Wanaume Kula Zaafarani Inaruhusiwa?

 

SWALI:

ningependa kuuliza wanaume hawafai kula zaafarani?siku zote nijuavyo haina neno hutia kwa chakula,nimeskia hivi juzi ya kuwa kiislaam hairuhusiwi. Tafadhali nijulisheni ikiwa ni ukweli na kwa sababu gani.

Shukran kwa jitihada zenu kutuongoza. Mungu awajaze kheyr. Ameen

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa ndugu yetu muulizaji swali. Kuhusu suala hilo wakati mmoja Yahya alimuuliza Imaam Maalik, je inafaa kwa mtu aliye katika ihraam kula chakula kulichotiwa zaafarani, naye akajibu: “Hakuna tatizo lolote kwa mtu aliye katika ihraam kula ikiwa chakula hicho kimepikwa. Lakini ikiwa hakijapikwa basi asile”. Ama Ibn Qudaamah anasema: “Niswaab ya zaafarani, pamba na vitu mfano wa hivyo ni ratili 1,600 ya Iraq. Hivyo, wizani wake ukisiwe”.

Bila shaka ikiwa inatolewa Zakaah itakuwa kuliwa pia hakuna tatizo kwa wanawake na wanaume.

Ama ikiwa unataka kujua kama inafaa kunywewa kama wanavyofanya wale wanaotengenezewa na waganga au mashekhe wa uongo kuwa ni kama dawa au kinga na kuandikiwa maandishi ya Qur-aan kwenye sahani kasha ikachanganywa na maji kisha akapewa mtu anywe, basi hiyo haifai na si sawa mtu kutumia. Haifai kutumia si kwa sababu ya zaafarani, bali ni kwa sababu njia hiyo iliyotumika si ya kisheria ambayo ni njia ya udanganyifu unaotumiwa na watu kwa kutumia maneno ya Allaah na kuvumbua mbinu mbalimbali za kutafutia chumo ndani yake kwa njia za udanganyifu kama hizo za kutengeneza kombe kwa Qur-aan, maji na zaafarani. Jambo hilo na mashekhe au waalimu wenye mchezo huo wanatakiwa wapigwe vita haswa wasile pesa za watu kwa dhulma na udanganyifu ambao haupo katika sheria.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share