Sigara Na Tumbaku: Mtazamo wa Uislamu - 4

 

Sigara Na Tumbaku: Mtizamo Wa Uislamu - 4

 

Imetafsiriwa na Naaswir Haamid

  

Fatwa Kutoka Kwa

 

Shaykh 'Abdullaah Bin 'Abdil-'Aziyz Bin Baaz

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Hukumu Kuhusiana Na Uvutaji Sigara Na Hukumu Ya Imaamu Muovu Anayevuta Sigara

 

 

Sifa zote ni Zake Allaah, Bwana wa ulimwengu wote, Rahmah na Amani za Allaah ziwe juu ya Mtume wetu, Muhammad, na juu ya watu wake wa nyumbani na Maswahaabah zake.

 

Niliulizwa na baadhi ya ndugu kuhusu hukumu ya uvutaji sigara na usahihi wa yule Imaam anayevuta wazi wazi, huku akieleza (muulizaji) kwamba ovu hili limeenea na limewaathiri watu wengi.

 

 

Hivyo, jibu ni kama lifuatalo:

 

Ushahidi wa Diyn unathibitisha kwamba uvutaji wa sigara ni haramu, na kwamba (ushahidi) unatokana na kuwa (hiyo sigara) ni khubth na yenye madhara mengi kutokana na kuitumia kwake, kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Hakuweka kikwazo chochote kwa chakula au kinywaji isipokuwa karuhusu kile kilicho kizuri na chenye manufaa. Na kwa yale mambo ambayo yanasababisha uharibifu wa Diyn ya mtu au maisha yake, au yenye kubadilisha ufahamu wa kawaida wa akili, Allaah, Mtukufu, Ameikataza. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ni Mwenye huruma zaidi kwa waja Wake kuliko wao wenyewe. Yeye Ndiye Mbora wa Hikmah na Mbora wa Ujuzi ndani ya matamko Yake, matendo, shari’ah na utanashati, na wala Haharamishi chochote bure bure. Haumbi kitu kwa kutumia uongo, wala Haamrishi kitu kwa waja Wake ikiwa ndani yake hakuna manufaa yoyote, kwani Yeye, Mtukufu, ndiye Mbora wa mahakimu na Mbora wa Rahmah. Yeye Mbora wa Ujuzi Anaelewa kipi kinafaa kwa waja Wake na kipi kina manufaa kwao ndani ya maisha yao haya na ya baadaye, kama Alivyosema (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

إِنَّ رَبَّكَ حَكِيمٌ عَلِيمٌ ﴿١٢٨﴾

Hakika Rabb wako ni Mwenye hikmah wa yote, Mjuzi wa yote. [Al-An'Aam: 128]

 

Na Amesema (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلِيمًا حَكِيمًا ﴿١١﴾

Hakika Allaah daima ni Mjuzi wa yote, Mwenye hikmah wa yote. [An-Nisaa: 11]

 

Na kuna Aayah nyengine nyingi ambazo zinaeleza maana hiyo hiyo.

 

Na kutokana na ushahidi wa Qur-aan kuhusiana na uharamu wa uvutaji sigara ni tamko Lake (Subhaanahu wa Ta’ala) ndani ya Kitabu Chake Kitukufu kwenye Suraatul-Maaidah:

 

يَسْأَلُونَكَ مَاذَا أُحِلَّ لَهُمْ ۖ قُلْ أُحِلَّ لَكُمُ الطَّيِّبَاتُ

Wanakuuliza wamehalalishiwa nini? Sema: Mmehalalishiwa vizuri.. [Al-Maaidah: 4]

 

Na Amesema ndani ya Suwraah Al-A'raaf Akimfafanulia Nabiy wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

الَّذِينَ يَتَّبِعُونَ الرَّسُولَ النَّبِيَّ الْأُمِّيَّ الَّذِي يَجِدُونَهُ مَكْتُوبًا عِندَهُمْ فِي التَّوْرَاةِ وَالْإِنجِيلِ يَأْمُرُهُم بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَاهُمْ عَنِ الْمُنكَرِ وَيُحِلُّ لَهُمُ الطَّيِّبَاتِ

