Kula Nyama Isiyochinjwa Kihalali Katika Nchi Ya Kigeni Inafaa?

 

SWALI:

Napenda kumshukuru Allah kwa kutupa uzima nakuendelea na shughuli zetu za kila siku. Napenda kuuliza suala, mimi nipo nje ya nchi nakula mkahawani nchi ambayo watu wake si waislam, nimenunua kuku ambae hakuchinjwa kihalali nikamla kwa vile sina njia nyengine ya kunipatia chakula. Jee nitakuwa ninakosea au nini hukumu yake? Ahsante sana. natanguliza shukurani zangu za dhati.JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako. Ama kuhusu mas-ala ya chakula kilichopikwa na Ahlul Kitaab ambacho si nyama hakina tatizo kabisa kula. Tatiz linakuja katika nyama ambazo zinachinjwa katika zile zilizo halali. Ikiwa nyama hizo zimechinjwa na mushirikina basi moja kwa moja hufai kula kwa hali yoyote ile. Katika hali hiyo inabidi utafute sehemu mbadala au upike nyumbani kwako..

Ama ikiwa nchi unayoishi ni ya Wakristo, basi Uislamu umekuruhusu kula vyakula wanavyopika. Kuhusu hilo Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:

"Leo mmehalalishiwa kila vilivyo vizuri. Na chakula cha waliopewa Kitabu ni halali kwenu, na chakula chenu ni halali kwao" (5: 5).

Ni muhimu kabisa uingie katika viungo vifuatavyo upate maelezo na ufafanuzi zaidi ya mas-ala haya   

Nyama Ya Halaal Uchinjaji Wake

Chakula Cha Halaali

Je, Wanyama Wanaochinjwa Na Mayahudi Ni Halali Kula?

Lakini tunavyojua, hakuna sehemu yoyote duniani hivi sasa utaweza kukosa chakula dukani kisichokuwa na mashaka. Na si lazima mtu ule kuku au nyama ikiwa una mashaka nayo. Na ikiwa unakusudia kuwa hapo ulipo kuna kuku tu na hakuna njia nyingine ya kukupatia chakula, hatujui unakusudia chakula kwako ni kuku au nyama, na vingine kama mikate, wali, n.k. si vyakula?

Hatudhani kuwa wewe uko jangwani au msituni ambako hakuna chakula. Maadam uko mjini, basi bila shaka utapata vyakula vya aina nyingine vilivyo halali na visivyo na mashaka, ma ukitafuta zaidi huenda uapata mikahawa ya Waislam au maduka ya halali. Siku hizi nchi za Kimagharibi maduka ya Halaal yamejaa tele kila mji, hivyo hatuona sababu ya Muislamu kulazimika kula chakula kisichokuwa cha halaal.

Jitahidi sana kutafuta njia mbadala na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atakupatia bila ya shaka yoyote.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share