Kuombewa Du'aa Na Mkristo Ili Apone

Kuombewa Du'aa Na Mkristo Ili Apone

  

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Assalam alaikum warahmatullah wabarakatu.

 

Bismmillahi Rahmani Rahiim

 

Suali langu ni kwamba mimi watoto wangu wanaumwa (wanakohoa sana) namuomba Allaah siku zote awape tahfifu, vile vile nishakwenda hospitali sana lakini matabibu wameshindwa kugundua ni tatizo gani na wamenishauri niwaangalie tu mpaka wakikuwa watapona lakini watoto hao wanateseka sana. Hivi karibuni nilikuwa nazungumza na mwenzangu asijekuwa muislam kuhusu tatizo hilo nae amenishauri kuwa aje kuniombea kwa jina la yesu kwani toka miaka yote watu wanaponywa na jina la yesu na si vyenginevyo, na akaniahidi kama akimaliza maombi anaamini kabisa kwamba watoto wangu tatizo hili litaondokaa kabisa na wala halitawarudia tena.

 

Utatanishi unaonikuta je nikubali aje awaombee? na je watoto wakipona si itakuwa Allaah anaijaribu imani yangu na huyo mwenzangu ndio atapata njia nyepesi ya kujifaharisha mbele yetu waislam kuwa jina la yesu limetuponya na kufanya hivo si shirki?

wabillahi taufik. shukran.

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Swali lako hilo muhimu kuhusu mas-ala hayo ya kuombewa na mkristo. Mwanzo inatakiwa tuelewe kuwa maombi yanapitia kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Kuomba kwa asiyekuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni shirki katika Uislamu. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameliita jambo hilo kuwa ni dhulma kubwa sana Anaposema:

 

إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ ﴿١٣﴾

Hakika shirki ni dhulma kubwa mno. [Luqmaan: 13]

 

Tafadhali bonyeza kiungo kifuatacho upate mafunzo na faida kuhusu maudhui muhimu mno hiyo:

 

Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!- إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ

 

Shirki pia ni dhambi ambalo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Hamghufurii kabisa mwenye kumshirikisha kama Anavyosema:

 

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدِ افْتَرَىٰ إِثْمًا عَظِيمًا ﴿٤٨﴾

Hakika Allaah Haghufurii kushirikishwa; lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae. Na yeyote atakayemshirikisha Allaah basi kwa yakini amezua dhambi kuu. [An-Nisaa: 48]

 

Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا بَعِيدًا﴿١١٦﴾

Hakika Allaah Haghufurii kushirikishwa; lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae. Na yeyote atakayemshirikisha Allaah basi kwa yakini amepotoka upotofu wa mbali.  [An-Nisaa: 116]

 

Tujue kuwa uzima, siha na ugonjwa yote ni mitihani kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kututazama tutabaki vipi katika Iymaan yetu. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

الَّذِي خَلَقَ الْمَوْتَ وَالْحَيَاةَ لِيَبْلُوَكُمْ أَيُّكُمْ أَحْسَنُ عَمَلًا ۚ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْغَفُورُ﴿٢﴾

Ambaye Ameumba mauti na uhai ili Akujaribuni ni nani kati yenu mwenye ‘amali nzuri zaidi. Naye ni Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwingi wa kughufuria. [Al-Mulk: 2]

 

Na hata ukiwa na ugonjwa ambao umewashinda madaktari walio mabingwa katika fani hiyo hairuhusiwi kwani inakuingiza katika shirki ambayo ni dhambi kubwa.

 

Kuwa umemuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa muda haitoshi, kwani hufai kufa moyo katika hilo wala kuona kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) hajakujibu. Huo ni utovu wa Iymaan kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwani Yeye mwenyewe Ametuahidi kuwa:

 

وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ ۚ إِنَّ الَّذِينَ يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِي سَيَدْخُلُونَ جَهَنَّمَ دَاخِرِينَ﴿٦٠﴾

Na Rabb wenu Amesema: “Niombeni, Nitakuitikieni. Hakika wale wanaotakabari katika kuniabudu wataingika Jahanam wadhalilike. [Ghaafir: 60]

 

Bila haka! Allaah Atakujibu kwa njia itakayowaondolea watoto wako matatizo na maradhi hayo.

 

Hakika inajulikana kuwa hao makasisi hawaponyeshi chochote bali wanatumia udanganyifu katika hilo.

 

Jambo linarohusika katika  ni Ruqya inayokubalika katika Shariy’ah ambayo maelezo na mafunzo yake bayana yanapatikana katika viungo vifuatavyo:

  

Ruqyah: Kinga Na Tiba Katika Shariy'ah

 

Du’aa Za Ruqyah (Kinga) Faida Na Sharh Zake

 

Tunakuombea kila la kheri na pia tuko nawe katika du’aa ili watoto wetu wawe ni wenye kupata shifaa kwa Idhini ya Allaah ('Azza wa Jalla).

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share