Kwenda Kwa Sheikh Kusomewa Kuondosha Mikosi Inajuzu? Je Allaah Kaumba Miti 99 Tujitibu Nayo?

 

 

Kwenda Kwa Sheikh Kusomewa Kuondosha Mikosi Inajuzu?

Je Allaah Kaumba Miti 99 Tujitibu Nayo?

 

  Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Asaalam aleykum. Inshaallah kheri kutoka kwa Allah iwe juu yenu.

Nimekuwa nikishawishika sana kutoka kwa jamaa zangu niende kwa masheikh kusomewa duaa ili kuondoshwa mikosi na nuksi kwani mambo yangu hasa ktk ndoa zimekuwa haziwi nimekua nikiwakatalia na kuwaambia madhara yake kwani unaweza kumshirikisha Allah kwani huko hupewa dawa za miti shamba kuogea kwa kutoa mikosi na kuwa na bahati na kunywa maji yaliyosomewa lkn wamekuwa wakiniambia Allah ameumba miti 99 ajili tuweze kujitibu kutokana nayo, sasa sina elimu ya kuweza kuwapinga ninaomba fatwa juu ya hilo niweze kuwaeleza na pia kama si vby ninaweza na mimi kwenda kusomewa niwe na bahati kwani ni kweli ndoa kwangu imekua ni hadithi lkn hata hivo namshkuru Allah kwani kuna mengi kanirudhuku. Jazaak Allaah khayra

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Matatizo hutokea na kumpata mtu kwa sababu kadhaa. Mara nyingine hayo mnayoyaita ni mikosi huenda ikawa ni mitihani kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).   Mtihani kukutazama uimara wako wa kuweza kushikilia Uislamu katika wakati tofauti.

 

Mitihani inapokuja inatakiwa Muislamu asiende kwa masheikh wala maustadh wala waalimu wenye kutumia uchawi ili kuondoa mikosi bali kurudi kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  na Rasuli Wake   (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)   kwa kufuata maagizo yao na kuacha makatazo yao.

 

Uchawi ni shirki na Muislamu hafai kutumia, bali anafaa awe ni mwenye kusoma Aayah, Surah pamoja na Adhkaar zilizothibiti katika Sunnah.

 

Bonyeza viungo vifuatavyo upate mafunzo   yanayohusiana na Ruqya (kinga) mbalimbali:

 

 

Ruqyah: Kinga Na Tiba Katika Shariy'ah

 

Du’aa Za Ruqyah (Kinga) Faida Na Sharh Zake

 

Na yafuatayo ni ziyada ya faida:

 

1-Kusoma Aayah kumi za al-Baqarah (2) ambazo zinaepusha nyumba ya mmoja wetu na mashaytwaan. Nazo ni kuanzia Aayah 1-5, 255-257 na 284-286. Hizi Aayah zinatakiwa zisomwe asubuhi na jioni.

 

2-Kusoma Suwrah Al-Ikhlaasw, al-Falaq na an-Naas mara tatu tatu, asubuhi na jioni na pia wakati wa kulala.

 

3-Qur-aan yote ni Shifaa inatakiwa kila Muislamu awe na ada ya kuisoma na kujua maana yake na kutekeleza yaliyomo ndani yake.

 

4-Usome du’aa ambazo ni kinga unapotoka nyumbani na unapoingia.

 

5-Du’aa ambayo wewe na mumeo mnatakiwa msome wakati wa kitendo cha ndoa ambayo inawalinda na kukilinda na Shaytwaan kitoto kitakachozaliwa kutokana na tendo hilo.

 

6-Adhkaar za baada ya Swalaah na pia wakati wa kulala.

 

7-Usome Adhkaar za asubuhi na jioni

 

Adhkaar hizo na nyenginezo tele zinapatikana katika kitabu kifuatacho:

  

Hiswnul-Muslim: Du’aa Na Adhkaar Kusoma Na Kwa Kusikiliza (Toleo Lilohaririwa)

 

Ama  kuhusu miti ambayo inaweza kutumika katika matibabu inaweza kuzidi 99 au kuwa chini ya idadi hiyo, kwani hakuna dalili yoyote kuhusu idadi hiyo. Inatakiwa ikiwa ni kufanya matibabu basi uende kwa madaktari waliobobea au kwa matabibu mahiri wanaotumia Sunnah katika kutibu kwao bila ya kutumia ushirikina. Tufahamu kuwa hakuna ugonjwa ambao hauna dawa, hiyo ni kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuamuru tutafute dawa tunapokuwa wagonjwa. Na katika kauli yake nyingine akasema:

 

 عن أبي الدرداء رضي الله عنه قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم : ((إن الله تعالى أنزل الداء والدواء وجعل لكل داء دواء فتداووا ولا تداووا بالحرام))

Abuu Dardaa (Radhwiya-Allaahu ‘anhu) amesimulia kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah Ameteremsha maradhi na dawa zake. Kwa kila maradhi kuna dawa yake, basi jitibuni wala msijitibu kwa yaliyo haraam)) [Al-Bukhaariy na Abu Daawuwd]

 

Na pia:

 

   عن عبدالله بن مسعود :قال رسول الله صلى الله عليه وآله وسلم  (( ما أنزل الله داء إلا أنزل له دواء فعليكم بألبان البقر فإنها ترم من كل الشجر))

Kutoka kwa Ibn Mas’uwd (Radhwiya-Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:  ((Allaah Hakuteremsha maradhi ila Ameteremsha dawa zake, basi juu yenu (kunyweni) maziwa ya ng'ombe  kwani yanatokana na kila aina ya miti)) [Hadiyth Swahiyh Hasan ameisahihisha Al-Albaaniy]

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share