Haki Za Mume Na Mke

 

Haki Za Mume Na Mke

 

Imekusanywa na: Ummu Iyyaad

 

Alhidaaya.com

 

 

Haki za mume na mke zimedhihirishwa katika Qur-aan na Sunnah. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

وَلَهُنَّ مِثْلُ الَّذِي عَلَيْهِنَّ بِالْمَعْرُوفِ وَلِلرِّجَالِ عَلَيْهِنَّ دَرَجَةٌ وَاللّهُ عَزِيزٌ حَكُيمٌ

Nao wake wana haki kama ambayo (ya waume zao) iliyo juu yao kwa mujibu wa shariy’ah. Na wanaume wana daraja zaidi juu yao. [Al-Baqara: 228]

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) akasema katika Hijjah ya kuaga aliposimama kuwahutubia Swahaba:

((يآ أيُّهَا النَّاسُ إِنَّ لِنِسَائِكُمْ عَلَيْكُمْ حَقاً وَلَكُمْ عَلَيْهِنَّ حَقّ)) أبو داود

"Ee nyie watu, hakika nyinyi mna haki juu ya wake zenu na wake zenu wana haki juu yenu,"  [Abu Daawuud]

 

Zifuatazo ni haki zinazowahusu wote wawili; mke na mume katika kuamiliana:    

 

1-Ukweli

Mke na mume wawe ni wakweli baina yao kwa kauli na vitendo. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آَمَنُوا اتَّقُوا اللَّهَ وَكُونُوا مَعَ الصَّادِقِينَ

Enyi mlioamini! Mcheni Allaah na kuweni pamoja na wakweli. [At-Tawbah: 11]

 

2-Mapenzi, Huruma Na Utulivu.

Kila mmoja amdhihirishie mwenziwe mapenzi, na wawe na huruma baina yao katika shida na matatizo mpaka iwe kila mmoja awe ni kutulizo cha mwenziwe wakati wa dhiki. Allaah (Subhanaahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا لِّتَسْكُنُوا إِلَيْهَا وَجَعَلَ بَيْنَكُم مَّوَدَّةً وَرَحْمَة ًإِنَّ فِي ذَلِكَ لَآ يَاتٍ لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ

Na katika Aayaat Zake ni kwamba Amekuumbieni kutokana na nafsi zenu (jinsi moja) wake ili mpate utulivu kwao; na Amekujaalieni baina yenu mapenzi na Rahmah. Hakika katika hayo bila shaka (kuna) Aayah kwa watu wanaotafakari.[Ar-Ruwm 30: 21]

 

3-Amana, Uaminifu Na Kutumiza Ahadi:

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amewasifu na kuwaahidi Jannah wanaotimiza amana na ahadi zao:

وَالَّذِينَ هُمْ لِأَمَانَاتِهِمْ وَعَهْدِهِمْ رَاعُونَ ﴿٨﴾

Na ambao amana zao na ahadi zao wanazichunga. [Al-Muuminuwn: 8]

 

Kuweko uaminifu kutazuia dhana mbaya au kutiliana shaka: 

فَإِنْ أَمِنَ بَعْضُكُم بَعْضًا فَلْيُؤَدِّ الَّذِي اؤْتُمِنَ أَمَانَتَهُ وَلْيَتَّقِ اللّهَ رَبَّهُ

Na ikiwa mmoja wenu amewekewa amana na mwengine, basi airudishe yule ambaye ameaminiwa amana ya mwenzake; na amche Allaah, Rabb wake;  [Al-Baqarah: 283]

 

4-Tabia Njema

Wawe na tabia njema katika kauli na matendo ili iwepo heshima baina yao:   

وَعَاشِرُوهُنَّ بِالْمَعْرُوفِ

Na kaeni nao kwa wema. [An-Nisaa: 19]

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) akausia:

 

"Nakuusieni kuwafanyia wema wanawake"  [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

5-Kuhifadhiana Siri

Haiwapasi wote kutoleana siri zao au kutoa aibu zao nje:

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema: "Watu watakaokuwa katika hali mbaya kabisa mbele ya Allaah Siku ya Qiyaamah ni mwanamme anaekwenda kwa mke wake na mke kwenda kwa mume wake kisha (mmojawao) akapita kutoa siri yake". [Muslim]

 

Haki hizo zitakapotimizwa kwa mume na mke, itakuwa ni kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

وَلاَ تَنسَوُاْ الْفَضْلَ بَيْنَكُمْ إِنَّ اللّهَ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ

Na wala msisahau fadhila baina yenu. Hakika Allaah kwa myatendayo ni Baswiyr (Mwenye kuona). [Al-Baqarah: 237]

 

Haki Za Mke Kutoka Kwa Mume: 

 1-Ni wajibu wa mume kumlisha mkewe kumvisha na kumtimizia mahitaji yake.  

