Nguo Za Rangi Ya Kijani Zina Maana Gani?

SWALI LA KWANZA:

 Rangi ya kijani in Islam ina maana gani?

SWALI LA PILI:

 Imekuwa ni kawaida yetu biharusi kuvaa kanzu ya kijani katika akdi. je, hii ni katika mafunzo yetu?  Je, walivaa hivo wanawake wa zama mtume?

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Rangi ya kijani imetajwa katika Qur-aan kuwa ni nguo ambazo watakazozivaa watu wa peponi:

((عَالِيَهُمْ ثِيَابُ سُندُسٍ خُضْرٌ وَإِسْتَبْرَقٌ وَحُلُّوا أَسَاوِرَ مِن فِضَّةٍ وَسَقَاهُمْ رَبُّهُمْ شَرَابًا طَهُورًا))

((Juu yao zipo nguo za hariri laini za kijani kibichi, na hariri nzito ya atilasi. Na watavikwa vikuku vya fedha, na Mola wao Mlezi Atawanywesha kinywaji safi kabisa)) Al-Insaan: 21]

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ إِنَّا لَا نُضِيعُ أَجْرَ مَنْ أَحْسَنَ عَمَلًا ﴿30 أُوْلَئِكَ لَهُمْ جَنَّاتُ عَدْنٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهِمُ الْأَنْهَارُ يُحَلَّوْنَ فِيهَا مِنْ أَسَاوِرَ مِن ذَهَبٍ وَيَلْبَسُونَ ثِيَابًا خُضْرًا مِّن سُندُسٍ وَإِسْتَبْرَقٍ مُّتَّكِئِينَ فِيهَا عَلَى الْأَرَائِكِ نِعْمَ الثَّوَابُ وَحَسُنَتْ مُرْتَفَقًا ﴿31

30.  Hakika wale walioamini na wakatenda mema - hakika Sisi hatupotezi ujira wa anayetenda mema

31. Hao watapata Bustani za milele, zinazo pita mito kati yake. Humo watapambwa kwa mavazi ya mikononi ya dhahabu, na watavaa nguo za kijani za hariri na atilasi, huku wakiegemea humo juu ya makochi. Ni malipo bora hayo! Na matandiko mazuri mno ya kupumzikia! [Al-Kahf:30-31]

Bila ya shaka kuna uzuri wake hiyo rangi hata ipewe sifa ya nguo za watu wa Peponi. Lakini isiwe ndio itikadi ya watu kuvaa nguo hizo kama ni hasa kwa ajili ya Hajj au 'Umrah, kama wanavyofanya baadhi ya watu.

Ama kumvalisha biharusi kanzu ya kijani pia hakuna dalili katika mafunzo ya dini yetu. Biharusi anaweza kuvaa nguo ya rangi yoyote. 

Hiyo ni itikadi tu ya watu wa zamani na jambo lililoanzishwa bila ya dalili na linaendelea kutendeka. Inatupasa sote tuache kushikilia mila na itikadi zisizokuwa katika sheria ya Dini yetu.

Kuweka itikadi hizo ni kama kuwafuata wengine wanaovaa nguo hasa kwa sherehe fulani, mfano; Mabaniani wanavaa nguo nyekundu, na hata baadhi ya ndugu zetu wengine wa Kiislamu kama Wahindi wameiga nao mila hiyo.  Au Wakristo wanawavalisha mabiharusi nguo nyeupe. Jambo hili pia tunaliona katika sherehe zetu za ndoa.

Waislamu tunapaswa tukate kabisa mizizi hiyo yenye itikadi na kufanya hivyo tutakuwa tumetekeleza mambo yafuatayo muhimu:

1.      Tutazuia itikadi, uzushi na mila zisizokuwa na dalili kuendelea kwa vizazi vyetu vinavyokuja, na hii itakuwa ni moja wa njia ya kuinusuru dini yetu na kuibakiza iwe safi bila ya mambo ya itikadi na uzushi.

2.      Tutapata thawabu kufanya hivyo.

3.      Tutajiondoshea taklifu kulazimika kutafuta nguo za rangi hizo kwa kuvaa nguo ya rangi yeyote.

4.       Tutajiokoa na kufuata mila za makafiri na dini nyingine, jambo linalomchukiza Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala  na sisi wenyewe tutakuwa na hisia ya fakhari katika nyoyo zetu kuwa hatufati mila za dini nyingine na pia tutaridhisha nafsi zetu kwa kufuata amri za Mola wetu na kuacha makatazo Yake.

Na Allaah Anajua zaidi   

 

Share