Nabiy Muwsaa (عَلَيْهِ السَّلام) Alizungumza Vipi Na Allaah?

 

 

 Nabiy Muwsaa (عَلَيْهِ السَّلام) Alizungumza Vipi Na Allaah?

 

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Asalam alaykum

 

Swali?  Maneno ya Allaah hayana sauti wala helufi, sasa ni kwa vipi Nabii wa Allaah ambae ni Musa Juu yake amani alikuwa akizungumza na Allaah?

 

NB: Haya maswali ninayo kuulizeni ni kwamba hata mimi nimeulizwa maswali haya ndio na mimi ninakuulizeni.

 

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Msingi wetu mkubwa wa kuelewa na kufahamu mambo yetu yote katika nyanja zote za kimaisha ni Qur-aan na Sunnah za Nabiy wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kwa hiyo, tungependa kueleza mambo fulani kabla ya kuja katika swali lenyewe ambalo nimeulizwa na ndugu yetu.

 

Muislamu anaamini yale aliyonayo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) miongoni mwa Majina Yake Mazuri na mema na Sifa Zake za juu wala Muislamu hamshirikishi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na mwingine asiyekuwa Yeye katika Majina na Sifa hizo. Muislamu hayafanyii taawiyl (tafsiri) Majina hayo na Sifa hizo, wala hafananishi Sifa za Allaah na sifa za viumbe  Vyake kwa kusema vipi Allaah ana uhai na vipi Allaah Anazungumza, Anaona na Kusikia, hayo kufanywa na Muislamu ni muhali na hayatakiwi.

 

 

Muislamu anathibitisha kwa Allaah yale Aliyojithibitishia Mwenyewe na Akayathibitisha Nabiy Wake miongoni mwa Majina na Sifa Zake. Muislamu anamkatalia Allaah Sifa Alizozikataa Mwenyewe na akazikataa Rasuli Wake, za kuepukana na kila aibu na upungufu kwa ujumla na kwa mchanganuo. 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amejisifu Mwenyewe kwamba Yeye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona, Mjuzi, Mwenye hikhma, Mwenye nguvu, Mpole, Mwenye kusamehe, Anzungumza, Ana mikono, Ana uso na kadhalika. Yeye Amezungumza na Nabiy Muwsa (‘Alayhis Salaam) na Amelingana sawasawa juu ya ‘Arsh Yake. Sifa ya kusikia na kuzungumza ni Yake kwani Amesema kuhusu hilo:

  وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ ﴿١١﴾

 

Naye Ndiye Mwenye kusikia yote, Mwenye kuona yote. [Ash-Shuwraa: 11]

 

na

 

تِلْكَ الرُّسُلُ فَضَّلْنَا بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ ۘ مِّنْهُم مَّن كَلَّمَ اللَّـهُ ۖ وَرَفَعَ بَعْضَهُمْ دَرَجَاتٍ ۚ  

Hao ni Rusuli, Tumewafadhilisha baadhi yao juu ya baadhi. Miongoni mwao kuna aliyesemeshwa na Allaah, na Akawapandisha baadhi yao vyeo. [Al-Baqarah: 253]

 

 

Hayo wamekiri Wanazuoni wema wa kale na wa sasa kuanzia kwa Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) juu ya Sifa za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala) bila kuzipa tafsiri potofu, au kuzikanusha au kuzitoa katika dhahiri yake. Kwani haikuthibiti kuna Swahaba yeyote aliyeipa tafsiri potofu Sifa miongoni mwa Sifa za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) au kuipindisha au kuipinga au akasema kuwa dhahiri yake sio iliyokusudiwa. Bali walikuwa wanaamini maana inayofahamika kutoka katika Sifa hiyo kama ilivyo, na wanaichukulia dhahiri yake, hali wanaelewa kuwa Sifa za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) sio sifa za viumbe Wake.

 

 

Imaam Maalik aliulizwa kuhusu kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ ﴿٥﴾

Mwingi wa rahmah Yuko juu (Istawaa) ya ‘Arshi. [Twaaha  (20: 5)]. 

 

Je, ni vipi Istawaa? Basi Imaam Maalik hakuwahi kughadhibika kutokana na kitu chochote kile kama alivyoghadhibika kutokana na swali la mtu huyo, kisha [Imaam Maalik] akatazama chini na huku akikwaruzakwaruza kwa kijiti kilichokuwa kwenye mkono wake mpaka akarowa jasho, kisha akanyanyua kichwa chake na kukirembea kile kijiti kisha akasema: ‘Vipi’ ni ghayr ma’quwl (hakutambuliki), na Al-Istiwaa ghayr maj-huwl (si jambo lisilojulikana), na kuamini hilo ni waajib (lazima), na kuuliza (au kuhoji hilo) ni bid’ah (uzushi); na nina khofu kuwa wewe ni mzushi! Akaamrisha mtu huyo atolewe, basi akatolewa. [Imesimuliwa kwenye Al-Hilyah (6/325-326) na pia imesimuliwa na Abuu ‘Uthmaan Asw-Swaabuniy katika ‘Aqiydatu As-Salaf Asw-haab Al-Hadiyth uk. (17-18), kutoka kwa Ja’far bin ‘Abdillaah]

