Kuchangia Na Kushiriki Shughuli Za Bidaa Ni Dhambi?

 

Kuchangia Na Kushiriki Shughuli Za Bidaa Ni Dhambi?

 

Alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Assalaam Alaykum

Nimepatwa na mtihani, mzazi wangu kafariki na ndugu wanataka tusome dua ya hitima mwezi huu, Sasa nauliza je nitoe mchango katika hiyo shughuli?

Pili je kama sitatoa pesa nikahudhuria naweza kula nyama iliyochinjwa katika hitima hiyo, Naomba mnipatie jibu mapema ili niwape msimamo kwani nahofia wasione nimewasaliti ila nataka kama haiwezekaniki niwakatalia kwa points

 

Wabilah Tawfiq

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Katika Swali hilo kuna mas-ala mawili ambayo yote hayafai kutendeka; khitmah na kuchinja kwa ajili ya aliyefariki:

 

Khitmah ni bid'ah (uzushi) kwani halimo kabisa katika mafunzo ya Sunnah, kwa maana hakuna dalili yoyote kama Nabiy Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alifanya khitmah au kukubali ifanywe. Na lau kama ni jambo sahihi basi tungelipata uthibitisho kuwa lilitendeka walipofariki watu wake au Maswahaba    zake.  Lakini hakuna hata usimulizi mmoja unaoelezea kuwa lilitendekea zama hizo wala zama za wema waliopita. Hivyo hatuna budi kujiepusha nalo kwani maonyo mengi tumepata kutoka kwa Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kujiepusha na mambo ya bid'ah.  

 

Bid’ah kama hizo ambazo zimeanzishwa zamani bila ya dalili, imekuwa ni jambo sugu katika jamii.

 

 

 

Ni wajibu wetu kuendelea kuwafunza watu na kuwafahamisha mafunzo sahihi tusichoke, hata kama ni jamaa zetu tujitahidi kuwapa nasaha na kutowatenga.

 

 

Bonyeza viungo kifuatacho upate maelezo kamili kuhusu hukmu ya khitmah na ujaribu kuwafikishia ndugu zako ujumbe huo ili wajiepushe nalo.

 

Khitma: Kutokufaa Na Madhara Yake

 

Kuchinja pia kwa ajili ya aliyefariki, hakuna ushahidi kuwa Nabiy  (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alifanya hivyo kwa ajili ya mtu aliyekufa.  Alichinja kwa ajili ya Umma huu wa Kiislamu Yawmun-Nahr (siku ya kuchinja) ambayo ni tarehe 10 Dhul-Hijjah.  Alichinja pia kwa ajili ya ‘Aqiyqah wanayofanyiwa watoto. Kama alivyowafanyia wajukuu zake kina Al-Hasan na Al-Husayn (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa).

 

 

Kuchangia katika mambo hayo haifasi kabisa kwani utahesabika kuwa ni mmojawapo wa mwenye kutenda bid’ah hiyo.  

 

 

Hivyo inakupasa kwanza ujiepushe kabisa na mambo hayo. Kisha ujaribu kuzuia bid’ah hizo zisitendeke, na kufanya hivyo utakuwa umetimiza wajibu wako wa kuzuia maovu yasitendeke kama tulivyoamrishwa katika Hadiyth ifuatayo:  

 

عن أَبي سعيدٍ الخُدْريِّ رضي اللَّه عنه قال : سمِعْتُ رسُولَ اللَّه صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم يقُولُ : ((مَنْ رَأَى مِنْكُم مُنْكراً فَلْيغيِّرْهُ بِيَدهِ ، فَإِنْ لَمْ يَسْتَطعْ فبِلِسَانِهِ ، فَإِنْ لَمْ يَسْتَطِعْ فَبقَلبهِ وَذَلَكَ أَضْعَفُ الإِيمانِ)) رواه مسلم .

Kutoka kwa Abuu Sa'iyd Al-Khudhriy (Radhwiya Allahu 'anhu) ambaye amesema: Nilimsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)   akisema: ((Yeyote yule atakayeona kitendo kiovu akiondoe (abadilishe) kwa mkono wake, ikiwa hawezi basi kwa ulimi wake (alikemee au kukataza), na ikiwa hawezi basi kwa moyo wake (achukie) na huo (yaani kuona baya na kunyamaza) ni udhaifu wa Imani)) [Imesimuliwa na Muslim]

 

 

Yanayompasa kumfanyia aliyefariki kama yalivyokuja katika mafunzo ya Sunnah ni; kumuombea du'aa, kumtolea swadaqah,  kumfanyia Hajj ikiwa hakuwahi kufanya.  Kwa hiyo badala ya kufanya jambo lisilo na msingi ni bora kufanya yale ambayo hayana shaka yaliyopatikana dalili zake katika mafunzo sahihi. Hivyo vile vile utakuwa umetoa mafunzo sahihi ya Sunnah na utajichumia thawabu kwa hayo.

 

 

Bonyeza kiungo kifutacho upate maelezo zaidi kuhusu mas-ala haya: 

 

Kumsomea Khitmah Maiti Kumchinjia Na Kumuombea D'uaa Kwa Pamoja

 

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Azidi kutuongoza kufuata yaliyo haki na kuacha yaliyo batili.

 

Na Allah Anajua zaidi

 

 

Share