Nafsi Nyingine Zimekidhiwa Kuwa Motoni?

 

Nafsi Nyingine Zimekidhiwa Kuwa Motoni?  

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Shukrani zote anastahiki Allah (SW), swali langu linaanza hivi 'Nimewahi kusikia katika mijadala ya kiislam kuhusiana na nafsi ya kwamba zipo nafsi ambazo Allaah (SW) keshaziumba kuwa ni za motoni nahitaji kueleweshwa kuhusiana na hili. In shaa Allaah faida itapatkana.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta’aalaa) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Nabiy. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea na kivivu

 

Ni hakika isiyopingika kuwa yapo baadhi ya masuala ya kidini ambayo hayajaeleweka vyema na hata sisi Waislamu wenyewe. Hivyo huwa kunazuka utata kuhusu hilo ambao unawafitini katika utenda kazi wao wa kidini. Ni juu yetu kuweza kuuelewa Uislamu kwa ukamilifu wake na sio pengine kushika baadhi ya sehemu au kuzielewa kimakosa.

 

Kuhusu hili tutajitahidi kuweka wazi jambo hilo. Suala hili linahusiana na Qadar aliyoiweka Allaah Aliyetukuka. Na katika Qadar hiyo ni wale waliokadiriwa kuingia Motoni. Inafaa mwanzo tuelewe kuwa Allaah Aliyetukuka Ana sifa nzuri na majina matukufu. Miongoni mwayo ni kuwa Yeye ni Mjuzi, Mwingi wa Rehema, Mpole, Muadilifu, Mfalme wa wafalme, Mwenye Kusikia, Ana habari ya yote na kadhalika. Kwa uadilifu Wake, Yeye hamdhulumu wala hatamdhulumu yeyote awe Muislamu au kafiri.  Kuhusu kutodhulumu kwake Allaah Aliyetukuka, Abu Dharr al-Ghifaariy (Radhwiya Allaahu 'anhu) kutokana na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa Sallam) katika aliyoyapokea kutoka kwa Mola Mlezi wake Aliyetukuka kuwa Aliyesema:

 

"Enyi waja Wangu! Mimi Nimejiharimishia dhulma juu ya Nafsi Yangu na nikaifanya ni haramu baina yenu basi msidhulumianeni" [Muslim].

 

Kwa hiyo, tufahamu kuwa Allaah Aliyetukuka Hamdhulumu yeyote na huu ni msingi muhimu ambao tunafaa tuelewe vilivyo kabla hata ya kuingia kulijibu swali lako.

 

Ama tunapoingia katika uliyouliza tungependa kuileta Hadiyth ambayo inafahamika vibaya. Imepokewa Ibn Mas'uud (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba:

 

"Ametuzungumzia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa Sallam) naye ndiye msema kweli wa kusadikika: hakika kila mmoja wenu hukusanywa umbo lake katika tumbo la mamake … Kisha hutumwa Malaika akampulizia roho ndani yake, na akaamrishwa mambo manne: Kuandika riziki yake, ajali yake, amali yake na kama ni mwema au muovu …" (al-Bukhaariy na Muslim, al-Arba'una an-Nawawiyyah, Hadiyth namba 4 au Riyaadhusw Swaalihiyn, Hadiyth namba 396). Hii ni Hadiyth moja ambayo imeeleweka vibaya mpaka Waislamu wengine wanaona kuwa hakuna haja ya kufanya lolote kwani kila mmoja wetu ameandikiwa ima kuwa mwema na hivyo kuingia Peponi au muovu hivyo kuelekea Motoni. Tufahamu Allaah Aliyetukuka Ambaye Ametuumba na Yeye ndiye mwenye habari zote na Mjuzi Anayejua yote atakayofanya mja. Sisi hatujui yaliyoandikwa na Allaah Aliyetukuka, wala hali ya mtu baina yake na Mola Wake, lakini twaona mwisho wake.

 

Hapa twaweza kutoa mfano mmoja wa kibinadamu japokuwa Allaah Aliyetukuka ni Mwenye mifano mizuri zaidi. Kufanya hivyo ni kutaka tuelewane na wasomaji na ndugu zetu. Tunaelewa kuwa waalimu wana vipaji vyao, kimojawapo ni kuweza kumsoma mwanafunzi wake katika kipindi ambacho anakuwa naye. Kwa matokeo anayofanya mwanafunzi mwalimu anaweza kutarajia matokeo yake bila tatizo. Ikiwa mwanafunzi anaanguka katika masomo kwa sababu ya kutosoma au kutohudhuria nyakati za masomo au kwa sababu nyingine yoyote ile. Kwa sababu mwalimu amemsoma mwanafunzi wake akiandika katika karatasi yake na kuiweka katika meza yake kuwa mwanafunzi huyu atafeli kabisa. Natija za mitihani zinapotoka na mwanafunzi akaenda shule kutazama matokeo. Alipofika tu mwalimu wake akamwambia kuwa nilijua kuwa utafeli. Je, mwanafunzi anaweza kusema kuwa aliyenifelisha ni mwalimu wangu. Bila shaka, akisema hivyo atakuwa anatafuta njia tu ya kujitetea na sio hakika. Nasi pia Muumba wetu anayetujua vilivyo kwa maisha yetu kuanzia kuzaliwa kwake mpaka kufariki Anayajua yale tutakayoyafanya hapa duniani.

