Historia Ya Luqmaan Mwenye Hekima

 

SWALI:

 

 

bismillahi rrahmani rrahim nilikua na swali ambalo labda naweza kupata ufafanuzi wake hapa na swali lenyewe si kubwa wala zito lakini ni kuzidiana ilmu na swali ni hivi kwamba ningependa kujua kisa cha luqman kuanzia maisha yake n hikma zake na kufa kwake maana huyu mtu ametajwa katika quraan naitakua si mtu wa kawaida ni hilo tuu ahsantum assalam alykum kila la kheri na mafanikio mema.

 


JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako.

 

 

Luqmaan alizaliwa katika Bara la Afrika. Jina lake ni Luqmaan bin 'Anqa' bin Saadun au kama anavyosema Ibn Jariyr, jina lake lilikuwa Luqmaan bin Tharan kutoka watu wa Aylah (Quds).

 

 

Alikuwa ni mtu mwema aliyefanya juhudi katika Ibaadah na kutunukiwa busara. 

 

 

Alikulia katika msitu na kutembea bila viatu. Kule kukutana kwake na wanyama kulifanya awe mwenye nguvu, ujasiri, madhubuti na kutoogopa chochote. Alikuwa na ada ya kutafakari sana kuhusu maumbile yaliyomzunguka. Huko kulimfanya awe ni mwenye kujifunza vitu vizuri vizuri kila uchao.

 

Luqmaan alishikwa na wafanyabiashara wa utumwa waliovamia Afrika na kuuzwa kama mtumwa. Alijikuta amevuliwa uhuru wake, hivyo kumfanya asiweze kutembea wala kuzungumza anavyotaka. Huu ulikuwa ni mtihani wa kwanza aliolazimika kuuvumilia. Aliumia katika utumwa lakini alivumilia kwa kusubiri huku akiwa na matumaini kuwa Allaah Aliyetukuka Atamtoa katika janga hilo.

 

 

Aliyemnunua alikuwa ni mtu mzuri, mwema na mwenye busara. Hivyo, alimtendea wema Luqmaan. Aliweza kutambua kuwa Luqmaan alikuwa si mtu wa kawaida kwa werevu aliokuwa nao.

 

Mtu huyu mwenye huruma aliacha wasiya kuwa anapoaga dunia tu Luqmaan aachwe huru. Na alipokufa, ombi hilo lilitekelezwa na hivyo kumfanya Luqmaan kwa mara nyingine tena kuwa huru. Luqmaan alisafiri kwa muda na kuweka makazi yake pamoja na wana wa Israili. Alichaguliwa kwa hakimu katika utawala wa Nabii Daawuud ('Alayhis Salaam), naye aliheshimiwa na watu wote kwa busara yake na hukumu zake za uadilifu. Alioa na kulea familia.

 

Amesema Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhuma): Luqmaan alikuwa mtumwa wa kutoka Ethiopia akifanya kazi ya useremala.

 

'Abdullaah bin Az-Zubayr (Radhiya Allaahu 'anhuma) amesema, nilimuuliza Jaabir bin 'Abdillaah kuhusu Luqmaan. Akasema: 'Alikuwa mfupi na pua mseto na alikuwa Mnubi'.

 

Imesimuliwa na Yahya bin Sa'iyd al-Answaariy kutoka kwa Sa'iyd bin al-Musayyib akisema: 'Luqmaan ni mtu mweusi kutoka Misri'.

 

Al-Awza'iy amesema: Niliambiwa na 'Abdur-Rahman bin Harmalah kuwa mtu mmoja mweusi alikuja kwa Sa'iyd bin AI-­Musayyib akimuomba sadaka. Sa'iyd alimwambia: Usihuzunike kwa sababu ya rangi yako nyeusi kwani kulikuwa miongoni mwa walio bora kati ya watu ni watu weusi watatu: Bilaal bin Rabaah, Mahja' (mwachwa huru 'Umar bin Al-Khatwtwaab) na Luqmaan, mtu mweusi mwenye busara, kutoka Nubia, ambaye midomo yake ilikuwa mipana.