 

2-Mume ana haki kumfunza adabu mke anapohisi mke anamuasi. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

وَاللاَّتِي تَخَافُونَ نُشُوزَهُنَّ فَعِظُوهُنَّ وَاهْجُرُوهُنَّ فِي الْمَضَاجِعِ وَاضْرِبُوهُنَّ فَإِنْ أَطَعْنَكُمْ فَلاَ تَبْغُواْ عَلَيْهِنَّ سَبِيلاً إِنَّ اللّهَ كَانَ عَلِيًّا كَبِيرًا

Na wale (wanawake) ambao mnakhofu uasi wao, basi waonyeni na (wakiendelea uasi) wahameni katika malazi (vitanda) na (mwishowe wakishikilia uasi) wapigeni. Wakikutiini, basi msitafute dhidi yao njia (ya kuwaudhi bure). Hakika Allaah ni ‘Aliyyan Kabiyraa (Mwenye Uluwa – Mkubwa wa dhati, vitendo na sifa). [An-Nisaa: 34]

 

Aayah hiyo inataka maelezo kidogo kwani baadhi wa wanaume wameifahamu sivyo kuhusu: ((wahameni katika malazi (vitanda) na (mwishowe wakishikilia uasi) wapigeni)).

Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) na wengineo wamesema: "Aayah imemaanisha kupiga mpigo usio mkali" (yaani mpigo hafifu) Al-Hasan Al-Baswriy kasema: "Ina maana mpigo usio wa nguvu".

 

Wanavyuoni wamefafanua kuhusu kauli hiyo ifautavyo:

 

i)             Kwanza mume amnasihi mkewe bila ya kumshutumu au kumuonea au kumtia aibu kwa watu. Mke atakapomtii mumewe, itosheleze kuwa matatizo yamekwisha.

 

ii)         Atakapoendelea mke kutokumtii mume wake, basi mume ajitenge naye kitandani, yaani asiwe analala nae kwa muda wala asiseme nae mpaka mke ahisi vibaya na atambue kuwa mumewe amamekasirikia. Pindi mke akikubali makosa yake, yaishe matatizo na warudiane katika hali yao ya kawaida.

 

iii)           Ikiwa bado mke hana utiifu, hapo mume anaweza kufuata amri hiyo ya kipigo. Lakini sio kumpiga kwa nguvu bali kama alivyosema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth ifuatayo:

عن جابر (رضي الله عنه) عن النبي صلى الله عليه وسلم: أنه قال في حجة الوداع: ((واتَّقُوا اللهَ في النِّساءِ، فإنهن عندكم عَوَانٌ، ولكم عليهن ألا يُوطِئْنَ فُرُشكم أحدا تكرهونه، فإن فَعَلْن فاضربوهن ضَرْبا غير مُبَرِّح، ولهن رزْقُهنَّ وكِسْوتهن بالمعروف))

Kutoka kwa Jaabir (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema katika Hijja ya kuaga: "Mcheni Allaah kuhusu wanawake kwani wao ni wasaidizi wenu.  Mnayo haki juu yao kuwa wasimuruhusu mtu msiyempenda kukanyaga zulia lenu. (kuingia katika nyumba) Lakini wakifanya hivyo, mnaruhusiwa kuwatia adabu ndogo. Wao wana haki kwenu kwamba muwatimizie matumizi yao na nguo kwa njia ya kuridhisha".[Muslim]

 

