Wanyama Wanaochinjwa Na Mayahudi Ni Halaal Kula?

 

SWALI:

assalamualeikum warahmatullahi ta'ala wabarakatu

ama ba'ad mimi ni mama naishi uk ninae rafiki yangu ambae mume wake ana fanya kazi kwenye kiwanda cha kuchinja kuku. sasa hao kuku wanachinjwa na mayahudi mimi swali langu ni je hao kuku ni halali kuliwa na muislamu? naomba majibu.

jazzakallah,

dada wa kiislam

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Maulamaa wengi wamekubaliana kwamba wanyama wanaochinjwa na Ahlul-Kitaab tunaruhusiwa kula nyama yao kutokana na dalili ya Qur-aan:  

 

((الْيَوْمَ أُحِلَّ لَكُمُ الطَّيِّبَاتُ وَطَعَامُ الَّذِينَ أُوتُواْ الْكِتَابَ حِلٌّ لَّكُمْ وَطَعَامُكُمْ حِلُّ لَّهُمْ))  

((Leo mmehalalishiwa kila vilivyo vizuri. Na chakula cha walio pewa Kitabu ni halali kwenu, na chakula chenu ni halali kwao)) [Al-Maaidah:5]

Ibn 'Abbaas رضي الله عنه na wengineo wamesema kwamba chakula cha Ahlul-Kitaab katika Aayah hii imekusudiwa ni wanyama wanaochinjwa.

 

Lakini Muislamu anayeishi nchi zisizo za Kiislamu ambako wengi wao ni Ahlul-Kitaab (Watu wa vitabu) wanahitaji kujua njia zinazotumika katika uchinjaji wa wanyama wa nchi hizo. Akitambua kwamba wanyama wanachinjwa kabla ya kufa anaweza kula baada ya kusema Bismillah. Na akitambua kwamba njia inayotumika sio ya sheria ya Kiislamu kama mfano  kuzubaishwa (stunning operation) nayo ni kumuua kwanza mnyama ambayo inatumika sana nchi za Kimagharibi basi haifai Muislamu kula nyama hiyo.

 

Katika hali nyingi inavyojulikana kuwa kwa wanyama wakubwa kama ng'ombe, kondoo n.k wanadungwa na mshtuko wa umeme ambao unawaathiri kwa muda mfupi kisha huchinjwa. Hufanywa hivyo ili kazi ya kuchinja iwe sio ya maumivu.  Hii inakubaliwa katika rai ya Kiislamu nayo ni kutokana na Hadiyth:

 

 ((إن الله كتب الإحسان على كل شيء . فإذا قتلتم فأحسنوا القتلة وإذا ذبحتم فأحسنوا الذبحة ، وليحد أحدكم شفرته وليرح ذبيحته)) صحيح الترمذي و قال الشيخ الإلباني صحيح  

 

 

 

((Allah Amefaradhisha ihsaan kwa kila kitu, kwa hiyo mnapoua (wanyama) fanyeni ihsaan katika uuaji na mnapochinja fanyeni ihsaan katika uchinjaji, basi atie makali mtu kisu chake na ampunguzie (amuondoshee makali) kichinjo chake)) [Swahiyh At-Tirmidhiy na Shaykh Al-Albaaniy pia kasema ni Swahiyh]

 

 

 

Lakini baadhi ya Maulamaa wanaona kwamba ikiwa Muislamu anaishi nchi za kikafiri na yako maduka ya Kiislamu ya Halaal basi ni bora zaidi kujitoa katika shaka na kununua nyama katika maduka hayo. Ila tu kama hakuna nyama inayochinjwa na Waislamu basi ndio anaweza kula hiyo ya Ahlul-Kitaab.

Kuhusu khaswa nyama inayochinjwa na Mayahudi inaitwa Kosher. Na inasemekana kwamba Mayahudi wanachinja kwa kutaja jina la Allaah سبحانه وتعالى, lakini hatujui wanasema nini katika lugha yao ya ki Hebrew wanapochinja, hivyo ni bora kuepukana nayo ikiwa inapatikana nyama inayochinjwa na Waislamu.  

Na Allaah Anajua zaidi.

 

Share