Mashairi: Kumbuka Mauti

                        

 Kumbuka Mauti

                                   ‘Abdallaah bin Eifan (Rahimahu Allaah)

        

Alhidaaya.com

 

                   

 

 

(1)  Salaam naieneza, haina utangulizi,

       Nimekuja kueleza, ya ukweli si upuzi,

       Nakuomba sikiliza, kuna mengi sikuhizi,

       Tunakumbuka mauti, tunapoona jeneza.

 

 

(2)  Tunapoona jeneza, tunapatwa na majonzi,

       Tunakaa tukiwaza, ametutoka mpenzi,

       Halafu twaomboleza, yakitutoka machozi,

       Tunakumbuka mauti, tunapoona jeneza.

 

 

(3)  Unapelekwa haraka, duniani huna kazi,

       Halafu wanaondoka, yanabaki simulizi,

       Fulani ametutoka, kawa na sisi majuzi,

       Tunakumbuka mauti, tunapoona jeneza.

 

 

(4)  Ndani ya shimo kumbuka, huna hapo mtetezi,

       Majuto yanakufika, na ukiwa na simanzi,

       Ubaki kuhangaika, hakuna cha usingizi,

       Tunakumbuka mauti, tunapoona jeneza.

 

 

(5)  Rasilmali ni sanda, nyeupe haichukizi,

       Kule hupewi kitanda, na nyimbo husikilizi,

       Utaoza utavunda, hakuna cha mkombozi,

       Tunakumbuka mauti, tunapoona jeneza.

 

 

(6)  Tajiri na masikini, hakuna cha ubaguzi,

       Huna hela mfukoni, akiba ya matumizi,

       Mtatafunwa mwilini, mifupa, nyama na ngozi,

       Tunakumbuka mauti, tunapoona jeneza.

 

 

(7)  Unaacha yote mali, dereva na wachukuzi,

       Unakwenda na amali, panda au shuka ngazi,

       Kule yote ni ya kweli, utaona waziwazi,

       Tunakumbuka mauti, tunapoona jeneza.

 

 

(8)  Kumbuka sana kaburi, dini yako kuienzi,

       Kwa hivyo acha kiburi, na tabia ya kishenzi, 

       Kaa na watu vizuri, usianze uchokozi,

       Tunakumbuka mauti, tunapoona jeneza.

 

 

(9)  Shetani yupo na sisi, kaweka yake mizizi,

       Hatuachi tukahisi, anakuja kama mwizi,

       Anachochea maasi, mwisho ni maangamizi,

       Tunakumbuka mauti, tunapoona jeneza.

 

 

       (10)  Wakati unatupita, mbio mwendo wa jahazi,

             Dunia ni ya kupita, sisi kama wakimbizi,

             Beti kumi ninasita, kuendelea siwezi,

             Tunakumbuka mauti, tunapoona jeneza.                

     

      

             

  

Share