Mashairi: Twamshukuru Manani, Wamehiji Kwa Salama

Twamshukuru Manani, Wamehiji Kwa Salama

Abdallah Bin Eifan (Rahimahu-Allaah)

www.alhidaaya.com

Salaam nyingi salaamu, natuma mtandaoni,

Kwa wote Waislamu, tajiri na masikini,

Sasa nashika kalamu, naanza toa maoni,

Twamshukuru Manani, Wamehiji kwa salaama.

Hija kweli imekwisha, salaama-u-salimini,

Ibada haijakwisha, iwazidishe imani,

Wazingatie maisha, mpaka kwenda kaburini,

Twamshukuru Manani, Wamehiji kwa salaama.

Wakisharudi safari, wakirejea nyumbani,

Wawe mfano mzuri, kwa ndugu na majirani,

Wasiache kuhubiri, apigwe vita shetani,

Twamshukuru Manani, Wamehiji kwa salaama.

Kuhiji ni majaliwa, Akijalia Manani,

Watu wengi wanalia, kuhiji wanatamani,

Waombe na kutulia, Wamuombe Rahmani,

Twamshukuru Manani, Wamehiji kwa salaama.

Wale waliobakia, in sha Allaah waje mwakani,

Allaah Atawajalia, na wao wawe kundini,

Kwa madua na kwa nia, watajibiwa mwishoni,

Twamshukuru Manani, Wamehiji kwa salaama.

Waloweza walichinja, na damu kumwaga chini,

Allah Awape daraja, katika yao mizani,

Waloshindwa sio hoja, Allaah Mwingi wa hisani,

Twamshukuru Manani, Wamehiji kwa salaama.

Sikukuu tumekula, kwa raha na kwa amani,

Tunamshukuru Mola, kwa neema zote mwilini,

Tukiamka tukilala, twazidisha shukurani,

Twamshukuru Manani, Wamehiji kwa salaama.

Na imani za msingi, zienee kila makani,

Beti nane sio nyingi, nawaomba samahani,

Sababu wageni wengi, waningoja barazani,

Twamshukuru Manani, Wamehiji kwa salaama.

Share