 

Imepokewa kwa Ibn Wahb: 'Mtu mmoja alikuja kwa Luqmaan, mwenye hekima na kumuuliza: Je, wewe ni Luqmaan? Je, wewe ni mtumwa wa fulani? Akajibu: Ndio. Yule mtu akasema: Wewe ndiye yule mchungaji mweusi. Luqmaan akasema: Ama kuhusu rangi yangu nyeusi, inaonekana dhahiri, kwani ni lipi linalokustaajabisha? Akasema yule mtu: Umekuwa ukizuriwa na watu kila mara ambao wanakubali hukumu yako. Luqmaan akasema:  Ewe ndugu yangu! Ukifanya ninayokuambia utakuwa kama hivi. Yule mtu akasema: Ni nini hayo? Luqmaan akasema: Inamisha macho yako, chunga ulimi wako, kula kilicho halali, kuwa mtwaharifu, timiza ahadi, kuwa mkarimu kwa wageni, waheshimu majirani, acha lisilokuhusu. Zote hizi zilinifanya mimi nikawa hivi.

 

 

Hata hivyo, wanazuoni wengi wana rai na muono kuwa Luqmaan alikuwa si Nabii bali mtu mwenye busara. Zaidi ya hayo, ametajwa katika Qur-aan na amesifiwa na Allaah Aliyetukuka, Ambaye Ametusimulia wasiya wake kwa mwanawe pale aliposema:

 

'Ee mwanangu! Usimshirikishe Allaah kwani kufanya hivyo ni dhuluma kubwa' (31: 13).

 

Kwa hiyo, alimuonya mwanawe na kumkataza kuingia katika shirki.

 

Imaam Al-Bukhaariy amesema: Niliambiwa na Qutaybah kutoka kwa Jariyr kutoka kwa Al-A'mash kutoka kwa Ibraahiym kutoka kwa 'Alqamah kutoka kwa 'Abdullah kwamba alisema:  'Aayah ifuatayo ilipoteremka: 'Ni wale wenye kuamini na hawachanganyi Imani na dhuluma' (6: 82) tulisema: 'Ee Mtume wa Allaah! Ni nani katika sisi asiyefanya dhuluma kwake yeye mwenyewe'. Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa sallam) akawajibu: ((Si kama msemavyo, kwani dhuluma katika Aayah na kutochanganya imani na dhuluma inamaanisha SHIRKI. Je hamjasikia kauli ya Luqmaan kwa mwanawe: 'Ee mwanangu! Usimshirikishe Allaah kwani kufanya hivyo ni dhuluma kubwa' (31: 13).

 

 

Katika nasaha alizompatia mwanawe ni kuwatendea wema wazazi, kutokua na kibri, kusimamisha Swalah, kuamrisha mema na kukataza maovu, kusubiri, kutonyanyua sauti na kadhalika kama Alivyotupa maelezo hayo Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

 

'Ee mwanangu! Kikiwapo kitu cha uzito wa chembe ya khardali kikawa ndani ya jabali au ndani ya mbingu au ndani ya ardhi, basi Allaah Atakileta. Hakika Allaah ni Mjuzi wa yaliyofichika, Mwenye khabari za yote'.  

 

'Ee mwanangu! Shika Swalah, na amrisha mema, na kataza maovu, na subiri kwa yanayo kupata. Hayo ni katika mambo ya kuazimiwa'

'Wala usiwabeuwe watu, wala usitembee katika nchi kwa maringo. Hakika Allaah Hampendi kila anayejivuna na kujifakhirisha' [Luqmaan:16-18].

 

 

Vipo visa kadhaa vinavyoonyesha hekima na busara yake lakini nasaha kwa mwanawe zilizotajwa katika Qur-aan ni tosha kwetu kupata mafunzo mazuri kabisa. Hivyo, haitakuwa na haja kutoa visa vingine ambavyo vingine huenda vikawa si sahihi.

