Zingatio: Sifa Njema Ni Za Allaah Ambaye Kwa Neema Yake Yanatimia Mambo Mema

 

Zingatio: Sifa Njema Ni Za Allaah Ambaye Kwa

Neema Yake Yanatimia Mambo Mema

 

Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

Moja katika sifa nzuri za Muislamu ni kushukuru kwa kile anachopewa. Shukurani hizi sio tu kwa Rabb Mtoaji bali hata kwa binaadamu wenzake.

 

Kwa hakika utoaji ni Wake Muumba, kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ndie Asiyekuwa na mwisho wa kufilisika neema Zake. Hivyo Anastahiki kushukuriwa na viumbe Vyake vyote. Shukurani hizi zinahitajika kuwa kwa kwa ulimi uliogandana na moyo pamoja na vitendo. Kauli bila ya kusafishwa nia ndani ya moyo haitakuwa na thamani ya shukurani.

Allaah Anasema ndani ya Aayah ifuatayo kushukuriwa Yeye na wazee wawili:

أَنِ اشْكُرْ لِي وَلِوَالِدَيْكَ 

… ya kwamba unishukuru Mimi na wazazi wako. [Luqmaan: 14]

 

Na pia Rabb Mlezi Ametuusia kutoa shukurani kwa vitendo:

اعْمَلُوا آلَ دَاوُودَ شُكْرًا

Tendeni enyi familia ya Daawuwd kwa shukurani!  [Sabaa: 13]

 

Shukurani hizo zinatakiwa kutolewa pasi na kukufuru:

وَاشْكُرُوا لِي وَلَا تَكْفُرُونِ

Na nishukuruni wala msinikufuru. [Al-Baqarah: 152]

Hivyo, Muislamu inamstahikia juu yake aangalie kwa umakini namna alivyoneemeshwa kwa neema zisizokuwa na mfano. Neema ambazo ameenemeshwa tokea alipokuwa ndani ya tumbo la mama yake hadi kuletwa hapa ulimwenguni, na bila ya shaka yoyote neema hizi huendelea hadi Siku ya Hesabu.

Naye Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amehimiza sana kushukuru kama inavyotuonesha Hadiyth ifuatayo:

 

An-Numan bin Bashiyr amesimulia kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Kuzungumzia neema za Allaah ni shukurani, na kutofanya hivyo ni ukosefu wa shukurani. Yule asiyeshukuru kwa kidogo hatashukuru kwa kikubwa na yule asiyewashukuru watu, hamshukuru Allaah. Jamaa ni neema na utengano ni laana."

Basi ni lazima kutoa shukurani kwa Rabb Mlezi kutokana na neema hizo. Shukurani sio tu kusema: AlhamduliLlaah, bali ni kutenda mema na kuachana na maovu. Muislamu akifanya hivyo atakuwa katenda adabu njema mbele ya Rabb Muumba. Kwani ni ukosefu wa adabu iwapo Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kakufadhili kwa neema nyingi kisha tena unazisahau neema hizo na unamsahau Yule aliyekufadhili na akakukirimu.

Kwa hakika hakuna neema yoyote tuliyonayo, isipokuwa imetoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Hivyo ni wajibu wetu kushukuru.

 

 

Share