Amekhasimiana Na Mwenziwe, Je, Swawm Yake Sahihi?

 

SWALI

 

Assalam aleikum ninawaomba mumueleze ndugu yangu wakiislamu ambaye hasemi na mwenziwe wa kiislamu na yeye yuko kwenye hali yakuwa amefunga ramadhani tukufu.nini faida yake?na nini hasara yake?na nini adhabu yake?je swaum yake ni maqbul?

shukran jazila.

 

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Kukhasimiana ndugu wa Kiislamu ni jambo la hatari sana ambalo halipasi kabisa, ikiwa ni katika mwezi wa Ramadhaan au siku za kawaida. Hatari yake ni kwamba 'amali za mja anazozitenda huwa hazipokelewa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) hadi wapatane. Hii ni kutokana na usimulizi ufuatao ambao ni Hadiyth Swahiyh: :

 

 

 عن أبي هريرة رضي الله عنه قال : قال رسول الله صلى الله عليه وسلم : (( تُعرض الأعمال في كل أثنين وخميس فيغفر الله لكل أمريء لايشرك بالله شيئاً، إلا إمرءاً بينه وبين أخيه شحناء فيقول : اتركوا هذين حتى يصطلحا((  رواه مسلم

 

 Imetoka kwa Abu Hurayrah رضي الله عنه kwamba kasema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  (('Amali njema (vitendo vyema) huoneshwa kila Jumatatu na Alkhamiys, kisha Allaah Humghufuria kila mtu asiyemshirikisha kitu Allaah, isipokuwa mtu aliyekuwa baina yake na baina ya ndugu yake uhasama, Husema: Waacheni hawa wawili mpaka wapatane)) [Muslim]

 

 

Tunaona kwamba 'amali huorodheshwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Hazitazami 'amali za waliogombana na juu ya hivyo Hawaghufurii madhambi yao hao wawili. Sasa ikiwa mwezi huu unajulikana kuwa ni mwezi wa Maghfirah na tunategemea kutoka tukiwa tumeghufuriwa madhambi yetu, itakuwaje ndugu hao wawili wasikhofu kukosa kusamehewa madhambi yao? Je hawaoni kwamba huenda   kukaa kwao na njaa na kiu huenda kukawa ni bure ikiwa hawatafuata maamrisho haya?

 

 

Hatari zaidi ni kwamba mwenye kukhasimiana na mwenziwe zaidi ya siku tatu bila ya kupatana naye, pindi yakimfika mauti akiwa katika hali hiyo basi atakosa kuingia Peponi, bali atakuwa ni mtu wa kuingizwa motoni:

 

 

 عن أبي أيوب الأنصاري رضي الله عنه قال : قال النبي صلى الله عليه وسلم : (( لا يَحِلُّ لِمُسْلِمٍ أَنْ يَهْجُرَ أَخَاهُ فَوْقَ ثَلَاثِ لَيَالٍ ، يَلْتَقِيَانِ فَيُعْرِضُ هَذَا وَيُعْرِضُ هَذَا ، وَخَيْرُهُمَا الَّذِي يَبْدَأُ بِالسَّلامِ  .(( رواه البخاري ومسلم و في رواية أبو داود بإسناد على شرط البخاري ومسلم ((فَمَنْ هَجَرَ فَوْقَ ثَلاَثٍ فَمَاتَ دَخَلَ النَارَ ))   

 

Imetoka kwa Abu Ayyuub Al-Answariy رضي الله عنه ambaye alisema: Kasema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم: ((Haimpasi Muislamu amhame ndugu yake kwa zaidi ya siku tatu hata wanapokutana huyu anamgeuzia (uso) huyu na huyu anamgeuzia (uso) huyu. Na aliye mbora wao ni yule anayeanza kutoa salaam)) [Al-Bukhaariy na Muslim.  Na katika Riwayaah ya Abu Daawuud ((Atakayemhama (mwenzake) kwa zaidi ya siku tatu akafariki basi ataingia  motoni))

 

 

Bila ya shaka kila mmoja wetu atakuwa na khofu kubwa ya madhara hayo, hivyo mwenye akili atakimbilia kupatana na mwenziwe ili awe ana hakika na ibada zake kukubaliwa, madhambi yake kusamehewa na kuepukana na moto wa Jahannam. Na yule mwenye kuanza kumkabili mwenziwe kwa ajili ya kupatana atakuwa ni mbora zaidi mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kuliko mwenziwe kama maelezo yalivyo katika usimulizi huo wa juu.

 

Ndugu Waislamu, tuache kiburi, na tumuepuke Ibiliys mwenye kupenda kugombanisha watu na asiyependa watu wapatane. Tutambue kwamba dunia si lolote si chochote kwani ni maisha ya kustarehe kwa muda tu, na Akhera ndio maisha ya raha ya kudumu. Kwa hiyo tusiziendekeze nafsi zetu kuwa ngumu tunapogombana na wenzetu, na tunapopata mafunzo kama haya yanayoonyesha hatari kubwa ya 'amali zetu na kukosa maghfira kutoka kwa Mola Mtukufu.

 

Nawe ndugu yetu uliyetuma hili swali kwa  mapenzi ya kutaka kuwaelemisha ndugu zako waepukane na kukhasimiana, inakupasa ufanye jitihada kubwa kuwapatanisha hao ndugu zetu ili nawe ujipatie fadhila kuu za kupatanisha ndugu waliokhasimiana.

Tafadhali ingia katika viungo vifuatavyo usome makala kuhusu umuhimu wa kusuluhisha waliogombana.

 

 

Fadhila Za Kusuluhisha Waliogombana (Sehemu Ya 1)

 

Fadhila Za Kusuluhisha Waliogombana (Sehemu ya 2)

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share