Mashairi: Yesu Ni Muislamu, Krismasi Hakuna

 

Yesu Ni Muislamu, Krismasi Hakuna

 'Abdallah Bin Eifan (Rahimahu Allaah)

 

Alhidaaya.com

 

  

 

 

Salaam  zangu natuma, ziwafikie nchini,

Nina mengi ya kusema, ndugu nisikilizeni,

Ninawaomba mapema, nikikosa samahani,

Yesu ni Muislamu, krismasi ya nini?

 

 

Krismasi ya nini, Yesu ni Muislamu,

Hana Baba Muhisani, ni mwana wa Mariamu,

Atarudi ardhini, afe kama binadamu,

Yesu ni Muislamu, hakufa yupo mbinguni.

 

 

Yesu Mtume wa Mungu (Allaah) kama Mitume awali,

Ni maadui wa Mungu (Allaah), walipotosha Injili,

Waelewe Walimwengu, ya sasa sio ya kweli,

Yesu ni Muislamu, krismasi ya nini?

 

 

Tunaamini Injili, iloteremshwa zamani,

Ile Injili asili, sasa haipatikani,

Ilikuwa ni ya kweli, Maneno ya Rahmani,

Yesu ni Muislamu, krismasi ya nini?

 

 

Injili ilieleza, atakuja Muhammadi,

Hili halikuwapendeza, Nasara na Mayahudi,

Kwa hivyo waligeuza, Injili kwa makusudi,

Yesu ni Muislamu, krismasi ya nini?

 

 

Na Yesu alitamka, kuna Mtume wa kesho,

Yupo njiani hakika, hakuna mabadilisho,

Muhammadi msifika, kaja na ndie wa mwisho,

Yesu ni Muislamu, hakufa yupo mbinguni.

 

 

Yesu hakuuwawa, hakuwa msalabani,

Mwengine aliyekuwa, sio Yesu asilani,

Yesu alinyanyuliwa, na akapazwa angani,

Yesu ni Muislamu, krismasi ya nini?

 

 

Maiti alifufuwa, kuwatoa kaburini,

Aliwatibu wagonjwa, na vipofu hadharani,

Na yote kwa majaliwa, kwa kudra Zake Manani,

Yesu ni Muislamu, krismasi ya nini?

 

 

 

Tarehe ya kuzaliwa, ina tofauti yakini,

Ya Desemba sio sawa, dalili tuonesheni,

Wafatwe na kuulizwa, Mapadri makanisani,

Yesu ni Muislamu, krismasi ya nini?

 

 

Biblia tazameni, haitaji Krismasi,

Neno hili silioni, pekua makaratasi,

Ni neno kabisa geni, geni bila wasiwasi,

Yesu ni Muislamu, krismasi ya nini?

 

 

Yesu hakuitukuza, siku yake kuzaliwa,

Na hilo tena nyongeza, na kuzidi kupotowa,

Wakati mnapoteza, na lini mtaelewa?

Yesu ni Muislamu, krismasi ya nini?

 

 

Na pia Waislamu, Maulidi wanasoma,

Hili pia si timamu, Subhaana Hakusema,

Ni kudanganya kaumu, na kuwatwisha lawama,

Yesu ni Muislamu, krismasi ya nini?

 

 

Maulidi, Krismasi, uzushi wa duniani,

Mitume na wafuasi, hawakufanya zamani,

Yanamuudhi Mkwasi, hamuelewi kwa nini?

Yesu ni Muislamu, hakufa yupo mbinguni.

 

 

Na mti wa Krismasi, unapambwa kwa makini,

Unavutia kiasi, ukitazama machoni,

Lakini ndio maasi, Biblia isomeni, (Jeremiah: 10-3,4)

Yesu ni Muislamu, krismasi ya nini?

 

 

Na pia "Santa Klausi'" hakutajwa kitabuni,

Iliobaki ni basi, umma wapo hatarini,

Wajiepushe upesi, wasiingie motoni,

Yesu ni Muislamu, krismasi ya nini?

 

 

Wasiwafanye wajinga, lazima waulizeni,

Kuuliza si ujinga, msichoke ulizeni,

Hapa shairi nafunga, nimefika kikomoni,

Yesu ni Muislamu, hakufa yupo mbinguni.

 

 

 

Share