 

Ili tusiwe na matatizo kabisa Allaah Aliyetukuka Ametupatia viungo vya kutusaidia katika kupata ufanisi hapa duniani na kesho Akhera na pia Akatuteremshia muongozo ili tupate uongofu. Ama wale wanaosema kuwa sisi tushaandikiwa hivyo ni mtu kutaka tu sababu tu ya kutotaka kufanya amali aliyoamrishwa kuifanya.

 

Kuhusu maradhi ya moyo, Allaah Aliyetukuka Anatuelezea:

 

فِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ فَزَادَهُمُ اللَّـهُ مَرَضًا ۖ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ بِمَا كَانُوا يَكْذِبُونَ ﴿١٠﴾

Ndani ya nyoyo zao mna maradhi na Allaah Akawazidishia maradhi, na watapata adhabu iumizayo kwa waliyokuwa wakiyakadhibisha. [Al-Baqarah: 10].

 

Maradhi haya yaliongezeka katika mioyo ya wanafiki kwa sababu hawakutaka kubadilika bali kuendelea na madhambi. Ni hakika kuwa anayetaka kubadilika Allaah Aliyetukuka Anamsaidia mwenye kujisaidia na kurekebisha makosa anayofanya mja. Ni kwa ajili hiyo, Allaah Aliyetukuka Anasema:

 

قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا ۚ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ﴿٥٣﴾

Sema: Enyi waja Wangu ambao wamepindukia mipaka juu ya nafsi zao: Msikate tamaa na rahmah ya Allaah; hakika Allaah Anaghufuria dhambi zote; hakika Yeye Ndiye Mwenye kughufuria, Mwenye kurehemu. [Az- Zumar: 53].

 

Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa Sallam) amesema: "Mja anapofanya dhambi kuna nukta nyeusi inayotiwa katika moyo wake, akiendelea inazidi nukta hiyo kuwa nyeusi. Akitubia na kurudi nukta hiyo hufutwa na moyo ukabaki kuwa safi kabisa".

 

Allaah Aliyetukuka Anatufahamisha kuhusu makundi ambayo yatapatikana kesho Aakhirah kwa yale waliyoyafanya hapa ulimwenguni:

 

يَوْمَ تَبْيَضُّ وُجُوهٌ وَتَسْوَدُّ وُجُوهٌ ۚ فَأَمَّا الَّذِينَ اسْوَدَّتْ وُجُوهُهُمْ أَكَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ فَذُوقُوا الْعَذَابَ بِمَا كُنتُمْ تَكْفُرُونَ ﴿١٠٦﴾وَأَمَّا الَّذِينَ ابْيَضَّتْ وُجُوهُهُمْ فَفِي رَحْمَةِ اللَّـهِ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿١٠٧﴾ 

Siku nyuso zitakuwa nyeupe na nyuso (nyingine) zitakuwa nyeusi. Basi wale ambao nyuso zao zitakuwa nyeusi (wataambiwa): Je, mlikufuru baada ya kuamini kwenu?!  Basi onjeni adhabu kwa yale mliyokuwa mkikufuru. Na wale ambao nyuso zao zitakuwa nyeupe; basi watakuwa katika rahmah ya Allaah. Wao humo ni wenye kudumu. [Aal-'Imraan: 106 – 107].

 

Tufahamu kuwa,

إِنَّ اللَّـهَ لَا يُغَيِّرُ مَا بِقَوْمٍ حَتَّىٰ يُغَيِّرُوا مَا بِأَنفُسِهِمْ ۗ 

"Hakika Allaah Habadilishi yale yaliyoko kwa watu mpaka wao wenyewe wabadilishe yale yaliyomo katika nafsi zao. [Ar-Ra'd: 11]

 

Kwa muongozo aliotupatia Allaah Aliyetukuka ni kama ufuatao:

 

إِنَّا هَدَيْنَاهُ السَّبِيلَ إِمَّا شَاكِرًا وَإِمَّا كَفُورًا﴿٣﴾

Hakika Sisi Tumemuongoza njia; ima (awe) ni mwenye kushukuru au mwenye kukufuru. [Al-Insaan: 3]

 

Ili ufahamu zaidi haya mas-ala, tafadhali ingia katika viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi yanayohusiana nayo:

 

Mema Na Mabaya Yameumbwa Na Allah?

 

Majaaliwa Na Makadario Ya Watu Wema Na Waovu

 

Ikiwa Ameandikiwa Ajiue Vipi Aingie Motoni?

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

Share