Afanye Nini Kwa Aliyemdhulumu? Ni Bora Kumlipa Kisasi Au Kumwachia Allaah?

SWALI:
 
Swali langu ni hili, ikiwa mtu amekudhulumu kwa aina yoyote wewe haki yako nikumfanya nini au muachiye mungu.
 

 
JIBU:
 
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
 
Shukrani zetu za dhati kwa ndugu yetu aliyeuliza swali hili kuhusu dhuluma. Mwanzo inahitajika ieleweke kuwa Muislamu hafai kukubali kudhulumiwa kwa njia yoyote ile na pia haifai kwake kudhulumu.
 
Hivyo, ikiwa mtu amekudhulumu inafaa uitafute haki yako kwa njia zote zile za kishariy'ah ili urudishiwe haki yako. Wala usichoke kufanya hivyo kwani kuachilia haki yako itamfanya mtu huyo awe na ujasiri wa kukudhulumu kwa mara nyingine tena.
 
Katika Hadiyth al-Qudsiy Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema: Allaah Aliyetukuka Amesema: “Enyi waja Wangu! Mimi Nimejiharamishia dhuluma juu ya Nafsi Yangu na Nikaifanya ni haramu baina yenu basi msidhulumiane” (Muslim).
 
Unapodhuliwa kwa namna yoyote ile Uislamu umekupatia njia tatu ya kuliendea suala hilo: Kulipiza kisasi au kumsamehe na kufanya subra au kumuachia Allaah. Hakika ni kuwa kusamehe ni bora, kwani kufanya hivyo kuna faida nyingi tunazitaja chache zifuatazo:
 
 
1- Kuwa pamoja na Allaah, na kulipwa ujira wa kusubiri.
 
 
Na mkilipiza basi lipizeni sawa na vile mlivyoadhibiwa. Na ikiwa mtasubiri, basi hakika hivyo ni bora zaidi kwa wanaosubiri. Na subiri. Na kusubiri kwako kusiwe ila kwa sababu ya Allaah tu. Wala usiwahuzunikie; wala usiwe katika dhiki kwa hila wanazozifanya. Hakika Allaah yu pamoja na wenye kumcha, na watendao mema” (16: 126 – 128).
 
 
2- Kusamehewa madhambi ya mja
 
Vile vile kumsamehe aliyekudhulumu au aliyekukosea ni kupata maghfirah kutoka kwa Mola wako ambayo hakuna mmoja wetu asiyetaka kusamehewa madhambi yake. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
 
 
 
((وَلْيَعْفُوا وَلْيَصْفَحُوا أَلَا تُحِبُّونَ أَن يَغْفِرَ اللَّهُ لَكُمْ وَاللَّهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ))
 
((Na wasamehe, na waachilie mbali. Je! Nyinyi hampendi Allaah Akusameheni? Na Allaah ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu)) [An-Nuur: 22]
 
 
3- Kupandishwa daraja na kuwa miongoni mwa Muhsiniyn
 
Pia ni kupandishwa daraja ya kuwa Muhsiniyn kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
 
 ((الَّذِينَ يُنفِقُونَ فِي السَّرَّاء وَالضَّرَّاء وَالْكَاظِمِينَالْغَيْظَ وَالْعَافِينَ عَنِ النَّاسِ وَاللّهُ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ))
  
((Ambao hutoa wanapokuwa na wasaa na wanapokuwa na dhiki, na wanajizuia ghadhabu, na wasamehevu kwa watu; na Allaah Huwapenda wafanyao wema)) [Al-'Imraan: 133]
 
 
4- Kulipwa ujira kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
 
 ((وَجَزَاء سَيِّئَةٍ سَيِّئَةٌ مِّثْلُهَا فَمَنْ عَفَا وَأَصْلَحَ فَأَجْرُهُ عَلَى اللَّهِ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الظَّالِمِينَ))
 
Na malipo ya uovu ni uovu mfano wa huo. Lakini mwenye kusamehe, na akasuluhisha, basi huyo malipo yake yapo kwa Allaah. Hakika Yeye hawapendi wenye kudhulumu)) [Ash-Shuwraa: 40]
 
 
Na Allaah Anajua zaidi
 
Share