3-Ni wajib wa mume kumpatia mafunzo ya Dini mke wake ikiwa mke hakujaaliwa kupata elimu ya Dini yake. Mume amfundishe mwenyewe, na pindi asipoweza, amruhusu mke kuhudhuria darasa kwa sababu ni muhimu kwake apate kujifunza yanayopasa kama ‘Aqiydah na Tawhiyd na ajiepushe na shirki. Pia ajifunze Fiqhi na yote yanayohusiana na Dini yake, aweze kutekeleza ibaada zake sawasawa na pia apate kuitakasa nafsi yake na aweze kujiepusha na maasi na aweze kulea watoto wake. Kwa ujumla aihami familia yake na Moto wa Jahannam.  Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anaamrisha hivyo:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ عَلَيْهَا مَلَائِكَةٌ غِلَاظٌ شِدَادٌ لَّا يَعْصُونَ اللَّـهَ مَا أَمَرَهُمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ ﴿٦﴾

Enyi walioamini! Jikingeni nafsi zenu na ahli zenu na moto ambao kuni zake ni watu na mawe; juu yake wako Malaika washupavu hawana huruma, shadidi, hawamuasi Allaah kwa yale Anayowaamrisha na wanafanya yale wanayoamrishwa. [At-Tahriym: 6]

 

4-Ni wajibu wa mume kumrekebisha mkewe anapokosea kufuata Shariy’ah za Dini; mfano mke asipotimiza hijaab. Vile vile asimwachie kuchanganyika na wanaume isipokuwa ambao kaharimishwa nao kuolewa. 

 

5-Ni wajibu wa mume kumhifadhi mke kwa kila njia. Mume awe ndio mlinzi na msimamizi wa mambo yake na ndiye mwenye majukumu ya kumhudumia:

الرِّجَالُ قَوَّامُونَ عَلَى النِّسَاءِ بِمَا فَضَّلَ اللَّـهُ بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ وَبِمَا أَنفَقُوا مِنْ أَمْوَالِهِمْ ۚ

Wanaume ni wasimamizi juu ya wanawake kwa kuwa Allaah Amefadhilisha baadhi yao kuliko wengine na pia kwa ambayo wanatoa katika mali zao. [An-Nisaa: 34]

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema: "Mwanamme ni mchunga (msimamizi) wa nyumbani kwake na ataulizwa kuhusu uchungaji (usimamizi) wake" [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

6-Ikiwa mume ana mke zaidi ya mmoja, inampasa afanye uadilifu baina ya hao wake. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anakataza kutokufanya uadillifu:

   

وَلَن تَسْتَطِيعُوا أَن تَعْدِلُوا بَيْنَ النِّسَاءِ وَلَوْ حَرَصْتُمْ ۖ فَلَا تَمِيلُوا كُلَّ الْمَيْلِ فَتَذَرُوهَا كَالْمُعَلَّقَةِ ۚ

Na wala hamtoweza kuadilisha baina ya wake japokuwa mkipania. Basi msimili muelemeo wote (kwa mke mmoja) mkamuacha (mwengine) kama kining’inio.  [An-Nisaa: 129]

 

Na Anasema:

 فَإِنْ خِف ْتُمْ أَلاَّ تَعْدِلُواْ فَوَاحِدَةً أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُمْ ذَلِكَ أَدْنَى أَلاَّ تَعُولُواْ

Lakini mkikhofu kuwa hamtoweza kufanya uadilifu, basi mmoja tu au ambao mikono yenu ya kulia imewamiliki. [An-Nisaa: 3]

 

Juu ya hivyo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) ameusia wanawake watendewe mema:

 

"Mbora wenu ni yule aliye mbora kwa familia yake na mimi ni mbora kabisa kwa familia yangu."   At-Twabaraaniy

 

Haki Za Mume Kutoka Kwa Mke:

 

1-Mke amtii mumewe na atambue kwamba ni amri ilotiliwa nguvu na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) kwa kuwa amesema:

لَوْ كُنْتُ آمِراً أَحَداً أَنْ يَسْجُدَ لأِحَدٍ لأَمَرْتُ الْمَرْأَةَ أَنْ تَسْجُدَ لِزَوْجِهَا مِنْ عِظَمِ حَقَّهِ عَلَيْهاَ

