Kufanya Majaribio Ya Fiziolojia Ya Wanyama

SWALI:

 

 

Jazaakallah kheir kwa jibu la swali langu. Alhamdulillah nimefanikiwa kufikia uamuzi wa kuoa mke wa pili...Allah awalipe jazaa ya kheir kwa ushauri wenu kwangu kulifanya hili ambao kwa namna moja ama nyingine umechangia kufikia maamuzi haya...naomba dua zenu inshaallah.

 

  Nina ombi lingine: Hapa chuoni nimepata fursa ya kufikiriwa kuwa katika undergraduate medical student innovative programme ambapo unachagua a unique title, unaiandikia proposal ambayo  inapitiwa na professor..ikipita kwake wapewa fund na facilities husika ili kufanya hiyo experiment.

Nimefikiria niifanye experiment inayohusu physiology (tunatumia wanyama kama vile sungura, mbwa, panya na chura)....ombi langu ni kuwa mjaribu kunitumia hadith na aya ambazo munafikiri zina relate na hii field from which ninaweza kupata title na inshallah ninahisi nitafikia sehemu nzuri katika hii fikra.  


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Tunashukuru kwa swali lako hilo ambalo inadhihirisha kuchunga kwako na kuwa na khofu ya kukiuka mipaka ya Shari’ah.

 

Kuchunga haki za wanyama ni jambo ambalo Uislamu umelipa nafasi na kulisisitiza. Wanyama wana haki zao kwetu pamoja na kwamba wameumbwa kwa ajili yetu.

 

Ama kuhusu kutaka kujua Aayah na Hadiyth ya jambo hilo la kufanya utafiti kwa kuwafanyia majaribio wanyama, hakuna Aayah au Hadiyth ya moja kwa moja ambayo inaeleza suala hilo ila kuna msingi wa Kiislamu kuhusu utendaji wa majaribio yako au yenu kwa kutumia wanyama, ni muhimu kufahamu kuwa inaruhusiwa kutumia wanyama kufanyia majaribio hayo ya kisayansi, ikiwa utumiaji wake utakuwa na manufaa kwa binaadamu. Lakini kuweko na mipaka ya kuhitajika kwake na pia watumiliwe kwa upole na huruma bila ya ukatili na bila ya kuwatesa.

 

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa alihi wa sallam) amesema:

 

 

  ((إن الله كتب الإحسان على كل شيء . فإذا قتلتم فأحسنوا القتلة وإذا ذبحتم فأحسنوا الذبحة ، وليحد أحدكم شفرته وليرح ذبيحته)) صحيح الترمذي و قال الشيخ الإلباني صحيح  

 

 

 

((Allah Amefaradhisha ihsaan kwa kila kitu, kwa hiyo mnapoua (wanyama) fanyeni ihsaan katika uuaji na mnapochinja fanyeni ihsaan katika uchinjaji, basi atie makali mtu kisu chake na ampunguzie (amuondoshee makali) kichinjo chake)) [Swahiyh At-Tirmidhiy na Shaykh Al-Albaaniy pia kasema ni Swahiyh]

 

 

 

Kuchunga mipaka hiyo ni kwa mfano ikiwa itapatikana matokeo baada ya jaribio la mnyama mmoja, basi hapana haja tena kutumia wanyama wengine kufanya jaribio hilohilo. Pia ikiwezekana kufanya majaribio kutokana na tissues cultures au cell cultures, basi ipendekezwe kutumia hivyo badala ya wanyama. Na ikibidi majaibio yafanywe kwa wanyama, basi kuwekwe vipimo vya kudhibiti ukatili, uumizaji au uuaji bila ya huruma, kwani Dini yetu imetuamrisha tuwafanyie upole, ihsani na huruma wanyama.

 

Tumepata mafunzo kutoka katika kisa maarufu kilichotajwa kwenye Hadiyth ambacho kulikuwa na mwanamke ambaye ingawa alikuwa ni Mcha mungu, lakini makazi yake yakawa motoni kwa kutokumfanyia ihsani paka.

 

Kadhalika kuna mtu mmoja alikwenda kwa Shaykhul Islaam Ibn Taymiya na kulalamika kwamba sisimizi wengi wameingia nyumbani kwake na akamuuliza kama anaruhusiwa kuwauwa kwa kuwachoma moto. Ibn Taymiyyah alimjulisha kwamba hairuhusiwi kuwachoma moto bali anaweza kuwaua kwa njia nyingine isiyo ya kikatili.

 

Hata hivyo, kwa ajili ya umuhimu wa mada yenyewe na pia unaweza kupata mahusiano ya Aayah na Hadiyth ya suala hilo, ni nasaha yetu kwamba utafute na kusoma vitabu vifuatavyo ambavyo vitakusaidia sana katika hilo:

 

  1. The Bible, The Qur-aan and Science – Dr. Maurice Bucaille.

  2. God Arises – Mawlana Wahiduddin Khan.

  3. Medical Sciences in the HOLY QUR'AN and SUNNAH – Prof. A. M. Adam (wa Kenya, hiki bado hakijachapishwa ila tunaweza kukupa anuani ya mwandishi uwasiliane naye kwa faida zaidi).

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share