Zingatio: Hawana Kheri Na Sisi

 

Zingatio: Hawana Kheri Na Sisi

 

Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

Hakika hakuna kiumbe kilichofika duniani kuwatakia wenziwe khayr isipokuwa kipenzi chetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hakutaka mali wala chakula kutoka kwa watu wake. Alielewa lengo lakena hakuingia kwenye ubadhirifu wala ufisadi.

 

Wakafuatia Waongofu wanne ambao walielewa maana ya utawala na wakajilazimisha kuongoza kwa haki na uadilifu. Taariykh zao zimejaa simulizi za kuhuzunisha na za kufurahisha. Walibeba magunia ya vyakula juu ya migongo yao wenyewe kuwapelekea wananchi wao. Viongozi ambao waliueneza Uislamu kutoka Mashariki hadi Magharibi. Kuenea huku haikuwa ni sababu kwao kuwadhulumu watu.

 

Lengo la Uislamu ni kuimarisha misingi ya haki na uadilifu. Aliye nacho amsaidie asiye nacho, mkubwa amsalimie mdogo, anayetiwa hatiani atumikie adhabu inayostahiki hata akiwa ni Rais wa nchi. Hizo ndizo cheche za moto alizotuachia Nabiy wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na Khulafaur-Raashiduun.

 

Hayo sio yanayotendeka juu ya utawala wa kimabavu wa sasa. Sio ukomunisti wala ubepari ulioleta utawala unaozalisha utulivu wa nafsi. Dunia ilivurumishiwa mizinga mwanzo wa karne ya 20 na yakarudi tena kati kati ya karne hiyo hiyo. Mamilioni ya viumbe walipoteza maisha yao na familia zikasambaratika kama kigae kilichovunjika.

 

Baada ya hapo, zikaja enzi za vita baridi ambavyo hakika viliugawa ulimwengu matabaka makuu mawili. Wakahasimiana wakashindwa kuishi kwa salama na amani. Uchumi wa Magharibi hausafirishwi Mashariki wala misaada ya Mashariki haiendi Magharibi.

 

Pande moja likaanguka na hivyo kuliachia pande la pili kusimama kwa kebehi, mabavu na ulimbwembwe wa kila aina. Ulimwengu ukaendelea kusikia misamiati ya 'demokrasia', 'haki za wanaadamu', 'haki za wanawake', 'bandari huru' na mengineyo. Hayo yote yalikuwa na azma moja tu; kuutawala ulimwengu wote ndani ya mkono mmoja.

 

Ulimwengu wa leo umejaa zahma mtindo mmoja. Sio nchi za wazungu, wachina, waarabu wala waafrika wenye kuwatakia wema wananchi wao. Hizo njia zinazotumika kuwapata viongozi wa nchi wala hazitambuliki ndani ya Uislamu. Propaganda zilizojaa uongo na ulaghai ndizo zinazomsafishia njia kiongozi kushika usukani. Sasa kama yeye ameingia kwa njia hizi, wananchi wategemee nini kutoka kwao? Au kwa sababu ana sura nzuri, mali na pengine jina la Kiislamu? Mbwa atabakia mbwa hata ukimbadili jina.

 

Tuelewe ya kwamba kiongozi anayewatakia wema mataifa ya wenziwe atawajengea kiwanda chenye kuzalisha kisawasawa. Hawezi kutoa misaada ya kuua mbu majumbani wakati vyanzo vya mazalio ya mbu vikinawiri maridadi kabisa. Haiwezekani atoe milioni za michango ya UKIMWI ilhali chanzo kikuu cha maradhi haya hayatakiwi kuzungumzwa wala kupigwa vita wazi wazi. Wala haingii akilini kutoa mikopo yenye riba ya juu huku akidai kwamba ni msaada. Ni mchezo wa kuzuga macho ya wananchi tu kuona kana kwamba ni mwenye kuyatakia kheri mataifa mengine.

 

Waswahili tuna msemo unasema 'Kikulacho kinguoni mwako.' Katu mataifa masikini yaelewe kwamba mwenye kumfuga simba ipo siku atamkwaruza au hata kumrarua rarua. Hata kama utaanza kumfuga angali yu mdogo kabisa.

 

Tujifunze kutoka kwa Nabiy Sulaymaan (‘Alayhi Swalaatu was-salaam) ambaye alipatiwa nguvu za kuongoza hajapatapo kutokezea kiongozi mfano wake. Aliutumia upepo, wanyama, majini, ndege na vyenginevyo kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Akatumia uwezo huu kumuelewesha ukweli wa mambo Malkia wa Sheba Bibi Balqiys.

 

Itambulike kwamba utawala wa kimabavu ni ule unaofanya jamii kukosa haki ya kutoa sauti zao na mawazo yao yakakubalika na viongozi husika. Mfano, Firauni aliwafanya watu wake kuwa ni wajinga na hakutuhumiwa hata chembe ya ovu ingawa alikuwa muovu wa waovu. Qur-aan inasema kuhusu namna Firauni alivyowafanya watu wake:

 

 فَلَمَّا كَشَفْنَا عَنْهُمُ الْعَذَابَ إِذَا هُمْ يَنكُثُونَ﴿٥٠﴾

Lakini Tulipowaondoshea adhabu tahamaki wao wanavunja ahadi. [Az-Zukhruuf: 50]

 

Basi na tuelewe ya kwamba sio dunia tu iliyojaa hila na mitego. Bali hata viongozi tunaowaamini pia wanafanya kila njia kuturubuni nafsi zetu. Turudi kwenye mafundisho sahihi ya Qur-aan na Sunnah ili tupate salama mbele ya Siku ya Hesabu.

Share