 

Ibn Abi Haatim amesema: Niliambiwa na babangu kutoka kwa Qatadah aliyesema: Allaah Aliyetukuka Alimpatia fursa Luqmaan kuchagua baina ya utume na kuwa na hekima, naye akachagua hekima. baadaye, Jibriyl alikuja kwake akiwa amelala na kummiminia hekima. Luqmaan alianza kuitamka siku ya pili yake. Inasemekana kuwa Luqmaan aliulizwa kwa nini alichagua hekima juu ya utume. Alisema: Lau kama Allaah Alinipatia utume ningeukubali na ningejaribu sana kupata radhi Yake, lakini Alinichaguza. Niliogopa kuwa dhaifu sana kwa utume, hivyo nikachagua busara. 

 

 

Masimulizi haya si sahihi kwani mpokeaji mmoja Sa'iyd bin Bashiyr, si mwaminifu. Hata hivyo, watangu wema wengi wa mwanzo na wanazuoni, kama Mujaahid, Sa'iyd bin Al-Musayyib and Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhum) walikuwa na muono kuwa ile kauli ya Allaah inayosema:

'Na hakika Tulimpatia Luqmaan Hikmah' (31: 12).

 

Hii ina maana uchambuzi na ufahamu wa kidini. Kwa hiyo, hakuwa Mtume na hakuna chochote kilichoteremshwa kuonyesha kuwa aliteremshiwa wahyi.

Hikma zake nyingine kama zilivyosimuliwa ni hizi:

 

 

Kutoka kwa Damurah As-Sariy Ibn Yahia: Nimeambiwa na baba yangu kutoka kwa  'Abdah Ibn Sulaymaan kutoka  kwa Ibn Mubaraak kutoka kwa 'Abdur-Rahmaan al Mas'uud  kutoka kwa 'Awn Ibn 'Abdillaah akisema:' ' Luqmaan alimwambia mwanawe: Ewe mwanangu ukikutana na watu anza kwa salaam [Assalaamu 'alaykum]. Kisha kaa upande na usiseme kitu hadi waseme wao. Ukiwaona wanamdhukuru Allaah, waunge, lakini wakishughulika na mengine, geuka uondoke mbali nao na tafuta wengineo [wanaomdhukuru Allaah].

 

Nimeambiwa na baba yangu kutoka kwa 'Amr Ibn 'Uthmaan kutoka kwa Damura Ibn Hafsw Ibn 'Umar akisema: 'Luqmaan aliweka gunia la chembe za haradali karibu yake na akaanza kumpa nasaha mwanae, kwa kumpa kila nasaha moja chembe moja ya hardali hadi zikaisha zote. Akasema: 'Ewe mwanangu nimekupa nasaha ambazo zingepewa mlima ungelipasuka'

 

'Abdur-Razaaq amesema: Niliambiwa na Hasan kutoka kwa Al-Junayd  kutoka kwa Sufyaan akisema: Luqmaan alimwambia mwanae: 'Ewe mwanangu! Sijapata kujuta kwa sababu ya kukaa kimya. 

 

Ibn Jariyr amenuku kwamba Khaalid ar-Rabaai alisema: 'Luqmaan alikuwa mtumwa wa ki-Ethiopia aliyekuwa na ujuzi wa useremala. Bwana (Tajiri) wake alimwambia: 'Tuchinjie kondoo huyu' Akamchinja, kisha akamwambia: 'Niletee viungo viwili vilivyokuwa ni bora kabisa'. Akampelekea ulimi na moyo. Baada ya siku kupita, alimtaka tena amchinjie kondoo, akachinja kisha Bwana wake akamwambia tena: 'Niletee viungo viwili vilivyokuwa ni viovu kabisa'. Akamletea vile vile ulimi na moyo. Bwana wake akamuuliza: 'Nilipokutaka uniletee viungo bora kabisa umeniletea ulimi na moyo; na nilipokutaka uniletee viungo viovu kabisa umeniletea hivyo hivyo' Luqmaan akamwambia: 'Hakuna vilivyo bora kuliko hivi vinapokuwa vizuri, na hakuna vilivyo viovu kabisa kuliko hivi vinapokuwa vibaya' [At-Twabariy: 20:135]

 

Haya ndiyo tuliyoweza kuyakusanya kumhusu Luqmaan.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share