Zingatio: Ipi Katika Neema Za Mola Wetu Tuikanushayo?

 

Zingatio: Ipi Katika Neema Za Mola Wetu Tuikanushayo?

 

Naaswir Haamid

Na

 Dkt. H. R. Hikmany

 

Alhidaaya.com

  

 

 

Ar-Rahmaani Mwingi wa Rehema,

Ametufundisha Qurani na mengi mema,

Akamuumba Binaadamu na kumpa kunena,

Akatuwekea Jua na Mwezi nazo ni neema,

Akaturuzuku neema za usiku na mchana,

Ipi tuikanushayo katika hizi neema?

 

 

Mbingu Kaziinua juu hizo ni Zake neema,

Jua mwezi nyota pia ni Zake neema,

Nuru na kiza kwa duru hujaziona neema?

Mvua na mengi madimbwi maji humo kutuama,

Mimea na wengi wanyama pia kwao ni neema,

Ipi tuikanushayo katika hizi neema?

 

 

Ardhi Katandika chini hebu zingatia neema,

Mitende na mengi matunda ya rahisi kuyachuma,

Zimo nafaka na mboga tambua hizo neema,

Majini na mengi maua uturi zisizo koma,

Watambaao na wendao wote jumla ni neema,

Ipi tuikanushayo katika hizi neema?

 

 

Tazama nuru ya macho haijawa ni neema?

Nuru machoni fifia ni nani aweza randama?

Miguu kupiga hatua ni nani anaye tuama?

Ulimi usiomfupa utoao anuwai lafudhi na kalima,

Masikio mawili ya kichwa ikawa mfano antena ,

Ipi tuikanushayo katika hizi neema?

 

 

Bahari nazo si duni kwa wingi zake neema,

Tumbawe lulu marijani huoni na hizo neema?

Vihori mitumbwi mashua na watu kuvuna neema,

Bahari na vyake vituko mawimbi na yake milima,

Bahari dharuba na radi nani aweza simama?

Ipi tuikanushayo katika hizi neema?

 

 

Nyangumi nguru na pweza tambua hizo neema,

Bahari ilivyo vimeza ni vyote katika neema,

Bahari yaweza toweka ni nani alete lawama?

Ardhi ikijatoweka ni sote twajia Kiyama

Tabaki dhati Yake Rabb Mwenye Enzi za Daima,

Ipi tuikanushayo katika hizi neema?

 

 

Metughururi dunia kuvuna kila pembe ghanima,

Mughafala metukumba shaytwani na zake nakama,

Tunamwabudu asiye Muumba kasoro iliyo laana,

Karibuni-karibuni tutabambua kilio kisicho tuama,

Lau watu twakumbuka Tukufu na nyingi Karima

Ipi tuikanushayo katika hizi neema?

 

 

 

Share