Wakristo Wanadai Kuwa Waislamu Tanzania Wameletewa Elimu Na Wazungu Na Si Na Waarabu

 

SWALI:

Swali langu ni kwamba wakristo wanadai sisi waislam hatukusoma, wakimaanisha kuwa hii elimu ya sasa [shule] walikuja nayo wazungu kwa maana ya [wakristo] sasa ikiwa hivyo ndivyo mbona mimi nasikia kuwa kilwa ktk karne ya kama 15 au 16 ivi kulikuwa na dola ya kiislam? Je wao walikuwa wakisoma ktk taratibu zipi? Wanakazia kwa kusema eti mwarabu hakuleta shule naomba mnisaidie shukrani.

Mkamilifu ni ALLAH. 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako hilo zuri kuhusu elimu na shule. Hakika ni kuwa watu wote kwa ujumla wana utata mkubwa kuhusu mas-ala ya elimu na shule. Kabla hatujaingia katika kiini cha maudhui yenyewe tungependa kuwafahamisha kuwa Waislamu kila walipokwenda walileta na kuanzisha Madrasah kwa ajili ya watoto na watu wazima. Je, Madrasah ni nini? Madrasah ni neno la Kiarabu lenye maana ya skuli au shule kwa lugha ya Kiswahili.

Uislamu umehimiza sana mas-ala ya elimu na kuendeleza masomo kwa kila mmoja. Ndio ukakuta kuwa kila mahali Waislamu walipokwenda walianzisha Madrasah kwa ajili ya kuwafundisha watoto na watu wengine elimu tofauti. Qur-aan na Sunnah za Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa sallam) zimehimiza sana Waislamu na watu kwa ujumla kutafuta ukweli, kutumia akili na kutafuta elimu. Ukosefu wa elimu katika Uislamu ni ujahili (ujinga). Hata hivyo, ulifika wakati ambapo Waislamu waliacha kutafuta elimu na kuingia katika anasa na starehe mpaka tukafika tulipo sasa tukiwa hatuna mbele wala nyuma katika mas-ala ya elimu.

Tufahamu kuwa Uislamu haukubagua baina ya elimu inayoitwa ya Kidini na ile ya kilimwengu. Kila tunachosoma cha halali ni lazima tukisome kwa jina la Allaah Aliyetukuka. Wakati Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa sallam) anaaga dunia alikuwa tayari amewaachia Maswahaba zake Qur-aan iliyokamilika na Sunnah zake safi na akawaambia:

'Yeyote atakayeshikama nazo hatapotea daima dawamu'.

Katika hali hiyo Maswahaba (Radhiya Allaahu 'anhum) walipiga hatua katika elimu kwa kasi sana pale walipotawanyika katika ardhi ili kuusambaza Uislamu kwa njia zilizo nzuri sana. Ilipokuja dola ya Bani Umayyah na baadaye Bani 'Abbaas, Waislamu walianza kuingilia kutafsiri na kusoma vitabu vya Wayunani (wagiriki) na nadharia zao katika Sayansi. Ilikuwa si kusoma na kutafsiri tu bali walianza kufanya tafiti kuhusu hayo. Katika kufanya hayo wakapiga hatua kwa kuvumbua mengi, na kuendeleza utafiti katika masomo yanayoitwa ya kisasa. Na zipo nadharia hizo za kisayansi walizozibadilisha kwa kuziona kuwa hazikwenda sambamba na sayansi hiyo.

Waliokuwa katika msitari wa mbele kwa kufanya utafiti na kuendeleza elimu ni kama wafuatao:

  1. Jaabir bin Hayyaan, aliyefariki 815 M alikuwa mwanakemia wa kutambulikana mpaka akapatiwa jina The Father of Chemistry (baba wa Kemia). Naye alivumbua acid, na njia za utengenezaji vitu kama distillation, evaporation, extraction, crystallization, na kadhalika. Aliweza kutengeneza Sulphuric acid na kadhalika. Jina lakelimebadilishwa ili asiweze kufahamika anajulikana Kilatini kama Geber.

  2. Khalaf bin 'Abbaas al-Zahrawi (930 – 1013 M), anayejulikana kama Bucasis. Aliandika encyclopedia ya upasuaji (surgery) na vitabu vyake vilitumika katika Vyuo Vikuu vya Magharibi hadi karne ya 19 miladi.

