Hataki Mkewe Apate Mimba Hivyo Anamuingilia Mapajani, Inafaa?

SWALI:

A/ALAYKUM

INSHAALLAH MTAKUWA KATIKA HALI YA UZIMA NA MALIPO MEMA KWA ALLAH AMIN. SWALI LANGU HILI? MIMI NI MKE WA MTU AMBAYE MIMI NA MUME WANGU TUNAPENDANA SANA NA TUMEBAHATIKA KUZAA MTOTO MMOJA, KWA SASA TUNATUMIA KALENDA ILI TUZAE KWA MPANGO TATIZO LINAKUJA HIVI SIKU AMBAZO MUME WANGU ANA HAMU YA KUNIINGILIA KWA TAREHE ILE INAKUWA SI SIKU YA KUNIINGILIA BASI HUWA ANANAMBIA NIGEUKE KIFUDIFUDI NA UUME WAKE HUWEKA KWENYE MAPAJA MPAKA HAMU YAKE INAISHA JE NI HALALI KUFANYA HIVYO? WABILLAH TAUFIQ


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta'ala) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Mtume. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea au kivivu. Pia hiyo ni ibada, na ibada inatakiwa ifanywe kwa namna iliyofundishwa na haifai kugeuza, kuongeza au kupunguza. Hali kadhalika Maswahaba walikuwa wakiandikiana barua na hakuna aliyekuwa akikatisha Salaam, wala kumswalia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wala kumtukuza Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwenye barua zao. Tuige na tufuate nyendo zao tusalimike.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mumeo kumaliza matamanio yake mapajani. Tufahamu kuwa Allaah Aliyetukuka Anafuhamisha kuhusu sifa za Waumini wema ambao watapata ujira mwema Kesho Akhera. Anasema:

"HAKIKA wamefanikiwa Waumini, Ambao ni wanyenyekevu katika Swalah zao, na ambao hujiepusha na mambo ya upuuzi, na ambao wanatoa Zakaah, na ambao wanazilinda tupu zao, isipokuwa kwa wake zao au kwa iliyo wamiliki mikono yao ya kulia. Kwani hao si wenye kulaumiwa. Lakini anayetaka kinyume cha haya, basi hao ndio warukao mipaka. Na ambao wanazitimiza amana zao na ahadi zao, Na ambao Swalah zao wanazihifadhi - Hao ndio warithi, Ambao watairithi Pepo ya Firdausi, wadumu humo" (23: 1 – 11).

Allaah Aliyetukuka katika Aayah zilizo juu ametufahamisha mambo ambayo yatawaingiza Waumini katika Firdaws na wanaoruka mipaka hawamo katika orodha hiyo. Warukao mipaka ni kina nani? Hawa ni wale wenye kufanya amali ya kaumu Luutw, wasaganao (wanawake kufanya tendo la ndoa na wanawake), kutumia mkono na kadhalika. Haya mambo tuliyoyataja yote ni ya haramu kwa Muislamu kufanya.

 

Allaah Aliyetukuka Amejaalia kuwa wanandoa ni kivazi mmoja kwa mwenziwe hata hivyo Hakujaalia watu watumie njia hii. Allaah Aliyetukuka Anasema:

"Wao ni vazi kwenu, na nyinyi ni vazi kwao" (2: 187).

Na pia,

"Wake zenu ni kama konde zenu. Basi ziendeeni konde zenu mpendavyo. Lakini jitangulizieni kheri nafsi zenu, na mcheni Allaah, na jueni kuwa hakika nyinyi mtakutana naye. Na wape bishara njema Waumini" (2: 223).

Hii Aayah inatuamuru tuwaendee wake vyovyote tunavyotaka lakini si popote. Sasa paja si sehemu ya kupanda mbegu kwani kufanya hivyo kutakuwa ni kinyume na matakwa yaliyokusudiwa na mazoea hayo yanaweza kukupeleka pabaya na pia kuna hatari ya kuteleza na ukatumbukia katika maeneo ya nyuma ambayo ni haraam kabisa au hata sehemu ya mbele ambayo kwa wakati huo pia imekatazwa.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa anataka kustarehe na mkewe wakati ana hedhi, alikuwa akimtaka ajifunike shuka au kitambaa kwenye maeneo ya kitovu hadi magotini na kisha akamchezea katika sehemu zilizobaki, hili limethibiti kwa Hadiyth ya mama wa waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) aliposema: “Alipokuwa mmoja wetu katika hedhi na Mtume akawa anataka kuwa naye (kitandani), basi  alikuwa akimuamrisha ajifunike shuka maeneo yake na kisha huwa naye (akimchezea)” (Al-Bukhaariy na Muslim).

Na pia karuhusu kumchezea mke sehemu zilizobaki za mwili lakini akakataza kumuingilia kama Hadiyth inavyoonyesha hapa chini:

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika suala hilo mke anapokuwa katika siku zake, anasema:

“Fanya kila jambo isipokuwa jimai” (Muslim).

Hivyo hapo tunaona kuwa mapaja ni sehemu isiyofaa kuchezea au kuiingilia kwa wakati huo wa hedhi.

Baadhi ya wanachuoni wa sasa wamesema pia hakuna makatazo ya mke kumchezea mume kwa mikono yake hadi mume akamaliza haja yake. Haipendezi tu kutumia mdomo kuweka katika utupu wa mume au wa mke kwani si jambo la muruwa na ni maagizo ya matendo ya makafiri japo hakuna uharamu wa wazi katika hilo.

Hata hivyo, katika masiku mengineyo yasiyo ya hedhi, hakuna makatazo ya wazi ya kumuingilia mke kwenye mapaja, matiti au hata katikati ya makalio yake bila kuingiza utupu ndani ya tundu. Hili wamelieleza wanachuoni mbalimbali kama tunavyoona:

Imaam Ash-Shaafi’iy anasema:  Hakuna tatizo mtu anapotaka kujifurahisha na mkewe kumuingilia katikati ya makalio yake lakini bila kutumbukiza utupu wake kwenye tundu”. [Al-Ummu mj. 8, uk. 257).

Naye Imaam Ibn Qudaamah anasema hayo kwenye kitabu chake cha ‘Al-Mughniy’

Vilevile katika kitabu cha Rawdh atw-Twaalib na Asnaa al-Matwaalib.

Kwa hiyo tunaona hakuna makatazo ya hayo maadam mtu anastarehe na mkewe. Mtu anaweza kustarehe kwa njia nyingi na mitindo mbalimbali bila kuvunja tu sheria ya kumuingilia mkewe nyuma.

Inafaa uzungumze na mumeo kuhusu hili ili ajichunge na kujiepusha na maeneo ya katikati ya kitovu na magoti wakati uko kwenye siku zako. Na hayo ni masiku machache tu mtu ajitahidi kujizuia ili asije kuingia kwenye makosa na madhambi kwa kufanya yasiyotakikana.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share