Mashairi: Kudura Na Imani

 

Kudura Na Imani

             ‘Abdallaah Bin Eifan (Rahimahu Allaah)

           

 

Salaam waheshimiwa, nawaombea baraka,
tunaomba kujaliwa, kila kheri na fanaka,
tupate kuokolewa, tutoke kwenye mashaka,
Lazima kitakufika, kile kilichoandikwa.

 

 

Kile kilicho andikwa, lazima kitakufika,
nahodha anaposhindwa, bahari ikichafuka,
na rubani kwenye hewa, ndege ikipeperuka,
Lazima kitakufika, kile kilichoandikwa.

 

 

Mvuvi anapovua, samaki kukusanyika,
akikosa anajua, leo Allaah Hakutaka,
hawezi kujisumbua, kununa kukasirika
Lazima kitakufika, kile kilichoandikwa.

 

 

Mkulima hushtushwa, shamba moto likiwaka,
ajue akiulizwa, kama ametoa zaka,
asiseme kasakamwa, au mkosi umefika,
Lazima kitakufika, kile kilichoandikwa.

 

 

Biashara  ikifanywa, na ukifungua duka,
kama hukufanikiwa, uache kunung'unika,
pengine hudhulumiwa, watu kwako hupunjika,
Lazima kitakufika, kile kilichoandikwa.

 

 

Yote yamesajiliwa, Allaah Ameshaandika,
kalamu kuinuliwa, wino umeshakauka,
kudura imeshapangwa, hakuna kubadilika,
Lazima kitakufika, kile kilicho andikwa.

 

 

Tangu bado kuzaliwa, vyote vimeandikika,
riziki imegawiwa, na ajali kadhalika,
utajiri ukipewa, usisahau sadaka,
Lazima kitakufika, kile kilicho andikwa.

 

 

Utajiri ukinyimwa, halafu ukasumbuka,
usidhani umetupwa, Kakusahau Rabuka,
mwisho wake utalipwa, ukisubiri hakika,
Lazima kitakufika, kile kilicho andikwa.

 

 

Na mitihani mikubwa, kama inamiminika,
tumshukuru MKUBWA, subira kulazimika,
tuzidi kuomba dua, hapana kulalamika,
Lazima kitakufika, kile kilicho andikwa.

 

 

Imani yako hupimwa, ovyo hapana ropoka,
yote hayo majaliwa, kukupima Anataka,
imani kuzingatiwa, rehema itateremka,
Lazima kitakufika, kile kilicho andikwa.

 

 

Msiba unapokuwa, dhaifu hutetemeka,
kama mwehu anakuwa, imani inamtoka,
anasahau ya kuwa, Allaah hivyo Ameweka,
Lazima kitakufika, kile kilicho andikwa.

 

 

Na makelele kupigwa, maafa yakimfika,
na yote yamekatazwa, Allaah Ataghadhibika,
Apenda  kushukuriwa, Mola wetu Mtukuka,
Lazima kitakufika, kile kilichoandikwa.

 

 

Kuvumilia ni sawa, na imani kuiweka,
hadhulumiwi muumbwa, kwa haki kinatendeka,
hakuna cha kuonewa, imani ya nguvu shika,
Lazima kitakufika, kile kilichoandikwa.

 

 

Usiseme umerogwa, sababu ya kuteseka,
yote hayo yanapingwa, imani kudhoofika,
huo ndio ni ugonjwa, wa shirki usotibika,
Lazima kitakufika, kile kilichoandikwa.

 

 

Kumbuka unavyozikwa, kaburini kukuweka,
watu wote sawasawa, sanda wanawafunika,
na wote wanasaliwa, hakuna kubagulika,
Lazima kitakufika, kile kilichoandikwa.

 

 

Usikubali kushindwa, shetani akakucheka,
utageuka mfungwa, wa shetani ni mateka,
hapo ndio umekumbwa, na imani kutoweka,
Lazima kitakufika, kile kilichoandikwa.

 

 

Hirizi ukivalishwa, shingoni kuipachika,
ujuwe umedanganywa, huwezi kunufaika,
madhambi utabebeshwa, hapo umehadaika,
Lazima kitakufika, kile kilichoandikwa.

 

 

Hapa nafunga baruwa, pengine mmeshachoka,
tunaomba maridhawa, Mola Apate Ridhika,
tunaomba kuepushwa, na madhambi kufutika,
Lazima Kitakufika, Kile Kilichoandikiwa.

 

 

 

 

Share