 

 

Imaam Ash-Shaafi‘iy alisema: “Nimemuamini Allaah na kilichokuja kutoka kwa Allaah kama Alivyokusudia Allaah na nimemuamini Rasuli wa Allaah, na kila kilichokuja kutoka kwa Rasuli wa Allaah, kama alivyokusudia Rasuli wa Allaah”.

 

 

Imaam Ahmad alikuwa akisema kutokana na kauli ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) isemayo kuwa: “Hakika Allaah Anateremka kwenye mbingu ya dunia, na kwamba Allaah Anafurahi, Anacheka, Anaridhia, Anaona karaha na Anapenda, alikuwa akisema: ‘Tunayaamini, na tunayakubali, si kwa namna wala kwa maana fulani’. Anakusudia kuwa sisi tunaamini kuwa Allaah Anaona, naye Yuko juu ya ‘Arsh Yake tofauti na viumbe Vyake. Lakini hatuelewi namna ya kushuka Kwake, wala kuona Kwake, wala kulingana Kwake, wala maana hasa ya hayo. Bali maana yake hiyo tunaiacha katika ilimu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa Aliyoyasema na Aliyomletea Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hatumpingi Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wala hatumpi sifa zaidi ya zile Alizojisifia Mwenyewe na Alizosifiwa na Rasuli Wake bila ya mpaka wala kikomo, nasi tunaelewa kuwa hakuna kilicho mfano Wake Naye ni Mwenye kusikia na Mwenye kuona”.

 

 

Kuhusu ibara yako: “Maneno ya Allaah hayana sauti wala herufi” hayana uthibitisho wowote bali Qur-aan ipo wazi kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alizungumza na Muwsaa (‘Alayhis Salaam) kama tutakavyoona hapa chini. Neno hili ambalo limetumika la kuzungumza limetumika sehemu nyingi katika Qur-aan. Miongoni mwayo ni mnyama ambaye atazungumza na watu kabla ya Qiyaamah:

 

 

وَإِذَا وَقَعَ الْقَوْلُ عَلَيْهِمْ أَخْرَجْنَا لَهُمْ دَابَّةً مِّنَ الْأَرْضِ تُكَلِّمُهُمْ أَنَّ النَّاسَ كَانُوا بِآيَاتِنَا لَا يُوقِنُونَ ﴿٨٢﴾

Na itakapotimizwa kauli dhidi yao, Tutawatolea mnyama atembeaye katika ardhi atakayewasemezesha kwa sababu watu walikuwa hawana yakini na Aayaat (na ishara) Zetu. [an-Naml: 82]

 

 

 

Na kuhusu Siku ya Qiyaamah, Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala) Anatuelezea kuwa kila kitu kitazungumza:

 

الْيَوْمَ نَخْتِمُ عَلَىٰ أَفْوَاهِهِمْ وَتُكَلِّمُنَا أَيْدِيهِمْ وَتَشْهَدُ أَرْجُلُهُم بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ ﴿٦٥﴾

Leo Tunatia vizibo juu ya vinywa vyao, na itatusemesha mikono yao, na itashuhudia miguu yao kwa yale waliyokuwa wakiyachuma.  [Yaasiyn: 65]

 

 

Ama kuhusu Maryam, Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Anatuelezea kuwa Malaika alimwambia aseme yafuatayo pindi anapokuja kwa watu wake:

 

 

فَكُلِي وَاشْرَبِي وَقَرِّي عَيْنًا ۖ فَإِمَّا تَرَيِنَّ مِنَ الْبَشَرِ أَحَدًا فَقُولِي إِنِّي نَذَرْتُ لِلرَّحْمَـٰنِ صَوْمًا فَلَنْ أُكَلِّمَ الْيَوْمَ إِنسِيًّا ﴿٢٦﴾

  Basi kula na kunywa na litue jicho lako. Na utakapokutana na mtu yeyote basi sema: Hakika mimi nimeweka nadhiri ya swawm kwa Ar-Rahmaan hivyo leo sitomsemesha mtu yeyote. [Maryam: 26]

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) naye Anatueleza kuwa Yeye Amezungumza na baadhi ya Rusuli Wake:

 

تِلْكَ الرُّسُلُ فَضَّلْنَا بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ ۘ مِّنْهُم مَّن كَلَّمَ اللَّـهُ    

Hao ni Rusuli, Tumewafadhilisha baadhi yao juu ya baadhi. Miongoni mwao kuna aliyesemeshwa na Allaah. [Al-Baqarah: 253]

