Ijumaa: Swalaah Gani Za Sunnah Aswali Baada Ya Swalaah Ya Ijumaa

 

Swalaah Gani Za Sunnah Aswali Baada Ya Swalaah Ya Ijumaa

 

www.alhidaaya.com

 

 

SWALI :

 

KWANZA NAPENDA KUTOA SHUKRAN KWA KUTUWEZESHA KUJUA MAMBO MBALIMBALI YA DINI! MWENYEZI MUNGU AWAZIDISHIE KILA LA KHEIR KWA KUTUPA ELMU AMINA.

SWALI LANGU HUENDA LISHAJIBIWA SEHEMU LAKINI NIMEJARIBU KUANGALIA SIJAONA!

 

NAULIZA HIVI! BAADA YA SWALA YA IJUMAA UNATAKIWA USWALI SWALA GANI ZAIDI! JE UNATAKIWA USWALI SWALA ZA SUNA AMBAZO NI BAADA YA SWALA YA FARDHI YA KAWAIDA? NIMEULIZA SWALA HILI MIMI KWA SABABU NIMEONA WATU WANASWALI SWALA ZA RAKAA 4, MARA TATU BAADA YA IJUMAA NAOMBA UFAFANUZI KWANI HILI SILIELEWI! SHUKRAN.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Kuswali raka’ah nne baada ya Ijumaa kuna ushahidi kutokana na Hadiyth kwamba Nabiy  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Akiswali mmoja wenu Ijumaa, aswali baada yake nne” [Muslim kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu).

 

Na Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) amesema: “Hakika yeye (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali baada ya Ijumaa Raka’ah mbili” [al-Bukhaariy na Muslim].

 

Hadiyth hizi mbili zinaweza kuoanishwa: Hiyo ni kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiswali nyumbani kwake, alikuwa akiswali raka’ah 2 na akiswali Msikitini, alikuwa akiswali nne [Shaykh Swaalih Fawzaan, Al-Mulakhkhasw al-Fiqhiy, Mj. 1, uk. 251].

 

Hivyo baada ya Swalaah ya Ijumaa unaweza kuswali mbili au nne kutegemea unaposwali.

 

Lakini kuswaliwa hizo raka’ah nne mara tatu; yaani kwa ujumla rak’ah 12 hatujaona ushahidi wake na hao wanaofanya hivyo.  

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share