Nimefanya Shirki, Je, Nitasamehewa?

SWALI:

Assalaam alaykum warahmatullah wabarakatuh Shukran kwa kutufahamisha tusiyoyajua katika dini Katika kusafiri kwangu kuelekea mwanza kwa ajili ya FIELD STUDY nilipitia kwa baba wa rafiki yangu ambaye ndo kama mwenyeji wangu YULE BABA AKACHUKUA UNGA UNGA MWEUSI AKANIPAKA MKONONI HUKU AKINISUGUA SUGUA nkamuuliza ni nn ye akasema ni kinga ya wachawi kwa sababu huko ninakoenda kuna wachawi Sana, nkamwambia kuwa MIMI ALLAH ANANITOSHA, akasema sawa lakini kinga muhimu, Ki ukweli nilichukia lakini nlishindwa kutoa mkono wangu. Swali Je, NIMEFANYA SHIRKI...? Na kama NDIO, je NITASAMEHEWA...? kwa mujibu wa Surat An-Nisaa Aya ya 48 ALLAH anasema

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدِ افْتَرَىٰ إِثْمًا عَظِيمًا﴿٤٨﴾

Hakika Allaah Haghufuri kushirikishwa; lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae.  Na yeyote atakayemshirikisha Allaah basi kwa yakini amebuni dhambi kuu. [An-Nisaa: 48]

 

JE,  TOBA  YANGU  KATIKA  SHIRKI  HIYO  SINTOSAMEHEWA....?

BARAKALLAH FIYKUM

 


 

JIBU:

 

Himdi zote Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalaah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kwa hakika umeshamshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) japo kama hukutaka, kwa sababu hapo umemtii na kumuogopa, na kumuonea hayaa kiumbe badala ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Haikupasa kabisa kumwachia akufanyie shirki yoyote. Lakini madamu umetambua kuwa kufanya hivyo ni dhambi, ukarudi kwa Rabb Wako ukamuomba maghfirah basi hakika Yeye Ni Mwingi wa kughufuria na Mpokeaji tawbah za waja Wake.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدِ افْتَرَىٰ إِثْمًا عَظِيمًا﴿٤٨﴾

Hakika Allaah Haghufuri kushirikishwa; lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae. Na yeyote atakayemshirikisha Allaah basi kwa yakini amebuni dhambi kuu. [An-Nisaa: 48]

 

Kadhaalika Anaeleza vilevile (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا بَعِيدًا ﴿١١٦﴾

Hakika Allaah Haghufurii kushirikishwa; lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae.  Na yeyote atakayemshirikisha Allaah basi kwa yakini amepotoka upotofu wa mbali. [An-Nisaa: 116]

 

Imekusudiwa kuwa hakika kitendo hicho anapofanya mtu, hatopata maghfirah kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  pindi mtu akimshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kisha asitubie. Au asitubie mpaka kufikia karibu na kufariki ndio atake kutubia, hapo basi Allaah Hatomghufuria na atakuwa ni mtu wa motoni. Lakini pindi mtu akatubia mapema na akatekeleza masharti ya tawbah ambayo ni :

  1. Kuomba maghfirah  
  2. Kuacha  hayo maasi
  3. Kuweka niyyah (azma) kuwa hatorudia tena
  4. Kama kaidhulumu haki ya mtu basi ni kuirudisha hiyo haki.

Basi hapo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atakughufuria madhambi yako In Shaa Allaah. Na dalili ni kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kuwa Amewataka Manaswara warudie kutubia Kwake kutokana na shirki ya kumshirikisha Allaah kwa kumfanya Nabiy ‘Iysaa ('Alayhis-Salaam) kuwa ni Allaah.

لَقَدْ كَفَرَ الَّذِينَ قَالُوا إِنَّ اللَّـهَ هُوَ الْمَسِيحُ ابْنُ مَرْيَمَ ۖ وَقَالَ الْمَسِيحُ يَا بَنِي إِسْرَائِيلَ اعْبُدُوا اللَّـهَ رَبِّي وَرَبَّكُمْ ۖ إِنَّهُ مَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ حَرَّمَ اللَّـهُ عَلَيْهِ الْجَنَّةَ وَمَأْوَاهُ النَّارُ ۖ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَارٍ﴿٧٢﴾

Kwa yakini wamekufuru wale waliosema: “Hakika Allaah ni Al-Masiyh mwana wa Maryam.” Na Al-Masiyh alisema: “Enyi wana wa Israaiyl! Mwabuduni Allaah, Rabb wangu na Rabb wenu. (Kwani) Hakika mwenye kumshirikisha Allaah bila shaka Allaah Atamharamishia Jannah, na makazi yake yatakuwa ni Motoni. Na madhalimu hawatopata mwenye kunusuru yeyote.”

لَّقَدْ كَفَرَ الَّذِينَ قَالُوا إِنَّ اللَّـهَ ثَالِثُ ثَلَاثَةٍ ۘ وَمَا مِنْ إِلَـٰهٍ إِلَّا إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ ۚ وَإِن لَّمْ يَنتَهُوا عَمَّا يَقُولُونَ لَيَمَسَّنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ﴿٧٣﴾

Kwa yakini wamekufuru wale waliosema: “Hakika Allaah ni watatu wa utatu. ”Na hali hapana ilaah (muabudiwa wa haki) isipokuwa Ilaah Mmoja (Pekee). Na wasipoacha yale wanayoyasema, bila ya shaka itawagusa wale waliokufuru miongoni mwao adhabu iumizayo.

أَفَلَا يَتُوبُونَ إِلَى اللَّـهِ وَيَسْتَغْفِرُونَهُ ۚ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ﴿٧٤﴾

Je, hawatubii kwa Allaah na wakamwomba maghfirah? Na Allaah ni Mwingi wa kughufuria - Mwenye kurehemu. [Al-Maaidah: 72-74]

Kwa hiyo inalokupasa sasa ni kufuata masharti hayo ya tawbah kwa azimio la nguvu na kuchukizwa kabisa na hicho kitendo na kuazimia kutokurudia na kutokumtii binaadamu badala ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

Hakuna utiifu kwa kiumbe katika kumuasi Muumba” [At-Tirmidhiy].

Kadhaalika, jitahidi umlinganie baba wa rafiki yako aachane na ushirikina na mweleze madhara ya shirki na khatima yake mbaya. Pia rafiki yako huyo atambue ushirikina wa baba yake na mnasihi naye amnasihi baba yake pia. Jaribu kuchukua mafunzo yaliyomo humu alhidaaya kuhusiana na shirki na madhara yake kisha umfikishie na umnasihi afanyie kazi haraka sana kabla mauti haayajamfika akaishia makazi mabaya mno.

Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!

http://alhidaaya.com/sw/node/7157  

 

Na kwa faida zaidi bonyeza kiungo kifuatacho upate Makala za kuhusu tawbah.

 

Faida Na Hukmu Za Kuomba Tawbah

 

Na Allaah Mjuzi zaidi

 

Share