 

Na tena:

 

وَرُسُلًا قَدْ قَصَصْنَاهُمْ عَلَيْكَ مِن قَبْلُ وَرُسُلًا لَّمْ نَقْصُصْهُمْ عَلَيْكَ ۚ وَكَلَّمَ اللَّـهُ مُوسَىٰ تَكْلِيمًا ﴿١٦٤﴾

Na Rusuli Tuliokwishakusimulia kabla; na Rusuli (wengine) Hatukukusimulia. Na bila shaka Allaah Alimsemesha Muwsaa maneno moja kwa moja [An-Nisaa: 164]

 

 

Na Amesema:

 

 

وَلَمَّا جَاءَ مُوسَىٰ لِمِيقَاتِنَا وَكَلَّمَهُ رَبُّهُ قَالَ رَبِّ أَرِنِي أَنظُرْ إِلَيْكَ ۚ قَالَ لَن تَرَانِي وَلَـٰكِنِ انظُرْ إِلَى الْجَبَلِ فَإِنِ اسْتَقَرَّ مَكَانَهُ فَسَوْفَ تَرَانِي ۚ  

  Na alipokuja Muwsaa katika muda na pahala pa miadi Yetu, na Rabb wake Akamsemesha, akasema Rabb wangu! Nionyeshe ili nikutazame. (Allaah) Akasema: Hutoniona! Lakini tazama mlima. Ukitulia mahali pake, basi utaniona..  [Al-A'raaf: 143]

 

 

Qur-aan pia inatuelezea mazungumzo baina ya Allaah na Nabiy Muwsaa (‘Alayhis Salaam):

 

 

فَلَمَّا أَتَاهَا نُودِيَ يَا مُوسَىٰ ﴿١١﴾ إِنِّي أَنَا رَبُّكَ فَاخْلَعْ نَعْلَيْكَ ۖ إِنَّكَ بِالْوَادِ الْمُقَدَّسِ طُوًى ﴿١٢﴾ وَأَنَا اخْتَرْتُكَ فَاسْتَمِعْ لِمَا يُوحَىٰ ﴿١٣﴾ إِنَّنِي أَنَا اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدْنِي وَأَقِمِ الصَّلَاةَ لِذِكْرِي ﴿١٤﴾

 

Basi alipoufikia, aliitwa: Ee Muwsaa! Hakika Mimi ni Rabb wako; basi vua viatu vyako, kwani wewe hakika uko katika bonde takatifu la Twuwaa. Nami nimekuchagua; basi sikiliza kwa makini yanayofunuliwa Wahy (kwako). Hakika mimi ni Allaah hapana mwabudiwa wa haki ila Mimi; basi niabudu, na simamisha Swalaah kwa ajili ya kunidhukuru. [Twaahaa: 11 na kuendelea]

 

 

Haya ni mazungumzo marefu baina ya Allaah na Nabiy Muwsaa. Hapana shaka kwa yeyote yule kuwa mazungumzo yanakuwa ni sauti ambapo mmoja anasema na mwengine anasikia.

 

 

Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipokwenda katika safari yake ya Israa wal Mi’raaj katika sehemu ya usiku alikuwa pia ni mwenye kuzungumza na Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) na kupokea maagizo ya Swalaah za faradhi ambazo tunazitekeleza sasa. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Anazungumza na Rusuli Wake na Manabii kwa njia kadhaa kama Alivyotuelezea hilo katika Qur-aan Tukufu. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَمَا كَانَ لِبَشَرٍ أَن يُكَلِّمَهُ اللَّـهُ إِلَّا وَحْيًا أَوْ مِن وَرَاءِ حِجَابٍ أَوْ يُرْسِلَ رَسُولًا فَيُوحِيَ بِإِذْنِهِ مَا يَشَاءُ ۚ إِنَّهُ عَلِيٌّ حَكِيمٌ﴿٥١﴾

Na wala haikuwa kwa mtu yeyote kwamba Allaah Amsemeze isipokuwa kwa Wahy au kutoka nyuma ya kizuizi, au Hutuma Mjumbe, kisha Anamfunulia Wahy Ayatakayo kwa idhini Yake; hakika Yeye ni Mwenye ‘Uluwa, Ametukuka,  Mwenye hikmah wa yote. [Ash-Shuwraa: 51]

 

  

Ibara kwa nyuma ya kizuizi ina maana kusikilizishwa sauti inatoka kwa Allaah pasina kumuona Allaah.

 

Kitu ambacho hatujui wala hatuwezi kuleta taawili (kugeuza maana yake) au kufananisha ni sauti hii inakuwa vipi kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Anasema:

 

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ﴿١١﴾

Hakuna chochote kinachofanana Naye, Naye Ndiye Mwenye kusikia yote, Mwenye kuona yote. [Ash-Shuwraa: 11]

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share