Mashairi: Aibariki Manani, Tovuti Ya Alhidaaya - 1

 

‘Abdallaah Bin Eifan (Rahimahu-Allaah)

www.alhidaaya.com

 

 

Narusha salaam zangu, kwa mapenzi na imani,

ziwafikie wenzangu, popote ulimwenguni,

tushikamane nduzangu, kwa umoja na amani,

Aibariki Manani, Tovuti ya Alhidaaya.

 

 

Tovuti ya Alhidaaya, Aibariki Manani,

ifike hadi ulaya, hata huko Marekani,

wazuri hata wabaya, waisome kwa makini,

Aibariki Manani, Tovuti ya Alhidaaya.

 

 

Watu wananufaika, kusoma mambo ya dini,

wengi wanafaidika, makala zenye thamani,

Ndugu wanashughulika, kutuletea yakini,

Aibariki Manani, Tovuti ya Alhidaaya.

 

 

Wote wanaohusika, Allaah waweke peponi,

wazidishie baraka, akhera na duniani,

waepushe na mashaka, wawe na matumaini,

Aibariki Manani, Tovuti ya Alhidaaya.

 

 

Sahalisha kazi yao, gumu lifanye laini,

Hifadhi thawabu zao, katika yao mizani,

Waweke kwenye makao, makao ya wahisani,

Aibariki Manani, Tovuti ya Alhidaaya.

 

 

Nchi zimeharibika, ametawala shetani,

tabia zimechafuka, kila pembe ardhini,

umeshavuka mipaka, ufisadi mitaani,

Aibariki Manani, Tovuti ya Alhidaaya.

 

 

Watu wanakunywa pombe, na wanapenda kuzini,

wengine humeza chembe, na unga wa heroini,

wengine kwenye vipembe, wengine mabarazani,

Aibariki Manani, Tovuti ya Alhidaaya.

 

 

Tumuombe Subhana, Aondoshe kisirani,

Awaongoze vijana, pamoja na wana-ndani,

si usiku si mchana, dua ziwe mdomoni,

Aibariki Manani, Tovuti ya Alhidaaya.

 

 

Tuepuke na ghadhabu, Ghadhabu za Rahmani,

tuepuke na adhabu, ya moto na kaburini,

tuwawekee adabu, wazazi na majirani,

Aibariki Manani, Tovuti ya Alhidaaya.

 

 

Hapa ndio kaditama, kalamu naweka chini,

dunia tutaihama, hapa ndio mtihani,

hapo siku ya kiama, ataepasi ni nani?

AIBARIKI MANANI, TOVUTI YA ALHIDAAYA.

 

 

Share