Mume Aliyesilimu Hafanyi Bidii Kujifunza Kusoma Qur-aan Anasoma Tafsiyr Pekee

 

SWALI:

 

Asalam aleykum warahmatulla, na mshukuru ALLAH SUBHANNA kwa kunionesha hii site. Swali langu ni kama ifuatavyo mimi nina mume ambaye aliyeingia dini kitambo lakini amejifundisha quraan kama surah nne, tano, na hatii bidii kujifunza surah zingine bali yeye husoma tafsiri peke yake akisema ni sawa kama kusoma quraan, swali langu ni sawa hivyo? Ama niaje tafadhali nahitaji majibu. Jazakaallah kheir ALLAH SUBHANNA atupe kheiri Inshallah.


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mume asiyefanya bidii kusoma Qur-aan yenyewe kwa Kiarabu.

Hakika wengi hukosea katika mas-ala ya usomaji wakidhania kuwa kusoma tafsiri yake ni sawa na kusoma Qur-aan. Hili ni kosa na inafaa tujirekebishe ili tuwe ni wenye kupata thawabu zinazohitajika.

 

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Kila herufi ya Qur-aan ina thawabu kumi na wala sisemi kuwa Alif Laam Miym ni herufi bali Alif ni herufi, Laam ni herufi na Miym ni herufi”. Kwa hiyo, kwa kusoma Alif Laam Miym Muislamu anapata thawabu thelathini. Ukichukuwa mfano labda wa BismiLlaahi (Kwa jina la Allaah), kwa Kiarabu zipo herufi zifuatazo – Baa, Siyn, Miym, Alif, Laam, Laam na Haa, kwa ujumla hizi ni herufi saba ilhali ukiitafsiri katika Kiswahili utapata herufi za Kiswahili kumi na tano, yaani mara mbili ya asli yake.

 

Jambo lililo zuri ni Muislamu kufanya bidii kuweza kuisoma Qur-aan katika lugha yake ya asili na pia kujua maana kwani bila kujua maana huenda natija ya kufuata isiwe nzuri. Kwa kuwa anasoma tafsiri atakuwa mtu anapata thawabu ya kusoma mambo mema na mazuri. Hata hivyo, hahesabiwi kuwa amesoma Qur-aan.

 

Kwa hiyo, unatakiwa umueleze mume wako afanye bidii katika kujifunza kusoma ili apate kuweza kuisoma Qur-aan katika lugha yake ya asili na asome tafsiri ili aweze kujua maana na makusudio ili aweze kufuata maagizo yaliyo ndani na kuacha makatazo.

 

Bonyeza viungo vifautavyo upate maelezo zaidi:

 

Thawabu Kusoma Tafsiyr Au Kusoma Qur-aan Kwa Kiarabu?

 

Kusoma Qur-aan Kwa Maandishi Ya Kilatini Atapata Thawabu Sawa Na Mwenye Kusoma Qur-aan Kwa Kiarabu?

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share