Wale wanomfuata Rasuli; Nabiy asiyejua kusoma wala kuandika ambaye wanamkuta ameandikwa kwao katika Tawraat na Injiyl, anawaamrisha mema na anawakataza munkari, na anawahalalishia vizuri na anawaharamishia maovu,.. [Al-A'raaf: 157]

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ameweka wazi ndani ya Aayah mbili hizi tukufu kwamba Yeye (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Hakuruhusu chochote kwa waja Wake isipokuwa yale mambo mazuri na yaliyo safi, ambayo yana manufaa kwa chakula na kinywaji. Na ama kwa chakula na kinywaji kinachodhuru, kama vile vyenye kulevya, kusinzilisha, au chakula chengine au kinywaji chenye madhara kwa Diyn ya mtu, mwili, au akili, hivyo ni miongoni mwa khabaaith zilizozuiliwa. Matabibu na wengineo wenye elimu ya mada hii wanakubaliana kwamba sigara zina madhara makubwa kwa afya. Pia wameeleza kwamba ni sababu ya kuenea maradhi mabaya, yakiwemo saratani, na kusimama kwa mapigo ya moyo. Na iwapo hili ni kweli hakika, basi hakutakuwa na shaka yoyote ndani ya uharamu wa chochote chenye mfano wa athari hizo, na inakuja kuwa ni wajibu kuonya dhidi yake. Wenye maarifa wasilaghaiwe na makundi makubwa ya watu wenye kuvuta sigara, kwani hakika Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amesema ndani ya Kitabu Chake Kilicho wazi:

 

وَإِن تُطِعْ أَكْثَرَ مَن فِي الْأَرْضِ يُضِلُّوكَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ ۚ إِن يَتَّبِعُونَ إِلَّا الظَّنَّ وَإِنْ هُمْ إِلَّا يَخْرُصُونَ ﴿١١٦﴾

Na kama ukiwatii wengi walioko ulimwenguni, watakupoteza na njia ya Allaah. Hawafuati isipokuwa dhana tu, na hawakuwa ila wenye kubuni uongo. [Al-An'aam: 116]

 

Na Amesema (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

أَمْ تَحْسَبُ أَنَّ أَكْثَرَهُمْ يَسْمَعُونَ أَوْ يَعْقِلُونَ ۚ إِنْ هُمْ إِلَّا كَالْأَنْعَامِ ۖ بَلْ هُمْ أَضَلُّ سَبِيلًا ﴿٤٤﴾

Je, unadhania kwamba wengi wao wanasikia au wanatia akilini? Wao si chochote isipokuwa kama wanyama, bali wao wamepotea zaidi njia. [Al-Furqaan: 44]

 

Ama kwa usahihi wa Uimamu mvuta sigara, au kwa mnasaba wa mada hii, mtu yeyote anayeasi, hakuna manufaa yoyote kwamba matashi yao yachukuliwe kama ni Uimamu. Isipokuwa, imeamrishwa kwamba mtu achaguwe kutoka kwa Waislamu walio waadilifu wanaojulikana kwa matendo yao mazuri na ucha Mungu, kwani suala linalohusu Uimamu hakika ni kubwa. Na kwa sababu hii Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

Kutoka kwa Abu Masúud Al-Badriyyi akisema: Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Awaswalishe watu yule mwenye kujua kusoma zaidi Kitabu cha Allaah na mwenye kutangulia zaidi kwa kisomo. Ikiwa visomo vyao ni sawa, basi aswalishe yule aliyetangulia kuhama (Hijrah), na ikiwa wako sawa katika Hijrah[1], aswalishe mkubwa wao kwa umri. Wala asiswalishe mtu katika nyumba yake wala katika mamlaka yake wala asikae kwa heshima yake isipokuwa kwa ruhusa yake [mwenyeji]." [Impokewa na Muslim, Abu Daawuud]

 

Katika mapokezi mengine, baada ya mwenye kujua zaidi Kitabu cha Allaah, anafuatia mwenye kujua zaidi Sunnah.

