Nini Tofauti Ya Nabiy Na Rasuli?

 

Nini Tofauti Ya Nabiy Na Rasuli?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Asalam Alaikum Warahmatullahi Taala Wabarakatu Alah Akulipeni Kwa Kutusaidia Elimu Hii Kwa Njia Ya Alhidaaya Awape Wepesi Na Kuwawezesha Mpate Na Channel Itayorushwa Hewani Inshaalah Swali Langu: Nini Tofauti Ya Nabiy Na Mjumbe Au Mtume.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

‘Ulamaa wamezungumza mengi kuhusu tofauti baina ya Nabii na Rasuli. Kimukhtasari ni kwamba Nabii ni yule ambaye Ametumwa na Allaah (عَزَّوجَلَّ) bila ya kuteremshiwa sharia au hukmu mpya. Ama Rasuli, ni yule ambaye ameteremshiwa sharia mpya na kuamriwa kufikisha Risala kwa watu wake. Hivyo, Nabiy hutumia sharia ya Rasuli aliyemtangulia.

 

Kwa msingi huu, kila Rasuli ni Nabii, lakini si kila Nabii ana sifa ya Rasuli. Na Rasuli ana daraja kubwa kuliko Nabii kwa sababu Rasuli hubalighisha Risala (Ujumbe) kwa watu wake, huwaonya na huwabashiria. Na jukumu hili bila shaka linahitajia kuwa na subira ya hali ya juu kwa sababu watu wao waliwapinga vikali, wakawakadhibisha, wakawashutumu, wakawasingizia sifa mbaya, na wakawafanyia istihzai, dhihaka, kejeli na hata kuwapangia makri kutaka kuwaua. Kati ya hao ni Rusuli watano waliotajwa katika Suwrat Al-Ahzaab (33:7) ambao walitoa fungamano gumu kwa Allaah (سُبْحَانَهُ وَتَعَالَى). Wanajulikana kuwa ni Ulul-‘Azmi; wenye azimio la nguvu. Rejea Al-Ahqaaf (46:35).

 

Imaam Ibn Baaz (رَحِمَهُ اللهُ) amesema: “Linalojulikana sana miongoni mwa ‘Ulamaa ni kwamba, Nabii ni ambaye ameteremshiwa sharia, lakini hakuamrishwa kubalighisha Risala (Ujumbe) kwa watu. Huamrishwa afanye kadhaa na kadhaa, aswali namna kadhaa, afunge Swawm namna kadhaa, lakini haamrishwi kubalighisha Ujumbe kwa watu. Hivyo huyu ni Nabii.  Ama akiamrishwa kubalighisha (Ujumbe) kwa kuwabashiria na kuwaonya watu, huyo anakuwa ni Nabii na Rasuli kama vile Nabiy Muhammad (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمَ), Muwsaa, ‘Iysaa, Nuwh, Huwd, Swaalih (عَلَيْهِم السَّلام) na wengineo”. [Mawqi' Ar-Rasmiy li-Samaahat Ash-Shaykh Ibn Baaz]

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share