Mashairi: Hija Yao Taqabali, Tunakuomba Jalali

 

Hija Yao Taqabali, Tunakuomba Jalali

 

Abdallah Bin Eifan (Rahimahu-Allaah)

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Salaam  kila pahali, ninawauliza hali,

Mashetani makatili, Allaah Watie kufuli,

Mola Utupe akili, tusibaki majahili,

Hija yao Taqabbali, Tunakuomba Jalali.

 

 

Tunakuomba Jalali, hija yao Taqabbali,

Mahujaji kwa halali, wamelipa yao mali,

Tena wametoka mbali, kwa ndege na kwenye meli,

Hija yao Taqabbali, Tunakuomba Jalali.

 

 

Kainua matofali, Baba yake Ismaili,

Kajenga Ka'aba asili, hakuna tena badili,

Ikawa ndio dalili, Qibla kuikabili,

Hija yao Taqabbali, Tunakuomba Jalali.

 

 

Dua zao Zikubali, Wewe ndio Mfadhili,

Na tabu hawakujali, na usiku hawalali,

Mchana ni jua kali, wamebeba miavuli.

Hija yao Taqabbali, Tunakuomba Jalali.

 

 

Mtihani wasifeli, Allaah Ifanye sahali,

Watu wametawakali, wote wameshawasili,

Wamevaa kwenye mwili, nguo nyeupe kamili,

Hija yao Taqabbali, Tunakuomba Jalali.

 

 

Wanaomba kwelikweli, wito wameukubali,

Wapo katika shughuli, ya ibada na kuswali,

Wanakuomba kibali, Peponi wape mahali,

Hija yao Taqabbali, Tunakuomba Jalali.

 

 

Pepo wanastahili, Waweke wao awali,

Na Wewe ndio Kamili, Mfalme kila pahali,

Thawabu kama jabali, Twakuomba Usajili,

Hija yao Taqabbali, Tunakuomba Jalali.

 

 

Wawe chini ya kivuli, Ppeponi wale asali,

Wawe kwenye nzuri hali, na Allaah Awafadhili,

Wawe ndio ni methali, Allaah Wamulike muli,

Hija yao Taqabbali, Tunakuomba Jalali.

 

 

Tunakuomba Qahari, Waepushe na batili,

Waepushe na khatari, Wasikumbwe na ajali,

Hapa nafunga shairi, kwenda mbele ni muhali,

Hija yao Taqabbali, Tunakuomba Jalali.

 

 

 

Share