Kisa Cha Julaybiyb Na Swahaabiyyah Aliyemtii Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)

 

Kisa Cha Julaybiyb Na Swahaabiyyah Aliyemtii Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)  

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

Swahaba aliyeitwa Julaybiyb alijulikana sana kuwa alikuwa ni mtu duni asiyemiliki mali na hakuwa ni mzuri kwa sura na umbo, na alikuwa ni mtu wa kuchekesha watu. Kwa hivyo hakuna aliyetaka kumuozesha binti yake. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuuliza Julaybib kama anataka kuoa, naye akamjibu: "Ee Rasuli wa Allaah, nani atakayekubali nimuoe mimi? Sina nyumba wala wala mali wala chochote katika mapambo ya dunia".

 

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamtuma mtu mmoja aende nyumba ya Answaariy fulani ambao walikuwa ni familia mashuhuri kwa kabila lao kubwa lenye kujulikana kwa heshima na wenye hali nzuri ya mali.

 

 

Alipopiga hodi, alifungua mlango mama wa binti huyo. Swahaba akamjulisha kuwa ametumwa na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuleta posa kwa binti yake. Mama huyo alifurahi sana kudhania kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) ndiye anayetaka kumposa binti yake.

 

 

Swahaba Alipomjulisha kuwa sio kwa ajili ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), bali ni kwa ajili ya Julaybiyb, mama huyo alisema: "Nani? Julaybib? Hapana! Hatumuozeshi yeye binti yetu!". Mara yule binti alisikia mazungumzo hayo akaja kuuliza vizuri: "Nani anayetaka kuniposa?" Mama mtu akamuelezea kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amemtuma mtu aje kumposa yeye kwa ajili ya Julaybiyb. Binti huyo alimwambia mama yake: "Vipi mama unakataa amri ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)? Fuata amri yake kwani hakuna kitakachonidhuru". (Katika usemi mmoja ni kwamba hapo hapo Aayah ifuatayo iliteremshwa [Ibnu Kathiyr 7: 692-694]) na katika usemi mwingine aliwaambia wazazi wake: "Hamkusikia kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّـهُ وَرَسُولُهُ أَمْرًا أَن يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ ۗ وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُّبِينًا ﴿٣٦﴾

Na haiwi kwa Muumini mwanamume na wala kwa Muumini mwanamke, Anapohukumu Allaah na Rasuli Wake jambo lolote, iwe wana hiari katika jambo lao.  Na anayemuasi Allaah na Rasuli Wake, basi kwa yakini amepotoka upotofu bayana. [Al-Ahzaab:36]

 

Ikabidi wamuozeshe binti yao kwa Julaybiyb.

 

 

Kisha katika vita fulani alitoka Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba miongoni mwao ni Julaybiyb na baada ya ushindi wa vita hivyo, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwauliza Swahaba kabla ya kurudi: “Je, kuna mtu aliyekosekana?”

 

 

Wakataja baadhi ya Swahaba waliokosekana kisha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawauliza tena wakasema: "Hakuna mtu mwingine aliyekosekana.” Lakini Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Lakini mimi naona kwamba Julaybiyb amekosekana.” yaani hayupo na sisi. “Nendeni mkamtafute miongoni mwa waliouliwa.”

 

 

Swahaba wakaenda kumtafuta wakamkuta ameuawa akiwa karibu yake makafiri saba ambao aliwahi kuwaua yeye Julaybiyb. Swahaba wakamjulisha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye alikwenda na kusimama karibu naye kisha akasema: “Ameua saba kisha wakamuua. Yeye ni wangu na mimi ni wake”.

 

 

Alisema hivyo mara mbili au tatu, kisha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akambeba kwa mikono yake na kwenda kumzika. Na akamuombea Du'aa mke wake:

 

((الَّلهُمَّ، صَبَّ عَلَيْهَا [الخير] صَبَّا، وَلاَ تَجْعَل عَيْشَها كَدَّا))

“Ee Allah, Mjaze kheri (nyingi) zilizojaa na Usimjaaliye maisha yake kuwa ni ya shida [tabu na mashaka]”.

 

 

Imesemekana kwamba hakuweko mjane aliyekuwa ana maisha mema kama maisha ya mke wa Julaybiy (Radhwiya Allaahu ‘anhaa).

 

 

[Kisa kimesimuliwa na Imaam Ahmad Muslim na An-Nasaaiy]

 

 

 

 

Share