Rajab: Kufunga (Swawm) Na Kusherehekea Siku Inayosemekana Ni Ya Israa na Mi'iraaj

 

Kufunga (Swawm) Na Kusherehekea Siku Inayosemekana Ni Ya Israa na Mi'iraaj

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Naomba mtujulishe kama kufunga tarehe 27 ya mwezi huu wa rajab na kusherehekea kama ni sahihi?

 

ahsanteni

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.  

 

 

Tukio la Israa na Mi’iraaj ni tukio adhimu na ni miongoni mwa miujiza aliyopangiwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  wetu karimu na Mola wake Mtukufu. Anasema Allaah kuhusiana na tukio hilo:

   بِسْمِ اللّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ  

 سُبْحَانَ الَّذِي أَسْرَىٰ بِعَبْدِهِ لَيْلًا مِّنَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ إِلَى الْمَسْجِدِ الْأَقْصَى الَّذِي بَارَكْنَا حَوْلَهُ لِنُرِيَهُ مِنْ آيَاتِنَا ۚ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ ﴿١﴾

1. Utakasifu ni wa Ambaye Amemsafirisha usiku mja Wake kutoka Al-Masjid Al-Haraam mpaka Al-Masjid Al-Aqswaa ambao Tumevibariki vilivyoko pembezoni mwake; ili Tumuonyeshe baadhi ya Aayaat (miujiza, ishara, dalili) Zetu. Hakika Yeye (Allaah) ni Mwenye kusikia yote, Mwenye kuona yote. [Al-Israa: 1]

 

 

Hapana shaka kwamba safari ya Israa na Mi'iraaj, (safari ya usiku mmoja kupanda Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika mbingu saba na kurudi siku hiyo hiyo kwamba ni jambo tukufu alilojaaliwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na limethibitika ukweli wake. Hali kadhalika ni jambo kuu la ajabu katika maajabu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kuonyesha uwezo na muujiza Wake kwa wana Aadam.

 

 

Usahihi wa tukio hili liko katika dalili kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alichukuliwa kupelekewa mbinguni na milango ilifunguliwa kwa ajili yake akapita kila mbingu na kuonana na Manabii walioko katika kila mbingu hadi kufika mbingu ya saba ambako Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alimuamrisha Swalaah tano. Idadi ya Swalaah hizo kwanza ilikuwa ni khamsini lakini Nabiy wetu (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alirudi kwa Mola Wake kwa kuomba hadi zikapunguzwa kuwa ni Swalaah tano ambazo Muislamu atakapozitimiza atapata thawabu za Swalaah khamsini kwa vile kila kitendo chema kinalipwa mara kumi. Na Ndipo  Swalaah ikawa na daraja ya juu, nzito na muhimu kuliko ‘ibaadah zote.  

 

Ama kuhusu usiku wenyewe wa tukio hili la Israa na Mi'iraaj hakuna Hadiyth Swahiyh inayoelezea kuwa ilikuwa katika mwezi wa Rajab au tarehe 27 ya mwezi huu wa Rajab kama wengi wanavyodhania. Usimulizi wowote unaotaja mwezi au tarehe ya tukio hili umekosa dalili Swahiyh kama wasemavyo ‘Ulamaa wa Hadiyth. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa hikma Yake Amewafanya watu wasahau siku hii. Hata kama ingelikuwa hiyo siku imetajwa katika dalili basi isingeliruhusiwa Muislamu kuipwekesha kwa kufanya ‘ibaadah fulani au kusherehekea. Hii kwa sababu Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wala Maswahaba zake hawakufanya hivyo. Na ingelikuwa kuipwekesha ni amri iliyo katika Dini yetu basi Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) angelitoa mafunzo kwa Ummah wake kwa kauli au vitendo. Na ingelikuwa imefanyika zama zake Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) basi bila shaka ingelijulikana na usimulizi ungelitufikia kwa isnaad Swahiyh kama tulivyopata mafunzo mengineyo ya uhakika.

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika khutbah yake mwisho kwenye Hijjatul-widaa' alisema: 

 

 ((يا أيها الناس،  ما من شيء يقربكم إلى الجنة ويباعدكم من النار إلا وقد أمرتكم به، وما من شيء يقربكم من النار ويباعدكم من الجنة إلا وقد نهيتكم عنه))

((Enyi watu, hakuna jambo lolote ambalo litakukurubisheni na Pepo na kukuepusheni na moto ila nimekuamrisheni nalo. Na hakuna jambo lolote litakalokukurubisheni na moto au kukuepusheni na Pepo ila nimekukatazeni nalo)).

 

Na ni amri kutoka kwa Mola wetu Mtukufu kufuata yote aliyotufunza Rasuli Wake:

 ((وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا))

((Na lolote (lile) analokupeni Rasuli (Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) basi lichukueni, na (lolote lile) analokukatazeni, basi acheni.)) [Al-Hashr: 7]

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa Mkweli Muaminifu aliyetimiza ujumbe aliopewa kwa ukamilifu na ndipo dini yetu ilipokamilika Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

  الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الإِسْلاَمَ دِينً

((Leo Nimekukamilishieni Dini (yenu), na Nimekutimizieni neema Yangu, na Nimekuridhieni kwenu Uislamu uwe (ndio) Dini yenu.)) [Al-Maaidah: 3]

 

Hivyo mwenye kufanya kitendo ambacho hakimo katika Dini yetu itakuwa ni kupoteza muda wake kwa ibada isiyo na thamani kama tulivyoonywa:

 

 (( من عمل عملاً ليس عليه أمرنا فهو رد)) البخاري

((Atakayetenda kitendo kisichokuwa chetu (katika dini yetu) basi kitarudishwa)) [Al-Bukhaariy]

 

Kwa hiyo Muislamu anapaswa kujiepusha na yote ambayo hayakuthibiti katika Shariy’ah.

 

Bonyeza viungo vifuatavyo upate faida na 'ilmu ziyada:

 

Rajab: Fadhila Za Mwezi Wa Rajab Na Yaliyozuliwa Ndani Yake

 

Rajab: Bid’ah Za Kujipeusha Nazo Katika Mwezi Wa Rajab Na Khaswa Tarehe 27

 

Imaam Ibn Al-Qayyim: Hakuna 'Ibaadah Maalumu Inayofungamana Na Mwezi Wa Rajab Wala Tukio La Israa Wal Mi'raaj

 

Imaam Ibn 'Uthaymiyn: Rajab: Haikuthibiti Kuwa Tarehe 27 Rajab Ni Siku Ya Israa Wal-Mi’raaj

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

Share