Zingatio: Unaikimbia Elimu Ya Bure

 

Zingatio: Unaikimbia Elimu Ya Bure

 

Naaswir Haamid

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Imekuwa ni kawaida kuzifuta forwards na emails zilizo sahihi kuhusu Uislamu. Wengi wa Waislamu watumiwao emails zenye mada ya Kiislamu humalizia kwenye icon ya delete tu. Hufikia hadi kuwekwa alama kichwani mwa mtu kuhusu emails za mtu Fulani, zikiingia tu basi hufutwa.

 

 

Kwa hakika, wenye elimu ndio wanapaswa kupembejewa na kuwa nao karibu kinyume na majahili. Katika utangulizi wa Hadiyth alizosimuliwa Imaam Az-Zuhuriy, anasema Ibnu Swalaah:

 

 

"Nilikwenda kwa Abdul-Malik bin Marwaan (Khalifa wa Waislam wakati wa utawala wa Banu Umayyah)

 

Akaniuliza: 'Unatokea wapi ee Az-Zuhuriy?'

 

Nikamwambia: 'Natokea Makkah.'

 

Akaniuliza: 'Huko Makkah, nani mwenye kupendwa na kufuatwa na kusikilizwa kauli zake?'

 

Nikamwambia: "Atwaa bin Abi Rabaah.'

 

Akaniuliza: "Ni katika Waarabu huyu au katika watumwa walioachwa huru?'

 

Nikamwambia: 'Ni katika watumwa walioachwa huru.'

 

Akaniuliza: 'Sababu gani zilizomfanya apendwe na kufuatwa?'

 

Nikamwambia: 'Elimu yake ya dini na riwaya.'

 

Akasema: 'Hakika wenye elimu ya dini na riwaya ndio wanaopaswa kupendwa na kufuatwa.' [Tuhfatul Ahwaziy – Al-Mubaarak Puriy – mlango wa 1804]

 

 

Ni wajibu wa kila Muislamu kuelewa Uislamu wake, kama hujakubaliana na hoja ya mtu fulani ni vizuri ukaijibu au ukaiachia tu baada ya kuisoma ndio ukaifuta, sio kuifuta moja kwa moja bila ya kuisoma. Ni muhimu kwa ndugu zetu wanaopokea emails (barua pepe) nzuri zilizo sahihi kuhusu Uislamu na nyenginezo zenye manufaa kuzisoma na kuzipitia japo kwa mara moja na sio kuzifuta hata bila ya kuzipitia.

 

Tabia hii ya kuzifuta emails zilizo sahihi kuhusu Uislamu huenda zikawa zinasababishwa na sababu zifuatazo:

 

1)     Dharau ya kutohitaji kuusoma Uislamu.

 

2)   Muislamu kushughulishwa sana na habari zisizo na manufaa kwenye Uislamu. Mfano habari za wanamichezo, muziki, runinga, redio, upeku, magazeti yanayoamsha hisia za mapenzi na hata kushughulikia kupita mpaka mtiririko wa mechi za mpira. Pia utakutia Muislamu mzima ana muda wa kwenda kucheza drafti, keram, play station na mengineyo. Ajabu hana muda wa kusoma hata email moja ya elimu kuhusu Uislamu lakini ana muda wa kusoma email za ajabu ajabu zenye upuuzi, mapicha na marembo mengi alimuradi zinamvutia yeye au kumuhusisha na matamanio ya nafsi yake na dunia yake. Au email za uzushi na mambo yanayohusishwa na dini lakini hayna dalili wala msingi, na hizo ndizo zenye kuenezwa sana.

 

3)    Kuamini mtu kuwa ametosheka na elimu alokuwa nayo, hali ya kuwa elimu haina mwisho na pia Wanazuoni wametuamrisha tutafute elimu hata ikiwa ni kuifuata mwisho wa dunia.

 

4)     Akili za watu zimetekwa nyara kutafuta rizki zaidi na anasa kuliko elimu ya Uislamu na hasanaati (mambo mema). Tunaona watu wakitumia muda mrefu sio tu kwenye kazi bali muda mwingi hupotezwa kwenye sinema, mipira na kadhalika.

 

 

Namna ya kujirekebisha:

 

a)    Jiweke karibu na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa kuswali ndani ya wakati wake na kusoma Qur-aan kila siku.

 

b)    Jiamini kuwa wewe ni Muislamu na kama Swalah ni faradhi ndivyo elimu inavyoangukia kuwa ni faradhi.

 

c)    Tambua na fahamu kuwa muda unakatika na haurudi. Unaweza kupoteza muda lakini kuurudisha haiwezekani. Uchunge muda wako kabla ya kifo chako.

 

d)  Kusoma email sahihi na kuisambaza forward kutakupelekea kuengeza kapu lako la thawabu. Hivyo, fanya bidii kwa makusudi kuitafuta elimu.

 

e)     Tenga wakati maalum kwa siku kusoma makala za Kiislamu japo nusu saa kwa siku moja. Achana kabisa na habari za muziki, mechi za mpira na mengineyo ya upuuzi.

 

f)     Ni vizuri kwa makala uliyoiona ina mvuto lakini kutokana na muda wako kuwa ni mdogo ukapelekea kushindwa kuisoma, basi ni vyema ukaihifadhi save kwenye drive. Na ukipata wakati unaipitia bila ya kulazimika computer kuunganishwa internet ndio upate kuirudia. Kama unayo printer, si vibaya ukaichapisha na kuipitia kwa wakati wako mnasaba.

 

g)     Omba kwa Rabb Mtukufu Akuwezeshe uwe na juhudi katika dini ya Kiislamu ili kuijenga Akhera yako kuliko dunia yako.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atuwezeshe kuwa na juhudi katika dini yetu tukufu ya Kiislamu.

 

 

Share