Ndoto Anazoota Zinatokea Kweli Hadi Zinamtia Khofu

 

SWALI LA KWANZA:

 

ndugu zangu Waislam tunawashukuru kwa kutujibu maswali yetu na Vilevile kabla ya kumsahau Allah (SWT) na Mtume wake (S.A.W) kwa kutongoza katika mambo ya kheri na kutupa afya njema. Na nyinyi Allah awabariki.

 

swali langu ni kwamba mimi ninaoteshwa lakini kama kweli maana yake vitu ninavyootesha vinatokea vile vile nilivyoota je hii hasa inakuwa ni nini maana yake mpaka naogopa sana maana mambo mengine yanatisha saa nyingine naota napaishwa na nafika nchi nyingine kwa kweli ninaogopa sana na nilimuuliza ustadhi mmoja akasema usiseme yaani usiwaambie watu hizo ni ndoto za manabii ambazo hutakiwi kusema na ukisema waweza rukwa na akili maana Allah anakuonyesha miujiza yake.

 

Naomba jibu kwa kweli inanitisha.

 

Allah awape wepesi wa kunijibu swali langu hili. Inshaalllah.

 

Assalam aleykum,

Sinabudi kumshukuru Allah na Mtume wake Muhammad (S.A.W) na watangu wema waliotangulia.

 

vipi hali zenu kama wazima nashukuru mungu na mimi pia mzima Allah awalipe Inshallah kwa kutuelimisha katika dini yetu Alhamdullilah.

 

Swali langu ni kuwa Mimi ni msichana wa umri wa miaka 30 Ninaota ndoto ambazo zinatokea hivyo hivyo nilivyoota hivi hii inakuwaje maana mpaka naogopa kwa sababu inatisha Wallah maana ndoto zake kama mfano wa atakufa mtu, au kupaishwa na kupelekwa nchi jirani na kuona vitu ambavyo sijawahi kuona kwa kweli na nikiuliza inakuwa kweli vipi kuhusu habari hii. Maana kuna ma ustadhi niliwauliza kuwa je hii ni Ishara ya Allah (swt) ama nini? Wakasema usihadhisie watu halafu wewe ni mchamungu nikweli habari hii

 

Naomba jibu Inshaallah Allah awabariki.

 

SWALI LA PILI:

 

assalam aleykum

 

Baada ya kumshukuru Allah na Mtume wake Muhammad (S.A.W)

 

SWALI: mimi ninaoteshwa ndoto halafu zinatokea kweli hii inatokea na ucha mungu au kitu gani inakuwa.

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta’ala) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Mtume. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea na kivivu

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako zuri kuhusu ndoto ambazo zimeelewa kwa kifupi au kwa urefu. Maswali haya mawili yanafanana hivyo tutayachanganya na kuyajibu kwa mpigo mmoja.

 

Ama kuhusu mas-ala haya ya ndoto ni mambo yaliyoelezewa na Uislamu. Hapa tutajaribu kuyafafanua kwa kifupi ili tupate angalau uelewo wa jambo hilo. Ndoto zimegawanyika sehemu mbili, nazo ni kama zifuatazo:

 

  1. Ndoto nzuri inatoka kwa Allaah Aliyetukuka.
  2. Ndoto mbaya inatoka kutoka kwa Shetani aliyelaaniwa.

 

Aina hizi zimeelezewa katika Hadiyth kadhaa ambazo tutazitaja hapa kwa faida ya waulizaji na wengine wenye kuingia katika tovuti hii ya Alhidaaya.

 

Abu Qataadah (Radhiya Allaahu 'anhu) anasema:

Nimemsikia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: "Ndoto nzuri (Ru'ya) inatokana na Allaah, na ndoto mbaya (Hulmu) inatokana na shaytwaan, hivyo anapoota mmoja wenu ndoto asiyoipenda basi anapoamka, ateme mara tatu, na ajilinde kwa Allaah na shari ya ndoto hiyo, kama atafanya hivyo haitamdhuru" (al-Bukhaariy na Muslim).

 

Hadiyth nyingine ni ile ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) aliyesema kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

"Zama zinapokaribia (za kufufuliwa) ndoto ya Muumini haitaongopa, na ndoto ya Muumini ni sehemu moja ya sehemu arubaini na sita ya Unabii" (al-Bukhaariy na Muslim).

 

Sehemu ya pili ya Hadiyth hii ya mwisho, inayosema: " ndoto ya Muumini ni sehemu moja ya sehemu arubaini na sita ya Unabii" (al-Bukhaariy na Muslim kutoka kwa 'Ubadah bin asw-Swaamit, Anas bin Maalik na Abu Hurayrah).

 

Ikiwa mtu ana wasiwasi kwa ndoto anayoota basi ni vyema afuate maagizo ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth ya kwanza hapo juu. Ukitia shaka kuwa ndoto hiyo ni mbaya basi usimuelezee mtu yeyote. Pindi utakapofanya hivyo basi shari yoyote itaponyoka wala haitakukaribia na kukufikia wewe kwa njia.

 

Hadiyth nyingine zinatufahamisha kule kuota na kutokea kama ulivyoota ni ishara nzuri ya ucha Mungu. Hivyo ni neema kwa mja na unapaswa umshukuru  Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwa neema hiyo na uzidishe taqwa.  Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuelezea kuwa ni sehemu katika sehemu ya Unabii (1/46 = 2.17%). Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa kabla ya kupatiwa Unabii alikuwa anaoota ndoto ambazo baadaye zilikuwa zinatokea kama alivyoota lakini baada yake hakuna tena Unabii kwani yeye (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndiye Mtume wa mwisho.

 

Ndoto kutokea kweli kama alivyoota ni ishara na alama ya kuwa Siku ya Qiyaama imekaribia. Kwa ajili hiyo tunatakiwa sisi tufanye juhudi kwa kufanya ‘Ibaadah ili tusije tukakhasirika vibaya sana kesho Akhera.

 

Mara nyingine hizi ndoto tunazoota huwa zinatokana na yale tuliyokuwa tukiyafikiriya asubuhi au tunapokuwa macho. Kwa hivyo, huwa ni kama kuendeleza zile fikra tulizokuwa nazo au kuzirudia. Na tashwishi tuliyopata kwenye swali lako ni huko kupaa kwenda nchi jirani au kuelekea mbinguni. Huko kupaa kunatokea kweli au suala hilo limetiwa katikati ya mambo mengine yaliyotokea?

 

Ama hao maustadhi na watu wanakupa ufafanuzi au tafsiri hizo, hakika si wa kuwaamini sana. Si rahisi kupata wanaojua kutafsiri ndoto, na wengi wanaodai kutafsiri ndoto huwa wanatafsiri kuridhisha waotao na huwa si tafsiri za kweli na za kisheria. Hata kitabu cha tafsiri za ndoto kinachodaiwa ni cha Imaam Ibn Siyriyn, Maulamaa wanasema si kitabu chake bali kimenasibishwa naye pamoja na kuwa yeye alikuwa ni mfasiri ndoto mkubwa wa kuaminika.

 

Kwa hali zote inatakiwa tuwe ni wenye kumtaja na kumdhukuru Allaah Aliyetukuka wakati tunakwenda kitandani ili Atuepushe na wasiwasi wa shetani na wasaidizi wake.

 

Soma Adhkaar mbalimbali hapa chini za kukusaidia unapolala na unapokumbana na ndoto mbalimbali.

 

 

 

Tunawaombea kila la kheri na tawfiki katika mambo yenu na Waislamu wote duniani.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share