Kutumia Kitu Kujitoa Matamanio Nini Hukmu Yake

 

Kutumia Kitu Kujitoa Matamanio Nini Hukmu Yake

 

Alhidaaya.com

 

Swali:

 

Asalam Alaykum ndugu waislamu, nimetumwaga na mwislamu niwaulize, je mtu akiwa mbali na mchumba wake, alafu akatamani kufanya tendo la ndoa, alafu akachukua kitu akaweka katikati ya miguu kwenye tupu lake bila kuingiza ndani, mpaka akahisi ile haja yakufanya tendo la ndoa ina malizika na akatokwa na manii; hicho kitendo ni haramu? na anatakiwa kuoga janaba? asante.

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho. 

 

Hakika ni kuwa kwa sababu ya kuingiliana na mataifa mengine mengi yasiyokuwa na ada na desturi kama zetu tumekuwa ni wenye kuwaigia kwa sababu moja au nyingine.

Kuhusu mas-alah haya Allaah Aliyetukuka Anatuambia:

وَالَّذِينَ هُمْ لِفُرُوجِهِمْ حَافِظُونَ ﴿٥﴾إِلَّا عَلَىٰ أَزْوَاجِهِمْ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُمْ فَإِنَّهُمْ غَيْرُ مَلُومِينَ ﴿٦﴾فَمَنِ ابْتَغَىٰ وَرَاءَ ذَٰلِكَ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْعَادُونَ ﴿٧﴾

Na ambao wanazihifadhi tupu zao. Isipokuwa kwa wake zao, au kwa iliyowamiliki mikono yao ya kuume basi hao hawalaumiwi. Lakini atakayetaka kinyume ya hayo; basi hao ndio wapindukao mipaka. [Al-Muuminuwn: 5–7].

 

Aayah ya saba inayosema:

فَمَنِ ابْتَغَىٰ وَرَاءَ ذَٰلِكَ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْعَادُونَ ﴿٧﴾

Lakini atakayetaka kinyume ya hayo; basi hao ndio wapindukao mipaka.

 

Ni ibara ya jumla ambayo inajumlisha kutekeleza matamanio kinyume na ile njia ya ndoa (yaani mume kufanya kitendo cha ndoa na mkewe kwa njia ile moja. Inaingia hapa zinaa, liwati na kujichua au njia nyingine mfano ni ile uliyoitaja.

 

Kuhusu hili Sa'iyd bin Jubayr, ambaye ni Tabii' mchaji Allaah, Mwanachuoni amesema: "Allaah Atauadhibu Ummah kwa kuchezea nyuchi zao (tupu za mbele". Na imepokewa pia: "Watu saba Allaah Hatowaangalia … Akawahesabu miongoni mwao: mwenye kuoa mkono wake (kupiga punyeto)" [Muhammad Al-Haamid, Ruduud 'alaa Abaatwiyl, uk. 40].

 

Kwa muhtasari ni kuwa kitendo hicho unachofanya ni haramu katika Uislamu. Kwa hiyo, nasaha yetu kwako ni kuwa ni wajibu kwako kuoa au kuolewa. Hakika ibara uliyoitumia niko mbali na mchumba wangu ina utata kwani katika Uislamu huwezi kufanya tendo la ndoa na mchumba wako kwani hajakuwa ni mkeo au mumeo. Ila ikiwa umemaanisha kwa ibara mchumba ni kuwa tayari umemuoa au umeolewa naye, na ni wako wa halali. Na ikiwa ni mkeo au mumeo wa halali basi ni vyema pale ulipo umchukue mumeo au mkeo ili usipate shida uliyo nayo.

 

Ama ikiwa umefanya kitendo hicho cha madhambi mwanzo unatakiwa umuombe msamaha Allaah Aliyetukuka, ujute na uazimie kutorudia tena. Na lau katika kufanya kitendo hicho utatokwa na manii basi itabidi ili uweze kufanya Ibaadah tofauti uoge josho la janaba. 

 

Pia soma katika kiungo hiki upate kuyajua masuala hayo kwa upana zaidi:

 

Nini Hukumu Ya Kujichua Sehemu Za Siri Au Kujisaga?

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share