Mwanamke Mchawi Anatekeleza Sana Ibada Lakini Anafanya Uchawi Wa Kuua Watu, Vipi Ibada Zake?

SWALI:

 

Kuna mwanamke mmoja hapa Oman ameshika dini sana suna zote anafunga,salaa zote anasali and mara kwa mara anafungu MIEZI MIWILI MFULULIZO (SIKU)60 TAWBAT NASUHA "SHAHAREEN MUTATABIEN" Lakini ni mchawi mkubwa sana hata watu wengi wamemshika uchawi.

 

Siku moja tulimuuliza mtoto wake wa kiume ambaye ameshika dini sana" nini jazaa ya mtu mchawi anatoa watu na anaweka watu vitandani ikiwa yeye ni mcha MUNGU bila ya kumtaja mama yake, Jibu LAKE KUWA KAMA MTU CHAWI anafanya ibada zote zinazotakiwa na anakwenda hajj, anafunga tawbat nasuha basi MWENYEZI MUNGU ANAMFUTIA MADHAMBI YAE YOTE ALIYOYAFANYA. Je ni kweli maana nasikia mtu mtu aliyemuua mwenzake hana msamah mbele ya "ALLAH"

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kushika dini kwa mtu kunajulikana na kueleweka kutokana na kushikamana huyo muhusika na kila alilokuwa ameshikamana nalo au amefundisha na kulishauri Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na sio kushikanama na matamanio ya nafsi yake; Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ndiye tunayeweza kusema pekee ameshika dini sana na juu ya kushika kwake dini yeye (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anamjua Allaah na kumcha kuliko sisi sote na hata hivyo kama ilivyothibiti hakuwa kufunga miezi miwili mfululizo. Qur-aan imewataka kufunga miezi miwili watu kwa makosa maalumu na sio kujifungia tu, wenye kufunga miezi miwili kwa mfululizo huwa ima ameua Muislamu kwa bahati mbaya (si kwa makusudi) kama inavyosema Qur-aan:

 

"Na haiwi Muumini kumuua Muumini ila kwa kukosea. Na mwenye kumuua Muumini kwa kukosea basi amkomboe mtumwa aliye Muumini, na atoe diya kuwapa jamaa za maiti, isipokuwa waache wenyewe kuwa ni Sadaqa. Na akiwa ni jamaa wa maadui zenu, hali yeye ni Muumini, basi ni kumkomboa mtumwa aliye Muumini. Na akiwa ni miongoni wa watu ambao pana ahadi baina yenu na wao basi wapewe diya watu wake na akombolewe mtumwa Muumini. Na asiyepata, basi afunge miezi miwili mfululizo, kuwa ni toba kwa Allaah. Na Allaah ni Mjuzi na Mwenye hikima" An-Nisaa: 92

 

Au amemuingilia mkewe mchana wa Ramadhaan, au amejitenga na mkewe kwa kufanya dhwihaar.

 

Kusema kuwa ameshikamana na dini na halafu ukasema kuwa Lakini ni mchawi mkubwa sana ni mambo mawili yenye kwenda upande mmoja bila ya kuweza kukutana au kushikana mpaka mwisho wa huu ulimwengu; kwani uchawi ni moja katika mambo yenye kupingana na kwenda kunyume na itikadi ya Kiislamu; na ni jambo lenye kuuvunja Uislamu wa mtu na ni katika madhambi makubwa 'Al-Kabaair' na ni miongoni mwa mambo saba yenye kuhilikisha 'Muwbiqaat' kwani mchawi ni lazima awe amekufuru kama inavyothibitisha Qur-aan:

 

"… Bali mashetani ndio waliokufuru, wakiwafundisha watu uchawi, na yaliyoteremshwa kwa Malaika wawili, Haaruta na Maaruta katika Baabil. Wala hao hawakumfundisha yeyote mpaka wamwambie: Hakika sisi ni mtihani; basi usikufuru" Al-Baqarah: 102.  

 

Ndugu yetu huyo, inapasa afahamishwe kuwa uchawi ni katika ‘amali ya Shaytwaan na ni haraam kwani inamvua Uislamu wake. Uchawi haupatikani isipokuwa kwa kupitia mambo yenye ushirikina na kujidai kujua mambo ya ghayb na yote yanakwenda kinyume na Uislamu na mafundisho ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Mpeni nasaha arudi kwa mola wake na atubie kwani, mchawi pamoja ya kuwa ni mshirikina, bado anaweza kutubia na tawbah yake ni kuacha uchawi mara moja na kujuta na kurudi kwa Mola wake na kutorejera tena mpaka ‘amali za uchawi na kila lenye kufungamana na uchawi mpaka akutane na Mola wake, na huenda tawbah yake ikakubaliwa akiwa mkweli.

 

Pia nasaha zetu kwako na kwa kila Muislamu tuwe tunashikamana na mafundisho ya dini na miongoni mwa mafundisho ni kuwa tusiwe mafasiki kwa kuzua jambo bila ya uhakika. Wala tusiwe ni wenye kudadisi mambo kama haya au kuwasingizia watu au kuwasema watu huenda tukawa tunaingia katika moja kati ya Aayah mbili za Al-Hujuraat; Qur-aan inasema:

 

"Enyi mlioamini! Akikujieni mpotovu na khabari yoyote, ichunguzeni, msije mkawasibu watu kwa kutojua, na mkawa tena wenye kujuta kwa mliyoyatenda." Al-Hujuraat: 6,

au,

"Enyi mlioamini! Jiepusheni na dhana nyingi, kwani baadhi ya dhana ni dhambi. Wala msipelelezane, wala msisengenyane nyinyi kwa nyinyi. Je! Yupo katika nyinyi anayependa kuila nyama ya nduguye aliyekufa? Mnalichukia hilo! Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kupokea toba, Mwenye kurehemu" Al-Hujuraat: 12.

 

Ama kuhusu maelezo yako kuwa mtu aliyemuua mwenzake hana msamaha mbele ya Allaah haya ni katika habari ambazo si sahihi, na kama ameua kama unavyodai basi ni katika madhambi makubwa 'Al-Kabaair'  na kila muuaji ana hukumu yake kulingana na namna ya mauaji yake na hakuna kosa katika Uislam lisilokuwa na tawbah.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share