazamo wa Uislam inatarajiwa:

 

1.     Kuhifadhi jamii na zinaa;

2.     Kuendeleza kizazi cha mwanaadamu kwa   utaratibu mzuri;

3.     Kujenga mapenzi, huruma na ushirikiano katika familia;

4.     Kukuza udugu na ushirikiano katika jamii.

 

Kwa hivyo kuoa mke zaidi ya mmoja ni jambo lisilo budi kwa mwanaadamu kama tulivyoeleza katika mada yetu hii ya ndoa.

 

Wa Allaahu A'alam

 

 

Du’aa Ya Mada Husika

Ee Allaah, hakika mimi nakuomba kheri ya (mke) huyu, na kheri ya maumbile Uliyomuumba nayo, na najilinda Kwako na shari yake na shari ya maumbile Uliyomuumba nayo.

 

Share