  3. Ibn Rushd (1126 – 1198 M), akijulikana kama Averroes, anayejulikana katika masomo ya fiziolojia na ametoa mchango wake kwa kuandika vitabu vya utabibu.

  4. 'Alaa ad-Diyn bin el-Nafis (1208 – 1288M), ndiye wa kwanza aliyeelezea kuhusu mzunguko wa damu katika mwili wa mwanadamu kwa uhakika zaidi karne tatu kabla ya Michael Servetus. Pia alikosoa zile nadharia za kina Galen kuhusu hilo.

  5. Waislamu walipiga hatua katika magonjwa ya macho na matibabu yake na pia utumiaji wa madawa yanayomlaza mgonjwa kabla ya kufanywa upasuaji.

  6. Pia upasuaji wa wanawake waliokuwa na shida katika mazazi. Majina yanayotajika katika hilo ni al-Firdaws na al-Biruni.

  7. Waislamu walikuwa na mohospitali yaliyokuwa yamepangika zaidi ya hospitali zetu. Hospitali ya kwanza iliyoanzishwa ni ile ya Damascus mwaka wa 706 M. Na zilikuwa nyingi nyinginezo huko al-Quds, Misri, Iraq, Afrika Kaskazini, Andalus (Spain na kadhalika.

 

Tatizo lilikuja wakati wa karne ya 15 Miladi pale Waislamu walipotolea Andalusia mwaka wa 1492 na kuingia katika starehe. Jambo hilo lilifanya Waislamu waanze kurudi nyuma katika elimu na kuanza kupenda watu wa Magharibi kwa kutia juhudi. Juhudi hii ilikuwa ni katika kufasiri vitabu vilivyoandikwa na wataalamu wa Kiislamu katika karne nyingi zilizopita na kuziendeleza. Kuonyesha umahiri wa Waislamu ni kule Vasco da Gama alipofika mwambao wa Kenya (Lamu, Malindi na Mombasa) mnamo mwaka 1498 huku akitafuta njia ya kufika India lakini akashindwa kufanya hivyo mpaka aliposaidiwa na Waislamu.

Tunafahamu Uislamu uliingia Kilwa takriban karne ya 13 hivi. Kwa kuwa Waislamu walikuwepo hapo watakuwa na Madrasah zao za kuweza kuwafundisha watoto wao na hata watu wazima walioingia katika Dini hii. Tatizo tulilonalo sisi ni kuwa mtu ikiwa hakusoma masomo kwa lugha ya kiingereza basi hatumtambui kuwa ni msomi. Leo tunapata wasomi ambao hawajui Kiingereza lakini kwetu huwa bado ni wajinga. Hakika jambo hili si sawa.

Katika mji wa Lamu, kulikuwa na Madrasah hata kabla ya kuja kwa Wazungu. Na katika Madrasah hizo wanafunzi walikuwa wakifundishwa si tu kusoma Qur-aan bali pia Hesabu, Historia, Jiografia na hata Sayansi kwa lugha ya Kiarabu. Na Kilwa pia ilikuwa hivyo. Na katika mji huo wa Lamu kulikuwa na matabibu (madaktari) karne nyingi zilizopita na hata katika miaka ya 70 kulikuja Mzungu aliyekwishamaliza madawa kwa ugonjwa aliokuwa nayo katika hospitali zote duniani. Alikuja pale na kutibiwa kwa tiba mbadala na kutoa katika tumbo lakekitu kikubwa kilichokuwa ndani. Yapo magonjwa mengi kwa sasa pia ambayo hayatibiki isipokuwa kwa tiba hii ambayo inajulikana kamaTwibb an-Nabawiy (Tiba ya Mtume).

Baada ya kusemwa hayo yote, hapa tunafupisha kwa kusema kuwa elimu na mfumo wake kama ulivyo sasa kwa hakika umeletwa na Wazungu waliokuja kututawala. Na jambo hilo si la ajabu kwani elimu hasa za Sayansi zinaendelea kila uchao na nadharia iliyo sahihi leo kesho itakuwa ni uongo. Hivyo, tunatakiwa nasi tufanye juhudi katika kuiendeleza elimu zenye manufaa. Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa sallam) ametuagizia:

'Hekima (elimu) ni kitu kilichompotea Muislamu, anapoipata huichukuwa' (Abu Daawuud). Na katika riwaya nyingine: 'Anapoipata ana haki zaidi nayo'.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share