Kuamini Majini Na Nyota Kuwa Ndizo Zinazoendesha Maisha

 
SWALI:
 
 
 
JE INASWIHI KWA MTU ANAEAMINI KUWA KUTUMIA MAJINI NA KUAMINI KUWA NYOTA NDIZO ZINAZOENDESHA MAISHA NA KUWASHAURI WATU KUFANYA HIVYO KUPITIA VYOMBO VYA HABARI, ASHAURI MAMBO YA DINI TENA KUPITIA KTK VIPINDI VYAKE HIVYO AU AITWE SHEIKH AU MTUMISHI WA QURUANI?                                     
 
                                                                          
AMANI YA ALLAAH IWE JUU YENU.
 
 

 
 
JIBU:
 
 
 
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
 
 
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako hilo kuhusu masuala hayo uliyoyataja. Kama Waislamu tunatakiwa tuamini kuwa majini wapo nao ni viumbe kama binaadamu lakini haifai kuwaabudu wala kuwatumia kwa njia yoyote ile. Wapo watu wanaojidai kuwa wao ni mashekhe na kufanya shughuli hiyo inayokwenda kinyume na Dini ya Uislamu.
 
Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anaeleza mtihani uliowapata wana wa Israili na baadaye kumsingizia Nabii Sulaymaan (‘Alayhis Salaam) kuwa alifanya kazi ya uchawi. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema:
 
Na wakafuata yale waliyozua mashetani kuuzulia ufalme wa Sulaymaan. Na wala Sulaymaan hakukufuru, bali mashetani ndio waliokufuru, wakiwafundisha watu uchawi, na yaliyoteremshwa kwa Malaika wawili, Haarut na Maarut katika Baabil. Wala hao hawakumfundisha yeyote mpaka wamwambie: Hakika sisi ni mtihani; basi usikufuru. Wakajifunza kwa hao wawili yale ya kumfarikisha mtu na mkewe. Wala hawawezi kumdhuru mtu ila kwa kutaka Allaah. Na wanajifunza yatayowadhuru wala hayawanufaishi. Na hakika wanajua kwamba aliye hiari haya hatakuwa na fungu lolote katika Akhera. Na hakika ni kiovu mno walichojiuzia nafsi zao laiti wangelijua (2: 102). Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anauita utumiaji wa majini kuwa ni kufuru inayomtoa mtu katika Uislamu.
 
Ama kuhusu nyota, ni kiumbe kilichoumbwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) kuwa na manufaa aina fulani kwa watu. Wala nyota hazikuumbwa kwa ajili ya kuabudiwa wala kutumiwa kuangalilia.
 
Zayd bin Khaalid al-Juhaniy (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alituswalisha Swalah ya Alfajiri Hudaybiyah baada ya mvua ya usiku. Baada ya kumaliza Swalah, alitugeukia na kusema:
 
Je, mwajua Mola wenu Mlezi aliyoteremsha?” Watu wakajibu: “Allaah na Mtume Wake wanajua zaidi”. Akasema: “Allaah Amesema: ‘Asubuhi hii baadhi ya waja Wangu wamebaki Waumini wa kweli na baadhi wengine kuwa makafiri; Yeyote anayesema kuwa mvua imenyesha kwa ajili ya baraka kutoka kwa Rehema ya Allaah Ameniamini na amekanusha nyota, na yeyote aliyesema kuwa mvua imenyesha kwa sababu ya nyota fulani hana Imani na Mimi lakini ameiamini nyota hiyo” (al-Bukhaariy).
 
Hakika ni kuwa mtu yeyote anayefanya shughuli hiyo anafaa anasihiwe ili arudi katika njia ya haki na hafai kuitwa shekhe kabisa. Wala hatakiwi kupatiwa fursa ya kuweza kuwaidhi watu katika idhaa au runinga (televisheni). Na ikiwezekana mtu kama huyo asusiwe kabisa. Na hao wanaompa nafasi mtu kama huyo, Uislam wao una mashaka sana; ima maslahi ya kidunia wameyaweka mbele kwa kupata vitega uchumi fulani kama anavyofanya huyo anayejiita shekhe kwa kutapeli watu na kula mali zao kwa mwavuli wa Dini, au kuna ile hali ya kuoneleana muhali kwa kuwa kuna maslaha fulani ya kidunia yasiharibike. Kwa kifupi, mtu huyo anayepiga ramli na kutabiria watu mambo yao, ni mtu muovu sana na anamshirikisha Allaah, na hao wanaomwendea pia hawakubaliwi Swalah zao siku arubaini kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu ’alayhi wa aalihi wa sallam): ”Atakayekwenda kwa mtabiri akamuuliza kitu haitokubaliwa Swalah yake siku arubaini[Muslim]
Na ikiwa watamwamini kwa yale anayowatabiria, basi watakuwa wamekufuru kabisa yale aliyokuja nayo Muhammad (Swalla Allaahu ’alayhi wa aalihi wa sallam) kama inavyonyesha Hadiyth hii ”Yeyote atakayejimai (kufanya kitendo cha ndoa) na mwanamke mwenye hedhi, au kwa kutumia njia ya nyuma, au kumkaribia mtabiri na kuamini aliyoambiwa, basi amekufuru yale aliyoteremshiwa Muhammad” [Hadiyth Sahiyh imesimuliwa na Abu Daawuud, Ibn Maajah, At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy na wengineo]
Soma katika viungo vifuatavyo upate faida zaidi:
 
Allaah Atulinde na hayo na Awaongoze wote.
 
Na Allaah Anajua zaidi
Share