Kuchelewesha Kusherehekea Sikukuu Ya ‘Iyd Kwa Ajili Ya Wasaa Inafaa?

 

Kuchelewesha Kusherehekea Sikukuu Ya ‘Iyd Kwa Ajili Ya Wasaa Inafaa?

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali:

 

Assalam alaykum,

 

Kuna kawaida ya kuisherehekea sikukuu siku ambayo ni ya nafasi kwa wootee kwa mfano sikukuu ikitokezea Jumatano sherehe ya kwa jumla ya watu woote hapa uingereza huweza kupangwa ikawa Jumamosi au Jumapili.......... SUALI Jee inafaa kushereheka kwa jina la skukuu na siku yenyewe ya sikukuu imepita? Na hii sikukuu inafaa kusherehewa siku ngapi?

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Hakika Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipohamia Madiynah aliwakuta, Answaar wakisherehekea siku mbili. Hapo akawaambia kuwa Allaah Aliyetukuka Amewabadilishia siku mbili zilizo bora kuliko hizo mbili zao, nazo ni ‘Iyd al-Fitwr na ‘Iyd al-Adhw-haa.

 

 

Kwa ajili hiyo siku za kusherehekea zimewekwa na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa muongozo kutoka kwa Allaah Aliyetukuka. Kwa hiyo, sherehe yenyewe ni siku ambayo Waislamu watajumuika kuswali pamoja, haitofaa kufanya siku nyingine kwa sababu moja au nyingine. Kusherehekea siku nyingine haitoleta tena ile mafhumu ya sherehe ya ‘Iyd labda ipatiwe jina jingine na si sikukuu ya ‘Iyd, kwani sikukuu hizo zimefungamanishwa na tarehe na mnasaba wake wa kutukia tukio hilo.

 

 

Ama katika siku ya ‘Iyd al-Fitwr sherehe ni baada tu ya kuonekana mwezi au kupatikana taarifa za kuonekanwa kwake.

 

 

Na katika ‘Iyd al-Adhw-haa ni wakati wa mahujaji kuondoka ‘Arafah, tarehe 10 ya mwezi wa Al-Muharram, na sherehe zinaendelea kwa kuchinja kwani Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliagiza hilo kwa siku tatu kufanya hivyo baada ya ‘Iyd hiyo lakini sherehe kwa ufupi ni siku mbili tu kwa mwaka na hazibadiliki.

 

 

Mara nyingi hushindwa kufanya sherehe inayotakiwa kisheria kwani huwa tunataka kuongeza sherehe hizo kwa njia ambazo hazikuidhinishwa na sheria. Lau tutafuata sheria nayo katika ‘Iyd ni Swalah, kufurahi, kuvaa vizuri, kula vizuri na kutembelea jamaa na marafiki siku hiyo ni jambo sahali sana kwa kila mmoja.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share