Wazazi Hawataki Niolewe Ndoa Ya Pili Na Mume Aliye Mdogo Kwangu

 

SWALI:

Asalam alaykum jamii yote ya kiislam pamoja na ndugu zengu wote mlioko hapa al hidaya mimi ninasuala langu muhimu ambalo linanisumbuwa akili yangu na sitaki kujamulia mwenyewe mpaka nipate jawabu kutoka kwa wislamu wenzangu.

mimi ni mwanamke ambaye niliolewa kama miaka 10 nyuma lakini baada yahapo ilitokea misukosuko mengi naikawa ndowa yangu ilisha na tukaamuwa kuachana na mume wangu natokea nimeachwa sasa ni miezi 8 natalaka zimeisha tayari.na nimezaa watoto watatu na sasa imetokea kheri nyengine  lakini uzito uko kwa wazazi wangu kuwa haitaki hii ndowa iwe kutokana na huyu kijana ni mdogo kwa umri .nikuwa kama atanipotezea time yangu kwakweli tumepishana kwa age yeye ni 25 na mimi 30 na huyo  kijana nimeulizia kwa watu na nimeambiwa nikijana mzuri hata kwa tabia. nategemea kupata jibu zuri kutoka kwenu, ahsanteni

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako. Jamii yetu ya Waislamu hasa Afrika Mashariki ina matatizo mengi ambayo inairudisha nyuma hasa katika mas-ala ya kijamii. Na katika matatizo ambayo yameikumba kwa kiasi kikubwa zaidi mpaka ikakaribia kuisambaratisha jamii hii ni katika mas-ala ya ndoa. Jamii yetu iko nyuma sana na inaonyesha hatujakuwa tayari kutatua changamoto zinazotukabili kwa njia moja au nyingine.

Pia kwa kiasi kikubwa hatuna malezi muruwa katika suala hili. Hivyo, linapokuja tatizo wazazi hutaka kujiamulia hatima ya binti yao bila kujali hisia zake. Je, binti huyo anampenda mume aliyekuja au hampendi si muhimu kwao? Ndoa zetu zimekuwa hazidumu kwa kuwa wazazi wamechukua jukumu la kumchagulia binti yao mume wanaomtaka wao. Lau atakuja mume ambaye binti anamtaka lakini wazazi wasimpende watamlazimisha kuolewa na ikiwa kinyume chake pia watatumia nguvu zao. Haya ni masuala yanayotuletea matatizo mengi katika jamii zetu.

Ingekuwa wazazi wanaielewa Dini basi wangechukua uamuzi muafaka kabisa na kuondosha utata aina yoyote. Uislamu haujakataza mwanamme kumuoa mwanamke aliye mkubwa kumliko yeye. Tunafahamu kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuoa Khadiyjah bint Khuwaylid (Radhiya Allaahu 'anha) aliyekuwa mkubwa wake kwa miaka 15. Tunaposoma katika Siyrah tunaona jinsi gani ndoa hiyo ilivyokuwa na ufanisi wa hali ya juu mpaka mafungamano yao yakawa yanapigiwa mifano kwa maelewano na masikilizano waliokuwa nayo.

Umri wa wanandoa si muhimu kukiwa na masikilizano. Itabidi uzungumze na wazazi wako na uwaeleze kwa njia nzuri kuhusu hayo. Ikiwa umepata habari kwa kuelezwa na unaowaamini kuwa huyo ni kijana nzuri basi itakuwa kheri. Japokuwa tungekunasihi pia uswali Swalah ya Istikhaarah kumtaka ushauri Allaah Aliyetukuka katika mas-ala hayo.

Na ikiwa wazazi bado hawataki kukuozesha kwa sababu zao nyingine ambazo hazikubaliki kisheria basi una haki kutafuta njia nyingine uweze kuolewa na huyo kijana. Kwanza utafute jamaa zako wa karibu kama ami au mjomba au kaka ili  wawe kama walii wako. Na kama hukupata basi mnaweza kumuona Qaadhi na kumfahamisha hali ilivyo na mumuombe akuozesheni. Hii ni kwa sababu ya kujiepusha kuingia katika maasi ikiwa mtaendelea kutakana nyinyi wawili na huku mmezuilika. Jaribu kwanza sana kuwakinaisha wazazi wako hata kwa kuwapatia watu wa kusema nao kuwafahamisha jambo hilo.

Maelezo zaidi soma maswali katika viungo vifuatavyo:

Ndoa Ikiwa Wazazi Hawataki

Wazazi Hawataki Nifunge Ndoa Hadi Nimalize Kusoma Nami Niko Katika Zinaa, Nifanyeje?

 

Tunakuombea tawfiki na ufanisi wa hali ya juu katika suala hilo. Na unapofanikiwa muwe na masikilizano katika kuishi pamoja.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share