"Ningeliweza kumuamrisha mtu  amsujudie binaadamu mwenzake, ningeliamrisha mwanamke amsujudie mume wake kwa jinsi haki ya mume ilivyo tukufu kwa mke wake" Tuhfat Al-Ahwadhi 4.323  kutoka Tafsiyr ya Ibn Kathiyr

 

2-Mke inampasa kumuitikia mumewe anapomhitaji kujimai naye. Kutomtimizia haja yake bila ya sababu inayokubalika katika Shariy’ah ya Dini ni kulaaniwa na Malaika kwa dalili:

((إذا دَعَا الرَّجُلُ امْرَأتَهُ إِلىَ فِرَاشِهِ فَأَبَتْ عَلَيْه لَعَنَتْهَا الْمَلائِكَةُ حَتَّى تُصْبِحَ))

"Mume atakapomwita mkewe kitandani na mke akikataa, basi Malaika watakuwa wanamlaani huyo mke mpaka asubuhi". [Imepokelewa na Imaam Al-Bukhaariy]

 

3-Haimpasi mke kutoa swadaqah yoyote bila ya idhini ya mumewe; amekataza Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((لاَ تُنْفِقُ الْمَرْأَةُ شَيْئًا مِنْ بَيْتِهَا إِلا بِإِذْنِ زَوْجِهَا)) قالوا: "يا رسول الله! وَلا الطَّعَامَ؟ قال: ((ذَاكَ أَفْضَلُ أَمْوَالِنَا)) صحيح ابن ماجه - حديث حسن  الألباني

"Mwanamke asitoe kitu chochote kutoka nyumbani kwake ila kwa idhini ya mumewe". Wakasema: "Hata chakula ee Rasuli wa Allaah"? Akasema: "Hicho ni mali bora yetu".   Hadiyth Imepokelewa na Ibn Maajah na Shaykh Al-Albaaniy kasema ni ‘Hasan’.

 

Lakini mke anayo haki kutoa swadaqah katika kipato chake mwenyewe. Pia mke anaweza kutoa swadaqah ikiwa anatambua kuwa hatoghadhibikiwa na mumewe:

عن همام (رضي الله عنه)  قال: سمعت أبا هريرة (رضي الله عنه) عن النبي صلى الله عليه وسلم قال: ((إِذَا أَنْفَقَتِ الْمَرْأَةُ مِنْ كَسْبِ زَوْجِهَا عَنْ غَيْرِ أَمْرِهِ فَلَهُ نِصْفُ أَجْرِهِ))  - البخاري

Kutoka kwa Hamaam (Radhwiyya Allaahu ‘anhu) amesema: “Nimemsikia Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Mwanamke akitoa swadaqah kutoka katika kipato cha mumewe bila ya amri yake basi na yeye atapata thawabu nusu yake". [Al-Bukhaariy]

 

4-Haimpasi mke kutoka nyumbani kwake bila ya idhini ya mumewe (hata kwenda kwa wazazi wake ila kwa makubaliaono).

 

5-Haimpasi mwanamke kumfanyia ujeuri, ufedhuli au usafihi mumewe. Atakapokuwa ni kinyume cha hivyo akamtii mumewe basi amepewa fadhila kubwa ya kuingia Jannah (Peponi):

عن عبد الرحمن ابن عوف (رضي الله عنه) قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: ((إِذَا صَلَّتْ الْمَرْأَةُ خَمْسَهَا، وَصَامَتْ شَهْرَهَا، وَحَفِظَتْ فَرْجَهَا، وَأَطَاعَتْ زَوْجَهَا, قِيلَ لَهَا: ادْخُلِي مِنْ أَيِّ أَبْوَابِ الْجَنَّةِ شِئْتِ)) صحيح الترغيب

Kutoka kwa Abdur-Rahmaan bin 'Awf (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Mwanamke atakaposwali Swalaah zake tano, akafunga Swawm mwezi wake (wa Ramadhwaan), akahifadhi sehemu zake za siri (asifanye uzinifu), akamtii mume wake, ataambiwa ingia Jannah (Peponi) kupitia mlango wowote autakao."  Swahiyh at-Targhiyb

 

Hizo ni baadhi ya haki tulizojaaliwa kuzinukuu, tukitaraji kwamba pindi zikitimzwa, basi ndoa itaendelea kudumua katika usalama na amani.

 

Share