Tunda Ambalo Alikula Adam Na Bibi Hawwaa

SWALI:

as salaam aleikum, mimi naitwa mussa ni mkaazi wa unguja na ambae ni mfuatiliaji sana wa darsa za maalim othman, lakini hivi sasa nipo turkey, nilikuwa nauliza kwamba kunu tetesi kuwa lile tunda ambalo walokula nabii adam na bi hani kitendo cha kujaamiana, sasa ni kweli au pr

 

 

 


 

JIBU:

 

 Tunamuhimidi Allah ambaye kwa neema Yake yanatimia kila yaliyo mema na mazuri na Akatufanya ni miongoni wa wenye kufuata Sunnah za Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Ninamshukuru ndugu yetu kwa swali lake hilo japokuwa sehemu ya mwisho haijafahamika vyema (sehemu niliyoipiga msitari). Hakika zipo rai nyingi na tofauti kuhusu mti aliokatzwa Nabii Aadam (‘Alayhis Salaam) kuukurubia. Tofauti hizi zipo baina ya Maswahaba na watangu wema waliokuja baada yao. Na katika hilo mufassirina wametofautiana wapo ambao hawakutaja majina ya miti yenyewe na wapo wale ambao walijitahidi na kuitaja kama katika tafsiri ya Ibn Kathiyr, na Ash-Shawkaaniy na Al-Qurtubiy. Wao wametoa tofauti za wanazuoni na kusema kuwa mti huo ulikuwa ni wa mzabibu, na wengine wanasema wa shayiri, mtende, mtini na kadhalika. Lakini Ibn Kathiir ameongeza kuwa hakuna aya ya wazi inayotaja jina la mti huo wala Hadithi Sahihi kuhusu jambo hilo.

 

Lililo muhimu ni kuwa kuujua mti aliokula Nabii Aadam (‘Alayhis Salaam) na mkewe haitotufaidi sisi kwa chochote. Imani yetu haitazidi wa kupungua kwa kuujua au kutoujua. Na sisi kama Waislamu hatufai kupoteza muda mwingi sana katika jambo kama hilo kwani Muislamu hana wakati katika huu ulimwengu kuupoteza au kuukata kwa kuuua. Kila nukta inahesabiwa na tutakwenda kuulizwa kuhusu ujana wetu na umri wetu Siku ya Kiyama. Hivyo, tuachane na mijadala au tafiti kama hizo.

 

Fundisho tunalopata muhimu katika maisha yetu kuhusu kisa cha Aadam (‘Alayhis Salaam) na mkewe ni kuwa shetani ana njia nyingi za kumpoteza mwanadamu na anakuja kwa njia nzuri. Na hii njia tunaiona hapa pale Iblis alipowaambia: “Naye akawaapia: Kwa yakini mimi ni mmoja wa wanao kunasihi. Basi akawateka kwa hadaa.” (7:21-22)

 

Na Allaah Anatueleza kwa uwazi kuhusu shaytwaan, Aliposema:

 “Wala msifuate nyayo za shaytwaan, hakika yeye kwenu nyinyi ni adui aliye wazi” (2: 208)

Hivyo, inafaa tujichunge sana tusije tukaingia katika mitego yake na hivyo kuhasirika hapa duniani na kesho Akhera.

 

Nukta ingine ni kusahihisha jina la mkewe Nabii Aadam (‘Alayhis Salaam), ambalo kaka yetu kasema ni bi Hani na huu ni ubinadamu kukosea. Hakika ni kuwa jina la mkewe lilikuwa ni Bi Hawwaa. Natumai katika sentensi iliyopigwa msitari ndugu yetu atatufafanulia ili tuweze kumjibu kwa hilo pia.

 

Na Allaah Anajua zaidi 

 

 

Share