 

Na ndani ya Swahiyhayyn, amesema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba alimwambia Maalik bin Huwayrith na Swahaba zake:

 

"Pale wakati wa Swalaah unapoingia, aadhini mmoja wenu, na aliye mkubwa wenu kwa umri aongoze (Swalaah)."

 

Lakini wanachuoni, (Rahimahum Allaahu), wametofautiana: Je Imaam na Swalaah yake ya jama’ah inaruhusika? Wengine wameeleza kwamba Swalah inayoswaliwa nyuma yake sio sahihi, kutokana na udhaifu wa Diyn yake na makosa ya Iymaan yake, wakati wengine wameeleza kwamba, wakitoa hoja kwamba iwapo Swalaah ni sahihi kwake mwenyewe, inajuzu kwamba ni sahihi pia kwa wale wanaomfuata. Pia, Swahaba wengi wameswali nyuma ya mabalozi na watawala ambao walijulikana kwa unyanyasaji wao na madhambi yao, kama Ibn Úmar (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) alivyoswali nyuma ya al-Hajjaaj aliyejulikana kwa kuwanyanyasa watu. Na hii ndio fatwa sahihi, kwamba Uimamu wa yule anayevuta sigara na pia Swalaah ya wale wanaomfuata yeye ni sahihi. Lakini itambulike kwamba sio vyema kwamba matendo yake yachukuliwe kama ni ya ki Imaamu, wakati wapo waadilifu wengine wanaoweza kuchaguliwa badala yake.

 

Na hili hakika linajibu kwa ufupi, kwani tunakusudia kutaja kanuni kuu kuhusiana na masuala haya mawili na kuthibitisha baadhi ya ushahidi kuhusiana nayo. Wanachuoni wamethibitisha hukumu kuhusiana na masuala haya yaliyo mkononi, na yeyote anayetaka maelezo (zaidi) ya mada hii, bila ya shaka yoyote watayapata.

 

Tunamuomba Allaah kwamba Ayabadilishe matendo ya Waislamu na Awaongoze kwenye usahihi wa Diyn na wawe wenye hadhari kwa kile (kinachotokea) kwa kupingana nayo. Hakika Yeye ni Mbora wa Ukarimu.

 

Na Rahmah na Amani Zake ziwe juu ya Nabiy wetu, Muhammad, na juu ya watu wake wa nyumbani na Maswahaabah zake.

 

Shaykh ‘Abdul-‘Aziyz bin ‘AbdiLlaah bin Baaz.

 

Mwenyekiti wa Baraza la Wanachuoni Wakuu.

Marejeo:

"Hukumu ya Uvutaji Sigara" Muhammad bin Ibraahiym (Rahimahu Allaahu)

"Hukumu Ya Uvutaji Sigara" 'Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa’diy. (Rahimahu Allaahu)

"Hukumu Ya Uvutaji Sigara" 'Abdul-'Aziyz bin 'AbdiLlaah bin Baaz. (Rahimahu Allaahu)

"Hukumu Ya Uvutaji Sigara" Muhamamd bin Swaalih al-'Uthaymin.

"Hukmul-lslami fiyt-Tadkhiyn" Muhammad bin Jamil bin Zinu.

"Hukmud-Diyn fil-Lihyati wat-Tadkhiyn" 'Aliy bin Hasan al-Halabiy.

"Uvutaji Sigara Na Athari Zake Kwa Afya" Dkt. Muhammad bin 'Aliy al-Barr.

 

 

 

 

[1] Hijrah: Kuhama kutoka ardhi ya kikafiri kwenda ardhi ya Kiislamu.

Share