Utaratibu Wa Kuunga Swalah Ya Jama‘ah

Utaratibu Wa Kuunga Swalah Ya Jamaa‘ah

 

 

SWALI:

 

Namshuru Allah, mwingi wa rehema na mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na ndogo ndogo na natakia reheme Mtume wetu mtukufu, Muhamaad (Salla Allaahu alayhi wa sallam). Baada ya haya, swali langu ni: “Watu wawili wa jinsia moja wanaposwali pamoja, anayeswalishwa anatakiwa asimame nyuma kidogo ya imam upande wa kulia, anapokuja mtu wa tatu kuunga swala, atasimama nyuma ya Imam na yule alie upande wa kulia wa imam atarudi nyuma kuungana na yule aliyekuja, je akija mtu kuunga swala na akasimama upande wa kulia wa yule anayeswalishwa, huyu anayeswalishwa atafanya nini? Asalaam Aleikum

 

 

 

 

JIBU:

 

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Hakika ya hilo ni kuwa hali inapokuwa kama ulivyoeleza basi yule anayeswalisha (Imaam) atasongea mbele kidogo kiasi cha maamuma kuweza kuswali bila ya kukanyagwa vichwa na Imaam. Na ikiwa hakuna nafasi ya kusongea mbele kwa Imaam kutokana na kuzuiwa na sutrah au nguzo au ukuta, basi hao Maamuma watarudi nyuma kidogo ikiwa wanataraji kutaongezeka wengine kujiunga na swafu yao, la kama ni hao wawili tu wanaweza kubaki hapo walipo maadam Imaam yupo mbele yao na hakuna shaka yoyote katika hilo kwani Swafu huanzwa kujazwa kulia.

 

Na umesema kuwa “Watu wawili wa jinsia moja wanaposwali pamoja, anayeswalishwa anatakiwa asimame nyuma kidogo ya imam”. Hili halina dalili, ilivyo ni kuwa wakiswali wawili basi wanakaa usawa mmoja wote Imaam na Maamuma, kwani Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa akiswali peke yake siku moja, kijana ‘Abdullaah bin ‘Abbaas alikuja akasimama upande wake wa kushoto, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimshika na kumzungusha asimame ubavuni mwake mwa kulia. Katika tukio hilo kunaonekana kuwa walisimama wote sambamba.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share