Haijuzu Muislamu Kusherehekea Mwaka Mpya Wa Milaadiyyah (Gregorian)

 

 

Haijuzu  Muislamu Kusherehekea Mwaka Mpya Wa Milaadiyyah (Gregorian)

 

Alhidaaya.com

 

 

Imepokelewa toka kwa Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

 لَتَتَّبِعُنَّ سَنَنَ مَنْ قَبْلَكُمْ شِبْرًا بِشِبْرٍ وَذِرَاعًا بِذِرَاعٍ حَتَّى لَوْ سَلَكُوا جُحْرَ ضَبٍّ لَسَلَكْتُمُوهُ, قُلْنَا يَا رَسُولَ اللَّهِ, الْيَهُودَ وَالنَّصَارَى؟ قَال: فَمَنْ

 

“Mtafuata nyendo za watu waliokuwa kabla yenu, kiganja kwa kiganja, mkono kwa mkono, hata wakiingia kwenye shimo la kenge mtawafuata)).  Tukasema: “Ee Rasuli wa Allaah, Je, Unamaanisha Mayahudi na Manaswara?” Akasema: “Kwani nani zaidi ya wao?” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Tunakaribia kuingia mwaka mpya wa Kikristo (wa kalenda ya Papa Gregory ijulikanayo kama ‘Gregorian Calendar’), na kuna Waislamu wengi wanaosherehekea mwaka huo mpya kama wanavyofanya makafiri, jambo ambalo halimo katika mafundisho ya Kiislamu.

 

Imekuwa ni kawaida Waislamu kujiunga na wafanyakazi wenzao au marafiki zao au majirani zao na kusherehekea sherehe hizi potofu, na kuwa na tabia isiyoendana na mwendo na mafundisho ya dini yetu tukufu. Hivyo tumeona ni muhimu tuwatumie ujumbe huu ndugu zetu popote walipo wajiepushe na mambo haya ya uzushi ya kuiga makafiri.

 

Swali ni kwamba, Vipi Muislamu ajitengee siku kama hizo na kusherehekea?  

 

Jibu kutoka kwa Mwanachuoni wa Ummah, Shaykhul Islaam Ibn Taymiyyah kwamba: 

 

"Sisi Waislamu tusifanye jambo lolote lilokuwa si la kawaida katika siku hizi. Iwe kama siku yoyote nyingine katika maisha yetu bila ya kuwa imekhusishwa na lolote kama mfano wao watu wa Vitabu walivyokuwa hawasherehekei wala kuzifanya siku zetu za ‘Iyd kuwa ni khaswa (maalum) kwao."  

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ametuonyesha ubaya wa makafiri katika Aayah nyingi kama:

 

إِنَّ الْكَافِرِينَ كَانُواْ لَكُمْ عَدُوًّا مُّبِينًا

Hakika makafiri ni maadui zenu walio wazi wazi.” [An-Nisaa: 101]

 

 

Vile vile Amewaita kuwa ni jamaa wa mashaytwaan na vikosi vyao.

 

Kuungana na Ahlul-Kitaab katika sherehe zao imekatazwa kama ilivyokatazwa kuungana na washirikina vile vile. Asibishe mtu kusema kuwa imemaanishwa ni washirikina peke yao na kwamba watu wa Vitabu wana mielekeo au mila kama ya Waislamu takriban.

 

Shaykhul Islaam Ibn Taymiyyah ametoa dalili za kuharamishwa kusherehekea Krismasi, sherehe za wafursi kama Neyrouz, Sherehe za Mayahudi na nyinginezo (kama hizi za mwaka mpya) kwa kusema kwamba zote zinakuja katika hukumu hiyo hiyo moja.

 

Muislamu anapaswa kukataa mwaliko huo wa kusherehekea mwaka mpya hata kama mwaliko huo umetoka kwa Muislamu mwenzake. 

 

Vile vile kaelezea Shaykhul Islaam kuhusu wakati na sehemu za sherehe. Amesema: “Mfano, Muislamu asiuze chakula, nguo au chochote ambacho kitamtia shauku Muislamu awe kama Ahlul-Kitaab katika sherehe zao.”

 

Kutokana na hili tunafahamu kwamba ikiwa kuuza vitu kama hivyo imeharamishwa, seuze kuuza kadi ambazo zina picha za msalaba, (au picha zinazodaiwa ni za Mama Maryam (‘Alayhas-Salaam) kabeba mtoto ambaye ni ‘Iysa (‘Alayhis-Salaam) au kanisa, kwa ajili ya kutumiana salaam na pongezi katika sherehe hizo. Na baya zaidi kujiunga na kuhusika na upotofu huo mkubwa. Makatazo yanaenea pia kwa kila jambo linalohusu sherehe  hizo kama vile kusalimiana (kama kusema “Merry Christmas”  au “Happy New Year” n.k.), kupeana zawadi, vyakula na kadhalika kwani haya ndiyo mambo yanayotendwa na kuwepo katika sherehe hizo.

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametukamilishia dini yetu kabla ya kufa kwake na hakuna jambo lililokuwa jema ila ametujulisha na hakuna jambo baya ila ametukataza. Kwa hiyo katika mafundisho yake ya Sunnah hakuna hata mwaka mmoja uliothibitika kwamba Maswahaba walisherehekea mwaka mpya unapoingia hata wa Kiislam sembuse huo wa kikafiri!

 

Katika Sunnah, Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuja Madiynah na walikuwa wana siku mbili ambazo walikuwa wakipumzika na kustarehe na kucheza. Akasema: "Hizi ni siku gani?" Wakasema: Ni siku ambazo tulikuwa tukicheza na kustarehe katika Ujaahiliya". Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: "Allaah Amekupeni zilizo bora kuliko hizo; Yawmul-Adhwhaa (‘Iydul-Adhwhaa) na Yawmul-Fitwr (‘Iydul-Fitr) )) [Abu Daawuwd]

 

Hii inaonyesha dhahiri kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameharamisha Ummah wake kusherehekea sherehe za makafiri na amefanya hima kuzifuta kwa kila njia.

 

Sababu mojawapo ya kuharamishwa sherehe zao kama za mwaka mpya ni kwa sababu ya maovu, uchafu na fitna zinazotokea humo. Na hata kama hakuna maovu yanayotendeka humo lakini kusherehekea kutasababisha uzushi huu kuendelea katika vizazi vyetu na kusababisha kuingiza mila za kikafiri ndani ya Uislamu.  

 

 

 ‘Umar Ibnil-Khatwtwaab amesema: "Jiepusheni na maadui wa Allaah katika sherehe zao"

 

Imeripotiwa katika mapokezi sahihi kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amr akisema: “Yeyote anayeishi katika nchi isiyo ya Kiislam na akasherehekea sherehe yao ya mwaka mpya, na kuwaiga na akafa katika hali hiyo, basi atakusanywa pamoja nao siku ya Qiyaamah.”

 

 

Wa biLLaahit-tawfiyq

 

 

Share