Mashairi 3: Ramadhani Kutufika, Twamshukuru Rahimu

 

 

Mashairi 3:  Ramadhani Kutufika, Twamshukuru Rahimu.

 

      ‘Abdallah Bin Eifan (Rahimahu-Allaah)

 

 Alhidaaya.com

 

 

 

Salamu Waislamu, kalamu nashikilia,

Tumo katika saumu, Mungu Anashuhudia,

Tunamuomba Karimu, ibada twazingatia,

Ramadhani kutufika, Twamshukuru Rahimu.

 

 

 

Lijalo kumi la pili, tunazidi kusogea,

Waumini hawalali, usiku wajisomea,

Wapo katika shughuli, maghfira kulilia,

Ramadhani kutufika, Twamshukuru Rahimu.

 

 

 

 

Dhambi zetu nyingi sana, Mungu tunakutubia,

Tusamehe Maulana, na radhi kutujalia,

Viumbe tunashindana, pepo kuipigania,

Ramadhani kutufika, Twamshukuru Rahimu.

 

 

  

Wanaocheza karata, wakati unapotea,

Lini tena watapata, nafasi ya kuombea,

Wakati unawapita, mwisho watajijutia,

Ramadhani kutufika, Twamshukuru Rahimu.

 

 

 

Wengine televisheni, kutwa wanajionea,

Hujuwi kama mwakani, upo katika dunia,

Haraka ndugu fanyeni, wakati umewadia,

Ramadhani kutufika, Twamshukuru Rahimu.

 

 

 

Ukienda haurudi, mwezi unatukimbia,

Mwezi tena ukirudi, pengine tumejifia,

Kwa Mungu tukisharudi, hakuna nyingine njia,

Ramadhani kutufika, Twamshukuru Rahimu.

 

 

 

Kwa hivyo ombeni sana, mwisho unakaribia,

Someni sana Qur-ani, thawabu kujipatia,

Hizo akiba wekeni, akhera husaidia,

Ramadhani kutufika, Twamshukuru Rahimu.

 

 

 

Mwezi huu tazameni, bahati kuufikia,

Maiti anatamani, arudi kuhudhuria,

Lakini haiyumkini, muhali kuturudia,

Ramadhani kutufika, Twamshukuru Rahimu.

 

 

 

Ghafla na bila hodi, mauti yanakujia,

Huwezi kusema “Rudi,” apate kukuachia,

Imeshafika ahadi, nani atakutetea,

Ramadhani kutufika, Twamshukuru Rahimu.

 

 

 

Mwezi huu ni adhimu, Mungu Ametujalia,

Kila dakika muhimu, fanya kheri na tulia,

Uwe sana mkarimu, na watu kusaidia,

Ramadhani kutufika, Twamshukuru Rahimu.

 

 

 

Mtu ukimdhulumu, haki yake rudishia,

Cha haramu hakidumu, mwisho kinateketea,

Utaharibu saumu, Mungu hatokubalia,

Ramadhani kutufika, Twamshukuru Rahimu.

 

 

 

Kawatazame wagonjwa, nenda kuwatembelea,

Jambo hili linapendwa, Mtume kahadithia,

Siku wewe ukilazwa, waje kukuangalia,

Ramadhani kutufika, Twamshukuru Rahimu.

 

 

 

Ni kumi hili tazama, Maghfira za Jalia,

Usiku kucha simama, soma, omba kisheria,

Usile daku mapema, baraka ukingojea,

Ramadhani kutufika, Twmshukuru Rahimu.

 

 

 

Harakisha kufuturu, adhana ukisikia,

Usikose kudhukuru, dua ya kufungulia,

Muumba Tumshukuru, chakula kutupatia,

Ramadhani kutufika, Twmshukuru Rahimu.

 

 

 

Kumbuka walionyimwa, nini watatafunia,

Ndivyo walivyojaliwa, Mungu Kawaandikia,

Kama wewe umepewa, shukurani ongezea,

Ramadhani kutufika, Twamshukuru Rahimu.

 

 

 

Shukuru Yake neema, Apate Kuzidishia,

Fanya kitu kwa kupima, israfu ndio udhia,

Omba ibaki daima, neema itabakia,

Ramadhani kutufika, Twamshukuru Rahimu.

 

 

 

Kula futari khafifu, usije ukaumia,

Uondoe na harufu, mswaki kuutumia,

Usichelewe halafu, msikiti kimbilia,

Ramadhani kutufika, Twamshukuru Rahimu.

 

 

  

Njaa si maana ya saumu, chakula kukisusia

Kila kilicho haramu, hapana kukaribia,

Saumu Yake Rahimu, Yeye Anakulipia

Ramadhani kutufika, Twamshukuru Rahimu.

 

 

 

Harufu mbaya kinywani, mchana ikitokea,

Kwa Mungu miski mbinguni, harufu ya kuvutia,

Anaipenda Manani, harufu ikimfikia,

Ramadhani kutufika, Twamshukuru Rahimu.

 

 

 

Mtume huwa mpole, sana wakupindukia,

Kila kitu polepole, hubadilika tabia,

Utadhani sio yule, wa kila siku Nabia

Ramadhani kutufika, Twamshukuru Rahimu.

 

 

 

Ukila kwa makusudi, machana ukiingia,

Hata ukijitahidi, mwaka wote kufungia,

Mema yako yatarudi, huwezi ukafidia,

Ramadhani kutufika, Twamshukuru Rahimu.

 

 

 

Dunia ni mtihani, hapa tunapita njia,

Akhera ni maskani, milele tutaishia,

Motoni au peponi, zote ni haki sawia,

Ramadhani  kutufika, Twamshukuru Rahimu.

 

 

 

Ukumbuke ndugu zako, na hali kuwajulia,

Wote na binamu zako, wajomba, shangazi pia,

Pamoja na dada zako, dini imetuambia

Ramadhani kutufika, Twamshukuru Rahimu.

 

 

 

Rehema Zako Jalali, Tunakuomba kwa nia,

Wewe unajua hali, Waona na Kusikia,

Hapa nimefika mbali, sasa nafunga pazia,

Ramadhani kutufika, Twamshukuru Rahimu.

 

 

 

 

Share